CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM), kimewageuka wanachama wake waliotumwa kufungua kesi za
kupinga matokeo ya uchaguzi katika majimbo mbalimbali nchini, Tanzania Daima
Jumapili limebaini.
Uchunguzi
uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa waliofungua kesi kupinga ubunge wa
Godbless Lema mkoani Arusha, wametoswa na sasa wanakusudia kumwangukia mbunge
huyo kumwomba radhi ili awasamehe deni la uendeshaji wa kesi tangu mwanzo hadi
juzi Mahakama ya Rufaa ilipomrejeshea ubunge.
Baada
ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, CCM kupitia Katibu Mkuu wake, kwa wakati huo,
Yusuf Makamba, iliandika barua yenye kumbukumbu namba CCM/OND/636/VOL.11/122 ya
Novemba 9, 2010 kwenda kwa makatibu wake wa mikoa na wilaya kuwaamuru wote
walioshindwa katika uchaguzi wapinge matokeo, na kwamba chama kingewasaidia
gharama za uendeshaji wa kesi hizo.
Katika
barua hiyo, Makamba aliwataka wagombea wa ubunge kufungua kesi katika Mahakama
Kuu ya Tanzania, huku wagombea udiwani walioangushwa kufungua kesi katika
mahakama za mahakimu wakazi ndani ya siku 30, tangu ulipofanyika uchaguzi huo.
Katika
barua hiyo ambayo Tanzania Daima Jumapili ina nakala yake, Makamba aliwaagiza
makatibu wa CCM wa mikoa kwa kushirikiana na makatibu wa wilaya na kata
kuwasaidia wagombea walioshindwa kwenye uchaguzi kuandaa hoja za malalamiko na
vielelezo kwa ajili ya kupeleka mahakamani, huku akisisitiza kuwa “Chama Cha
Mapinduzi Makao Makuu kitachangia gharama za mawakili kwa wagombea ambao hawana
uwezo kifedha.”
Baadhi
ya wabunge wa upinzani walioshitakiwa na kesi zao kuhukumiwa na kuibuka
kidedea, hawajalipwa gharama za uendeshaji wa kesi hizo.
Mbunge
wa Mbozi Magharibi, David Silinde (CHADEMA) kupitia kwa wakili wake, Benjamin
Mwakagamba wa Kampuni ya uwakili ya BM ya jijini Dar es Salaam, alisema kuwa,
mdaiwa katika kesi hiyo, Dk. Lucas Siame (CCM) tangu aamriwe na mahakama
kulipa, amekuwa haonekani mahakamani au kuonesha dalili zozote za kulipa
gharama za uendeshaji wa kesi.
Wakili
huyo anasema kuwa, mdaiwa huyo ambaye alipinga matokeo, amekuwa akiishi kwa
kujificha maeneno ya Sinza, jijini Dar es Salaam.
Tanzania
Daima Jumapili lilimtafuta Dk. Siyame kupitia simu yake ya mkononi akapatikana,
ila alisema hajui utaratibu kama alipaswa kulipa au la.
“Mwandishi
hizo habari za kulipa ndio nazisikia kwako,” alisema lakini alikiri kuwa CCM
haikumsaidia uendeshaji wa kesi aliyofungua dhidi ya Silinde. Silinde,
alishinda kesi katika Mahakama Kuu ya Rufaa Kanda ya Mbeya, baada ya kufuta
shauri la kesi ya rufaa iliyopelekwa na Siame, aliyekuwa mgombea wa CCM, Mei 2,
mwaka huu.
Siame
aliyekuwa amekata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa Julai mosi, mwaka jana dhidi
ya uamuzi wa Mahakama Kuu uliompa ushindi mbunge huyo wa CHADEMA, alilazimika
kuomba mahakama kuondoa shauri hilo.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (CHADEMA)
ambaye naye alishinda kesi ya pingamizi iliyofunguliwa na Benson Mpesya (CCM),
alipoulizwa endapo amelipwa fidia kama ilivyoamriwa na mahakama, alisema kuwa
amelipwa sehemu ya fedha, na nyingine bado.
Sugu
alisema kuwa, hata hivyo Mpesya amekuwa akimtuma wakili wake kuonana na wa
kwake ili angalau amwongezee muda wa kulipa.
“Nimekuwa
mstaarabu sana, ningeweza kutafuta amri ya mahakama ili mali zake zikamatwe,
lakini alimtuma wakili wake nimvumilie,” alisema Mbilinyi.
Wakati
mzigo wa kulipa gharama ukiwaangukia wafungua kesi, waliomshtaki Mbunge wa Singida
Mjini, Tundu Lissu (CHADEMA) wanatafuta suluhu.
Walalamikaji
wawili waliokata rufaa dhidi ya Lissu, ambao kesi yao bado haijaanza
kusikilizwa, tayari wameshaanza kumtafuta mbunge huyo ili wafanye utaratibu wa
kuondoa kesi Mahakama ya Rufaa.
Akizungumza
kwa simu kutoka Muyanji-Makiungu, Singida, mlalamikaji wa kwanza katika kesi
hiyo, Shabani Selema alisema: “Natamani sana kuiondoa kesi hiyo mahakamani
ambayo Chama chetu Cha Mapinduzi kilishinikiza tukate rufaa, lakini kwa sasa
chama hakieleweki, sina haja tena na hiyo kesi, sitaki na ninataka kwenda
Dodoma nionane na wakili wetu angalau nichukue hata kitambulisho changu cha
mpiga kura kwani kilikuwa ni sehemu ya vielelezo, mimi nakuahidi kuwa nakuja
Dar es Salaam wakati wowote na nitamtafuta Lissu tukafute hiyo kesi.”
Alipohojiwa
inakuwaje ajitoe katika hatua hii ya rufaa, Selema alijibu: “Mwandishi kama
kuandika andika tu, mimi hii kesi sina hamu nayo, nimekuwa naiendesha mwenyewe,
hata familia yangu, rafiki zangu na wasomi mbalimbali sasa wananishangaa, chama
kimeniacha, kwanza wamenivuruga sana.”
Kwa
upande wake, Lissu alisema taarifa kwamba mlalamikaji wake anamtafuta ili
wafute kesi, amezisikia kutoka kwa wanafamilia yake.
Tanzania
Daima Jumapili iliwatafuta viongozi wa CCM Makao Makuu kuzungumzia suala hilo,
lakini simu zao hazikuweza kupatikana hewani huku simu ya Naibu Katibu Mkuu
bara, ikiita muda wote bila kupokelewa.
Kwa
upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda alipopigiwa simu
hakuweza kupokea, lakini baadaye alimpigia mwandishi na kumuuliza: “wewe nani?”
Mwandishi
alipojitambulisha kwamba anatoka Tanzania Daima Jumapili, Chatanda alisema:
“Kama wewe ni wa Tanzania Daima, nipigie sina haja ya kukupigia.”
Baada
ya kusema hayo akakata simu, na alipopigiwa tena, simu ilikuwa tayari imefungwa
- haikupatikana tena.
No comments:
Post a Comment