DK. SLAA ADAI JK
ANAMLINDA IGP MWEMA
HOJA nzito zinazoendelea kuibuliwa na
viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuhusu
utendaji wa Rais Jakaya Kikwete, zinaonekana kuwa mwiba na kuikoroga serikali
yake.
Wakati hoja ya Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu, ya uteuzi wa baadhi ya majaji wasio na sifa ikiwa bado
haijapatiwa majibu ya kuridhisha, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa,
naye amepigilia msumari mwingine akisema Rais Kikwete anamlinda Mkuu wa Jeshi
la Polisi, IGP Said Mwema.
Dk. Slaa aliibua hoja hiyo wakati
akizungumzia mauaji mbalimbali yanayodaiwa kufanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya
raia wema, akisema hali hiyo ni matokeo ya IGP Mwema, kulindwa na mkuu wake, na
hivyo kushindwa kuwachukulia hatua wahusika.
Wakati hoja hizo zikiibuliwa, wasaidizi
waandamizi wa Rais Kikwete wakiwemo mawaziri na watendaji wengine, wameonekana
kupwaya, wakishindwa kuhimili mikiki ya kutoa majibu yenye kufafanua kile
kinachohojiwa.
Akizungumza jana jijiji Dar es Salaam,
wakati akifungua mkutano mkuu wa chama hicho Jimbo la Kinondoni, Dk. Slaa
alisema kama IGP Mwema anashindwa kuchukua hatua juu ya matatizo
yanayojitokeza, ikiwamo mauaji na kujeruhi wanayofanyiwa wananchi na polisi,
rais anapaswa kuchukua hatua kwa lengo la kuiokoa nchi.
Huku akirejea matukio kadhaa ya mauaji
na mateso mbalimbali yaliyofanyika katika mikoa ya Tabora, Morogoro, Iringa,
Arusha, Mara, Mwanza, Mbeya, Dar es Salaam na maeneo mengine, Dk. Slaa alisema
sheria zipo wazi juu ya suala hilo katika kuunda tume ya kimahakama katika
kupata ukweli wa madhila hayo.
“Nyote mnajua kuwa haki katika nchi
yetu imekuwa bidhaa adimu, matukio ya kutisha yanajitokeza kila siku, viongozi
wenye dhamana na maisha yetu wanakaa kimya, katika hili kama rais hajui sheria
si ana watu wanaomsaidia, hivi haoni hata haja ya kuunda tume huru ya
kimahakama?” alihoji.
Alisema kuwa kutokana na ukimya wa
rais, ikiwa ni pamoja na kushindwa kuwachukulia hatua Waziri wa Mambo ya Ndani,
IGP Mwema, makamanda wa polisi wa mikoa ya Iringa na Morogoro, CHADEMA
watakutana kabla ya Krismasi na kutoa msimamo wa nini kifanyike kutetea haki ya
wananchi.
Dk. Slaa alisema madhumuni ya CHADEMA
ni kukuza, kulinda na kutetea haki za binadamu, hivyo wanapaswa kuhakikisha
wanafuatilia ukandamizaji wa watu katika misingi ya rangi jinsia, ukanda, rika
na itikadi, jambo alilodai limewashinda CCM.
“CCM leo kila wanaposimama wanaomba
waendelee kuungwa mkono ili watawale…wameacha yale yaliyo katika katiba ya nchi
na kusahau maandiko yaliyo nyuma ya ilani ya chama,” alisema.
No comments:
Post a Comment