CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), kimetangaza mkakati mzito kwamba mwaka 2013 utakuwa ni wa
kuunganisha nguvu ya umma kitaifa, kuishinikiza serikali ya Rais Jakaya Kikwete
kutoa tamko juu ya kuundwa tume huru ya kimahakama, itakayochunguza ya mauaji
mbalimbali ya utatanishi yaliyotokea nchini katika kipindi cha zaidi ya mwaka
mmoja uliopita.
Mbali na kuunganisha nguvu ya umma,
chama hicho pia kimeazimia kuitumia kambi rasmi ya upinzani bungeni kutumia
njia za Kibunge kupitia hoja binafsi au muswada binafsi kuwasilisha bungeni
mapendekezo ya marekebisho ya Katiba ya mpito kuhakikisha Tume Huru ya Uchaguzi
na marekebisho ya sheria zinazosimamia uchaguzi, yanafanyika kabla ya Katiba
Mpya.
Tamko la maazimio hayo yalitolewa jana
jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, wakati
akizungumza na waandishi wa habari juu ya maazimio ya mkutano wa Kamati Kuu ya
chama hicho, uliofanyika Desemba 15-16 mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Katika maazimio hayo yapatayo 10, Mbowe
alisema baada ya chama hicho kumuandikia Rais Jakaya Kikwete barua ya kutaka
tume huru ya kimahakama juu ya mauaji yenye utata, ikiwamo la kuuawa kwa
mwandisahi wa habari wa Kituo cha Chanel Ten, Daudi Mwangosi, Ikulu haikutoa
jibu lolote la kuwafahamisha wananchi nini kinaendelea.
“Mtakumbuka 9/9 mwaka huu tulimuandikia
Rais Kikwete barua tukimtaka aunde tume huru ya kimahakama na hata tulipokutana
naye, tulimuelezea umuhimu wa suala hili na akaahidi kushughulikia lakini hadi
leo kimya sasa tutalirudisha suala hili kwa wananchi,” alisema Mbowe.
Alisema kuanzia Januari mwakani
kutakuwa na mipango mipya ya kisiasa ambayo ni kuhamasisha umma kuishinikiza
serikali kuchukua hatua katika masuala ya msingi.
Kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
Mbowe alisema iliyopo haifanyi kazi kwa maslahi ya wananchi bali kwa ajili ya
chama tawala huku akitolea mfano wa kushindwa kuitishwa kwa uchaguzi wa
madiwani wa kata 13 kwa muda wa miaka miwili licha ya maeneo hayo kuwa wazi na
sheria inaeleza kuwa siku 90 zikifika, lazima uchaguzi uitishwe katika maeneo
yaliyokosa viongozi kwa sababu mbalimbali.
Aliongeza kuwa katika maeneo ambayo CCM
ina kila sababu za kushindwa, NEC imekuwa ikibeba jukumu la kuokoa jahazi kwa
kuacha kuitisha uchaguzi na kuwafanya wananchi kukosa wawakilishi.
Alisema kutokana na hali hiyo, CHADEMA
haitaibembeleza serikali kuwajibika bali watawafahamisha wananchi umuhimu wa
kuheshimiwa na kupewa uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa bila kuingiliwa na Tume
ya Uchaguzi.
“Tume itaarifiwa juu ya kucheleweshwa
kwa chaguzi za marudio za udiwani, mitaa, vijiji na vitongoji katika maeneo
mbali mbali, sisi CHADEMA tumeazimia kuunganisha nguvu ya umma kufanya
shinikizo la kisiasa kwa mamlaka zinazohusika kutangaza nafasi kuwa wazi ili
wananchi waweze kupata wawakilishi kwa wakati,” aliongeza Mbowe.
Kuhusu uboreshwaji wa daftari la wapiga
kura, Mbowe alisema Kamati Kuu imezingatia hatua ya serikali na Tume ya Taifa
ya Uchaguzi kukwepa wajibu wa kuboresha daftari hilo hivyo kuwanyima wananchi
haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika marudio ya uchaguzi zinazofanyika katika
maeneo mbalimbali.
Kutokana na hali hiyo Mbowe aliongeza
kuwa Kamati Kuu (CC) imeazimia kambi rasmi ya upinzani bungeni inayoongozwa na
CHADEMA ichukue hatua za kibunge kuhakikisha daftari hilo linaboreshwa mwaka
2013 kwa kile alichoeleza kuwa mwaka 2013 daftari hilo litatumika kwenye kura
za maoni ya Katiba mpya.
Akizungumzia mchakato wa upatikanaji
Katiba mpya mwaka 2014, Mbowe alisema Kamati Kuu imebaini upungufu katika
mchakato mzima unaoendelea ya kukusanya maoni, hali aliyoelezea kuwa inaweza
kukwamisha upatikanaji wa Katiba mpya bora mwaka 2014 kama ilivyotangazwa na
serikali na tume husika.
Alisema wameazimia kwamba kamati ndogo
ya Kamati Kuu ikutane haraka na kufanya tathmini zaidi na kutoa taarifa kwa
umma na pia ipendekeze kwenye tume maoni ya CHADEMA ya kuzingatiwa katika
Katiba mpya.
“Katika hili hatutanii mpaka sasa
hakuna chama kinachojua kitaingia katika uchaguzi wa mwaka 2014 wa serikali ya
mitaa na ule wa mwaka 2015 tukiwa katika mfumo gani; ni wakati muafaka wa
kujadili mustakabali wa taifa na tusifungwe na hoja kuwa mambo hayo yasubiri
katiba mpya,” alisema Mbowe.
Alisema ni wakati wa kuwa na muafaka wa
kitaifa juu ya mfumo ambao hata Katiba mpya itakuwa imeufuata na kutolea mfano
tatizo la kuzuiwa mijadala inayoendelea visiwani Zanzibar.
Alisisitiza kuwa wakati huu wa
kuisubiria Katiba mpya ni vema taifa likaangalia masuala mbali mbali yanayogusa
maisha ya Watanzania kila siku ambayo hayahitaji kusubiri mchakato wa Katiba
mpya.
Kuhusu hali ya kisiasa, Mbowe alisema
Kamati Kuu ilitaarifiwa kuhusu hoja binafsi zilizowasilishwa na wabunge wa
(CHADEMA) Halima Mdee (Kawe) juu ya ugawaji holela wa ardhi na Zitto Kabwe
(Kigoma Kaskazini), kuhusu fedha zilizofichwa nje ya nchi pamoja na kusudio
lililotolewa na Tundu Lissu (Singida Vijijni), kuhusu hoja ya uteuzi wenye
kasoro wa baadhi ya majaji na kwamba wameazimia kambi rasmi iifuatilie kwa
karibu serikali kuhusu hoja hizo.
Akizungumzia kile kinachodaiwa kuna
mgogoro wa CHADEMA wilayani Karatu, Mbowe alisema baada ya kupokea taarifa ya
kamati waliyounda kufuatilia na kuchunguza hali hiyo, wameamua kuisimamisha
kamati nzima ya utendaji ya chama hicho katika wilaya hiyo na kuiweka wilaya
hiyo chini ya uangalizi wa Kamati Kuu Taifa mpaka hatua zingine
zitakapochukuliwa.
Kuhusu serikali ya Chama cha Mapinduzi
kutekeleza sera za CHADEMA, Mbowe alisema Kamati Kuu imezingatia kuwa hatua
hiyo ni uthibitisho wa ziada kuwa CHADEMA ina sera nzuri na kwamba propaganda
za CCM haziwezi kufanikiwa.
Alisema kutokana na hali hiyo ni wazi
serikali ya CCM haiwezi kuzitekeleza kwa ufanisi sera hizo na kwamba kuna haja
ya CHADEMA kuongeza nguvu kwa ajili ya kuzisimamia sera zake kwa umakini
itakaposhika madaraka ya kuongoza serikali za mitaa mwaka 2014 na Serikali Kuu
2015
No comments:
Post a Comment