Ndg. Kattikiro katika moja ya harakati zake za kisiasa |
Maxmillian Kattikiro Blog inapenda kuchukua
nafasi hii kuwakumbusha wananchi wote kuwa, mwisho wa kutoa maoni juu ya katiba
mpya umekaribia (20th December 2012), hivyo kila mtu anaalikwa
kuendelea kutoa maoni yake juu ya katiba mpya, kwani ni haki ya kila mwananchi
kushiriki/kushirikishwa katika mchakato mzima wa kuundwa kwa katiba mpya.
Kama
haukupata nafasi ya kutoa maoni juu ya katiba mpya wakati kamati ya kukusanya
maoni ilipopita katika maeneo yako, Maxmillian Kattikiro Blog, tunakukumbusha kuwa
bado unaweza kuendelea kutoa maoni kwa njia zifuatazo;-
1.
Kwa njia ya barua pepe (e-mail): katibu@katiba.go.tz
2.
Kwa barua za posta, kwa anuani ifuatayo:
S. L. P. 1681, Dar-Es-Salaam, Tanzania.
3.
Maoni katika tovuti ya kamati ya katiba mpya. Fuata link hii hapa ili kutoa
maoni yako;
Hakikisha
unashiriki, ni haki ya kila mwananchi (wale waishio nnchi/hata nchi za
nje). Pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kweli, na maendeleo katika nchi yetu
kwa kutoa michango mihimu ambayo itakuwa ni mwongozo wa uwajibikaji kwa wote
walio na dhamana ya kuwatumikia wananchi.
Haya ni maoni yangu
ambayo pia niliyatoa kwa njia ya Mtandao siku chache zilizopita:-
1. Nimeshauri kuwa Katiba ijayo ijaribu kupunguza mamlaka aliyopewa Rais,
pamoja na shughuli zake. Mfano: Rais kuwa ni mwenye dhamana na kauli ya mwisho
juu ya Ardhi pamoja na mambo mengine ambayo yangeweza kufanywa hata watendaji
wa ngazi nyingine mfano mawaziri n.k
2.
Nimeshauri kuwa Katiba ijayo, ni
lazima ieleze au itoe mamlaka kwa
wananchi juu ya kuwawajibisha viongozi wa umma hususani wale waliowachagua
kuwaongoza mfano: Wabunge. Naamini wazi kuwa kama wananchi watakuwa na
mamlaka hayo, basi utendaji na uwajibikaji wao kwa wananchi utakuwa ni wa tija
kwakuwa watakuwa moja kwa moja wanawajibishwa na wananchi wenyewe. Hili
litachochea kasi ya maendeleo na kupunguza mzigo wa watumishi wazembe ambao si
watendaji wanosubiri posho ambazo ni pesa za walipa kodi wa Taifa hili.
3.
Nimeshauri pia, Katiba ijayo ihakikishe kuwa Kinga ya Rais kushitakiwa inaondolea.
Kwa kumwekea Rais kinga ya kumshtaki hata baada ya kuondoka madarakani kumekuwa
kunaliumiza Taifa letu, kwani tumeona jinsi baadhi ya marais wetu wastaafu
jinsi walivyoweza kujilimbikizia na kujimilikisha mali za umma, tumeona pia jinsi
walivyoliingizia taifa hasara kwa kubariki na kukubaliana na mikataba ya “KISANII”
ambayo imeligharimu taifa letu mno. Na haya yote ni kwa sababu huamini kuwa
hakuna madhara watakayoyapata baada ya kumaliza vipindi vyao vya utawala.
Lakini kwa nchi change kama Tanzania tunapaswa kutokubaliana wala kuunga mkono
swala hili la kinga kwani tumeona kwa baadhi ya nchi nyingine za kiafrika
zilivyoweza kuwaburuza marais wao mahakamani kwa tuhuma za ufisadi, ubadhilifu,
matumizi mabaya ya ofisi za umma n.k
4.
Ardhi:
Kwa mujibu wa katiba ardhi ni mali ya wananchi, na ndiyo maana hata ikitokea
serikali au mwekezaji anahitaji sehemu ya ardhi ya wananchi Fulani huwapa fidia.
Hivyo katiba mpya inapaswa kuonesha na kuzingatia hilo kuwa ardhi ni milki
halali ya wananchi na ikiwa wananyang’anywa au kuondolewa katika ardhi hiyo
basi wanapaswa kutendewa nini kama fidia. Hili litazuia unyanyaswaji wa
wananchi ambao umekuwa ukiendelea nchini kwa baadhi ya matajiri kujiamuli
kujitwalia ardhi ya wananchi huku wakikingiwa kifua na viongozi wa umma kwa
dhana ya uwekezaji. Sheria ya ardhi lazima irekebishwe na itoe mamlaka na
vipaumbele kwa wazawa na wageni kama ilivyo sasa.
5.
Matumizi
mabaya ya ofisi za umma (Madaraka) pamoja na ubadhilifu ma rasilimali za Taifa:
Katiba ijayo ni vyema ikaeleza wazi juu adhabu ya matumizi machafu ya ofisi za
walipa kodi na rasilimali zetu tulizonazo. Tungependa kuona hawa wanaopewa
mamlaka kuongoza au kusimamia rasilimali za taifa wanafanya hivyo tena kwa moyo
wa uzalendo kwa manufaa ya Taifa zima na vizazi vyetu vijavyo na sisi wao na
familia zao pekee. Rasilimali zetu zimekuwa zikimilikishwa kwa wageni wachache,
na kuibwa huku watanzania tukiendelea kuwa maskini siku hadi siku, hii yote ni
kwakuwa hakuna sheria iliyowazi na inayosimamia moja kwa moja rasilimali hizi
na mamlaka ya watawala wetu.
6.
Umri
wa kugombea nafasi ya Urais: Katiba ijayo ni vyema ikashusha
kiwango cha umri unaoruhusiwa kwa mtu kugombea urais, nimependekeza iwe ni
kuanzia miaka 35 na kuendelea. Kwani naamini kabisa kuwa vijana wa sasa
wanauwezo na mitazamo chanya inayoendana zaidi na mabadiliko ya Sayansi na
Teknolojia kuliko ilivyo kwa watu wa umri mkubwa zaidi. Naamini kuwa tunaweza
kukwamuka toka kwenye umaskini huu uliokithiri kama tu, tutaweza kubadili mfumo
wa uongozi uliopo madarakani na unoendesha nchi yetu kwa sasa. Hili limeonekana
kushindikana na wazee waliowengi hususani walio madarakani, kwani wao pia
wamekuwa ni sehemu ya huo mfumo kwa kipindi kirefu sasa.
7.
Muda
wa utumishi wa Wabunge: nimependekeza kuwa kuwe na
ukomo wa utumishi bungeni kama vile ilivyo kwa rais, lakini tofauti hapa ni
hivi, wabunge wakae madarakani kwa muda wa miaka kumi tu kisha baada ya hapo
wasiruhusiwe kugombea jimbo hilo hilo kwa mara nyingine. Wataruhusiwa kugombea
ubunge kwa kupitia jimbo lingine tu. Kwanini hivi: ikiwa mbunge atakuwa
amefanya mazuri kwa jimbo lake ndani ya miaka 10 basi yeye anaweza kukubalika
kwingine kokote kwani atakuwa anaaminika kwa uchapa kazi wake. Lakini kama si
mchapa kazi basi haina sababu ya kuendelea kuwa naye kwani ni mzigo na namna
hii ya wabunge wamekuwa wakitumia pesa za walipa kodi pasipo manufaa yeyote kwa
wananchi. Hivyo hawatastahili kurushwa bungeni baada ya miaka hiyo 10.
Kumbuka, kila mmoja
ana haki ya kutoa maoni yake binafsi bila kushinikizwa, hivyo haya ni maoni
yangu binafsi ambayo nimeyatoa kwa utashi wangu timamu bila shinikizo toka kwa
mtu, taasisi, wala kikundi fulani cha watu. Naamini yataheshimiwa na
kuzingatiwa kama moja ya mochango muhimu ili kufikia malengo na mategemeo ya
watanzania katika kupata katiba mpya.
No comments:
Post a Comment