Dr. Slaa |
MKAKATI wa
kumchafua Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, unaoratibiwa na baadhi ya
viongozi waliotimuliwa kwenye Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA),
umedaiwa kufadhiliwa na CCM, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Vijana hao
ambao wamedaka kauli ya uzushi ya Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa wa CCM,
Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kuwa Dk. Slaa anamiliki kadi ya chama hicho na
anaendelea kuilipia, wanazunguka mikoani wakimchafua kiongozi huyo wakidai
ajiuzulu.
Licha ya
vijana hao kufukuzwa uongozi na wengine kuvuliwa uanachama, lakini bado
wameendelea kufanya mikutano na waandishi wa habari wakijipachika nyadhifa za
BAVICHA, wakidai kuwa wanaandaa maandamano ya kumng’oa Dk. Slaa.
Hata hivyo,
Tanzania Daima Jumapili limefahamishwa kuwa, mkakati wa vijana hao tayari
umefichuliwa na CHADEMA na kubainika kuandaliwa na CCM ili kuendeleza hoja hiyo
ya Nape ya kumchafua Dk. Slaa.
Chanzo chetu
cha ndani kinaeleza kuwa, kasi ya Dk. Slaa kwa sasa inawatia kiwewe CCM, hivyo
chama hicho kupitia kwa Nape kimelazimika kuwatumia mamluki hao kikidhani
kinaweza kufifisha nguvu ya CHADEMA mikoani.
Tayari Dk.
Slaa amefafanua hoja ya Nape akieleza kuwa kadi ya CCM ameendelea kubaki nayo
kama mali yake na kumbukumbu kwa wajukuu zake, huku akikanusha madai ya
kuilipia akisema ni jambo lisilowezekana kisheria.
Pia
mwanasheria maarufu jijini Arusha, Method Kimomogoro, naye alijitokeza kutoa
ufafanuzi wa kisheria, akisema kuwa kadi ya chama ni mali ya mwanachama, hivyo
ana hiari ya kuirejesha akihama au kubaki nayo.
Kimomogoro
aliongeza kuwa, wanaohama na kusalimisha kadi zao, wanafanya hivyo kwa mapenzi
yao na kutaka kuonekana, lakini hakuna mahala wanakotakiwa kufanya hivyo
kisheria.
Wakati
wasomi mbalimbali wakijitokeza kuipinga hoja ya Nape, kada huyo aliibuka na
kujikanyaga kwenye mtandao wa kijamii, akidai kuwa hakumlenga moja kwa moja Dk.
Slaa, bali baadhi ya viongozi wa upinzani akiwemo yeye, wanaendelea kumiliki
kadi za CCM.
Kwa kile
kinachoonekana kuwa propaganda hiyo iliibuliwa makusudi kwa ajili ya
kumdhoofisha Dk. Slaa, inadaiwa kuwa CCM imefanya mazungumzo na kuwawezesha
kifedha baadhi ya vijana waliofukuzwa BAVICHA ili wabebe ajenda hiyo na
kuieneza mikoani, ionekane kuna mgogoro ndani ya CHADEMA.
Tayari
vigogo wa juu wa CHADEMA wamethibitisha kuudaka mkakati huo wa CCM ulioasisiwa
na Nape na kueleza kuwa, unaratibiwa kwa kutumia fedha za mafisadi.
“Hao
wanafanya kazi ya Nape wakidhani wataisaidia CCM…ila kwa kuwasaidia tu kama
hawana taarifa kuhusu Dk. Slaa, waje makao makuu tutawaelimisha kuliko uongo
huo wanaoufanya,” alisema mmoja wa viongozi wa CHADEMA.
Naye kada wa
chama hicho, Arcado Ntagazwa aliyewahi kuongoza wizara mbalimbali ikiwemo Idara
ya Usalama wa Taifa katika utawala wa awamu zilizopita, alisema CCM kamwe
hawawezi kufanikiwa kwa ajenda hiyo.
“Unajua tena
wenzetu wana fedha za mafisadi, hivyo kutokana na vijana wetu kukosa ajira,
wameamua kuwarubuni na kuwazungusha mikoani ili kumpaka matope Dk. Slaa,”
alisema.
Ntagazwa
alisema kuwa wala CHADEMA hawahitaji kupoteza muda kuzunguka kukanusha uongo
huo wa CCM, na badala yake wawapuuze tu kwa vile hawawezi kumsambaratisha Dk.
Slaa.
Wiki iliyopita, Ntagazwa alizungumza na gazeti hili akisema CCM inababaishwa na nyota ya Dk. Slaa, hivyo viongozi wake na serikali wamejikuta wakibabaika na kufanya vitendo vya ajabu wakidhani wataweza kumzuia.
Ntagazwa
alieleza kushangazwa na kiwewe wanachokipata viongozi wa serikali na CCM kwa
Dk. Slaa, ambaye alidai nyota yake inazidi kung’ara kwa wananchi licha ya
juhudi kubwa ya kujaribu kumchafua.
“CCM
wanamwona Dk. Slaa ni tishio kwao, hivyo katika kubabaisha watu wanadhani
watapunguza imani kwake, wameibua mambo ya ajabu na kupoteza muda kama
alivyofanya Nape kudai kuwa hajarudisha kadi ya CCM,” alisema.
Alisema kuwa
kwa sasa CCM wanashindwa kutambua kwamba mambo yamebadilika, Watanzania
wanachuja na kuchambua mambo si kama ilivyokuwa zamani.
“Hili jambo
la kupotoka na kushindwa kusimamia misingi na kuwatetea wanyonge, ndilo Dk.
Slaa pia amekuwa akilikemea kwa baadhi ya viongozi na wafuasi wa CHADEMA, ambao
wamegeuka kucheza ngoma ya mafisadi wa CCM,” alisema.
Ntagazwa kwa
kujiamini alisema kuwa, katiba za TANU na CCM ziliandikwa vizuri na kuwekwa
mambo ya msingi, lakini akasikitika na kuhoji ni pepo gani amewaingilia
viongozi wa CCM sasa na kushindwa kusimamia mambo hayo.
“Wanachokifanya
CCM sasa ni tofauti kabisa, yaani sawa na ardhi na mbingu. Wanafanya mambo ya
ajabu kwa wananchi na hadi kufikia kuibua mambo ya ajabu kama alivyofanya
kijana wao (Nape),” alisema.
Aliongeza
kuwa, kwa sasa wanamshukuru Mungu kwani wananchi wanajionea jinsi CCM
ilivyoshindwa kurejesha misingi, na badala yake imehamia kushirikiana na
serikali kufanya vitendo vya hovyo kwa kutumia polisi na vyombo vingine vya
dola.
Mpaka sasa
wamejitokeza vijana wawili walioenguliwa ndani ya BAVICHA na kufanya mikutano
na waandishi wa habari, wakijipachika vyeo vya ukatibu wa mikoa wa baraza hilo
na kudai wataongoza maandamano ya kumng’oa Dk. Slaa.
Vijana hao
ni Edo Mwamalala wa Mbeya ambaye hata hivyo CHADEMA mkoani humo ilithibitisha
kuwa ilikwishamtimua uanachama, huku Salvatory Magafu naye akiibuka juzi mkoani
Mwanza akijitambulisha kama Katibu wa Mkoa BAVICHA wakati uongozi wao ulivunjwa
muda mrefu.
Katika
harakati hizo za kueneza propaganda hiyo ya kuonesha kuna mgogoro ndani ya
CHADEMA, inadaiwa kuwa baadhi ya vyombo vya habari vimepenyezewa fungu
kuhakikisha vinaandika habari za kukisambaratisha chama hicho.
No comments:
Post a Comment