To Chat with me click here

Monday, December 31, 2012

MBOWE AWAKUNA WATANZANIA


SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, kutangaza kutogombea urais mwaka 2015 na kwamba badala yake anajielekeza kupanga na kutekeleza mikakati kuhakikisha chama chake kinaingia Ikulu, Watanzania wamemuunga mkono wakisema ni mkomavu kisiasa.

Mbowe alihutubia mkutano jimboni Karatu juzi na kusema kuwa kazi yake itakuwa kusimamia kupata viongozi bora wa kupeperusha bendera ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Kauli hiyo ya Mbowe ilimaliza uvumi uliokuwepo kuwa huenda angegombea, ila aliweka bayana kuwa mgombea wao wa mwaka 2010, Dk. Willibrod Slaa, bado anatosha kugombea wadhifa huo kutokana na kazi nzuri aliyoifanya ya kuwapatia wabunge wengi.

Msimamo huo wa Mbowe, jana ulitawala katika mijadala ya wananchi kwenye mazungumzo ya kawaida na mitandao ya kijamii, huku wengi wakimuunga mkono na kudai si king’ang’anizi wa madaraka.

Wananchi hao katika mitandao ya kijamii walikwenda mbali zaidi wakiwataka hata viongozi wakuu wa vyama vingine vya upinzani, ambao wamewahi kuwania nafasi hiyo bila mafanikio makubwa, kutengeneza mkakati wa kuwaandaa wagombea wengine wanaokubalika zaidi yao.

Miongoni mwa viongozi waliotajwa kupoteza mvuto ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu wake Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, ambao wamegombea kiti hicho bila mafanikio mara nne mfululizo tangu mwaka 1995.

Akizungumza na Tanzania Daima, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alimpongeza Mbowe kwa hatua ya hiyo.
Dk. Bana alisema kuwa, Mbowe ameonesha ukomavu wa kutokuwa king’ang’anizi wa madaraka, jambo alilodai ni jema la kujipima mwenyewe na akatoa msimamo usiotiliwa shaka.

“Mbowe kwa sasa ni mwanasiasa pekee aliyeonesha upeo wa hali ya juu, na kweli anafaa kuwa kiongozi wa chama anachokiongoza, na tumemshuhudia akiongoza kwa ukomavu sio katika chama tu ila hata kambi rasmi ya upinzani bungeni,” alisema.

Aliongeza kuwa, kama anaweza aangalie wagombea mbalimbali kuwaandaa mapema na si kuwakurupua kama walivyofanya wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010 kwa kumkurupua Dk. Slaa.

Naye mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Bashiru Ally, alisema kuwa CHADEMA kimeonesha mfano, na hivyo CCM waige kwani suala la mbio za urais kupitia CCM limekuwa ni vita hadi limetikisa nchi.

“Watu wamechafuliana majina, wanakamiana kisa urais. CCM wanaumwa ugonjwa wa kutaja majina badala ya sifa za wagombea, kila siku ukiwauliza kama wanagombea au hawatagombea, watu hujibu majibu ya mkato, subiri nitaoteshwa au huwezi kuvuka daraja kabla ya kulifikia,” alisema.

Alisisitiza kuwa, kweli wanampongeza Mbowe na sasa wanamshauri atengeneze mchakato wa wazi wa kupata mgombea ambaye ataungwa mkono na Watanzania wengi.

“CHADEMA sasa kinakua kwa kasi, haijulikani ni kwanini japo watu wengi wanahusisha na uungwaji mkono na vijana na wasomi mbalimbali, hivyo ni wakati wa kuwafunda vijana wake ili wajue sifa za uongozi,” alisema.

Bashiru alisisitiza kuwa, vijana wanapaswa kujulishwa kuwa ujana si sifa ya mtu kuwa rais, kwamba kuna sifa zaidi ya ujana zinahitajika.

Katika mchango wake kwenye mtandao wa kijamii, mhadhiri mwandamizi wa UDSM, Dk. Azavery Lwaitama alisema kuwa Mbowe ametoa kauli ya kumuunga mkono Dk. Slaa ambaye kura zake zilichakachuliwa mwaka 2010.

“Kwa Mbowe kusema kuwa hatakuwemo katika kinyang’anyiro cha kugombea urais ndani ya CHADEMA, hivi ndani ya CCM kungekuwa hakuna ukomo wa urais si ningekuwa  nasikia maoni kama haya kuwa mgombea wa 2010 ndiye huyo wa 2015?” alihoji.

Aliongeza kuwa, hivi karibuni wakati wa uchanguzi wa UVCCM ililazimishwa kuwa mwenyekiti atoke Zanzibar na kwamba vile vile kwa Spika Anne Makinda ililazimishwa ili kumwengua Samuel Sitta.

“Tumpongeze Mbowe kwa kuondoa ubinafsi na kumtangaza mwenzake kuwa anatosha kwani si alishinda 2010 bwana, lakini kura zikachakachuliwa na wale wale ambao wamekuwa wanapanga na kutekeleza mipango ya kishetani ya kumuua Dk. Slaa ili kuuzima umaarufu wake na kuisambaratisha CHADEMA,” alisema.

Dk. Lwaitama aliongeza kuwa, CCM kwenyewe tayari Januari Makamba ameishatangaza kuwa lazima mgombea awe kijana na kwamba hata Rais Jakaya Kikwete aliishatangaza kuwa atakapotoka anataka akabidhi urais kwa mtu mwenye umri mdogo kuliko yeye.

“Nadhani tuwaache CHADEMA wapeane maelekezo wao kwa wao. Na tumpongeze Mbowe kwa kutanguliza masilahi ya chama chake na taifa kwa ujumla badala ya masilahi ya kwake binafsi,” alisema.

Alifafanua kuwa, sasa propaganda za CCM kwamba Mbowe naye anautaka urais zimetunguliwa hivyo na labda sasa zitabaki za Zitto Kabwe kuusaka urais.

Kwamba ikitokea Zitto akatamka kama alivyotamka Mbowe, basi nazo zitapeperushwa na upepo zibaki sasa propaganda za kumchafua Dk. Slaa.

No comments:

Post a Comment