To Chat with me click here

Wednesday, August 7, 2013

SERA, ITIKADI ZA VYAMA ZIKAE KANDO, KATIBA MALI YA WATANZANIA WOTE



Zanzibar.  Mabaraza ya Katiba yaliyosimamiwa na Tume ya Katiba kwa sehemu kubwa yametupa picha ya namna watu walivyokuwa wameyafikiria. Ingawa Tume ilitoa muongozo, wengi hawakuusoma au nisema hawakutaka kuelewa.

Tulichokiishuhudia ni baadhi ya wajumbe kutoka katika vyama vya siasa kushiriki katika mabaraza wakiwa na waraka mfukoni wenye maelekezo ya vyama vyao!

Ni jambo la kushangaza, lakini ndio demokrasia yenu ilipofikia kwamba watu wazima wanashindwa kujenga hoja wenyewe aina ya katiba wanaitakayo, wanasubiri kulishwa maneno kutoka kwa wanasiasa.

Ninaipongeza Tume ya Jaji Warioba kwa kuwa haikuruhusu taratibu na miongozo iliyowekwa na Tume hiyo kuvunjwa kwa makusudi, muda wote walisimama kwenye upande wa haki na pale alipozuka mtu akiwa na “waraka” wenye maelekezo alipigwa ‘stop’, ili aeleze ya kwake.

Siku chache baada ya kuanza kwa mabaraza tulimsikia Jaji Warioba akiwakosoa wajumbe wa mabaraza hayo waliokuwa wakienda  na matamko au nyaraka za vyama, badala ya maoni ya wananchi waliowachagua.

Inavyoelekea baadhi ya watu bado wana mawazo kuwa mfumo wa chama dola unaendelea katika nchi yetu na inawezekana mfumo huo umewalemaza baadhi ya watu kiasi cha kuingia woga hata katika yale mambo yenye uhusiano wa maisha ya kila siku.

Bado wanafikiri chama kushika hatamu katika wakati huu wa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Wanasahau kuwa Katiba ni mali ya wananchi, na ni wao wenye haki na mamlaka ya kueleza wanataka namna gani nchi yao iongozwe.

Wananchi ndio wenye uamuzi wa mwisho kuamua Katiba yao iweje na wala sio watawala wala vyama vya siasa vinavyoweza kujigeuza au kupora mamlaka na nguvu za wananchi.

Kwa maana hii sera za vyama vya siasa hazina upenyo wa kwenye suala zima la Katiba Mpya maana wananchi wanaweza hata wakasema kwa mfano hawaoni ulazima wa kuwepo kwa vyama vya siasa na badala yake wakapendekeza aina nyingine ya mifumo ya kidemokrasia ambayo inakubalika.

Sisemi kuwa tuachane na vyama vingi, la hasha, isipokuwa ninachora picha kwamba nguvu ya mwisho ya uamuzi katika nchi yeyote ya kidemokrasia ni kwa wananchi wenyewe.

Tunasimama pamoja na Tume ya Jaji Warioba kwa kitendo chao cha ushupavu katika kuona Taifa letu linapata Katiba ambayo inatokana na matakwa ya wananchi badala ya wanasiasa.

Kamwe tusikubali kufanya mambo kwa ajili ya maslahi ya muda mfupi, lazima tutangulize uzalendo kwa ajili ya kupata Katiba bora inayotokana na matakwa ya watu wenyewe na sio kundi fulani.

Ni wajibu wa wajumbe wa mabaraza ya Katiba kujiepusha na makundi maslahi kwa kuwa mwisho wa siku hata wao watakuja kuona uzuri au ubaya wa Katiba waliyoiandika.

Katika hili pia sina budi kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa nyakati tofauti amekuwa akisisitiza uhuru wa mawazo, kwamba kila mtu atoe mawazo yake mwenyewe bila ya woga wala wasiwasi.

Ni wajibu wake akiwa Rais wa watu wote kusimamia sheria na taratibu za nchi tulizojiwekea. Hapa Zanzibar wamejitokeza baadhi ya wajumbe wa mabaraza ya katiba wakiwa na maelekezo ya vyama vyao vya siasa, lakini tunashukuru Mungu Tume imesimama imara kuwaeleza haja ya wajumbe kuboresha Rasimu ya Katiba kwa mtazamo wao.
 
Sitaki kuamini kuwa mchakato wa Katiba tulioanza tangu mwaka jana ni kiini macho au kupoteza wakati na fedha, siamini hivyo kwa sababu suala la kuwa na Katiba mpya limepigiwa kelele siku nyingi,l akini pia tukiwa watu wazima hatuna sababu ya kudanganyana kwani Serikali ingeweza kujifungia na kuandika Katiba wanayoitaka kisha kuipeleka bungeni.

Kwa kuwa nchi yetu inaongozwa na Katiba na sheria pamoja na viongozi wenye dhamira ya dhati ya uongozi wao, hatuwezi kufanya mchezo wa aina hiyo ambao hauna faida kwao wala kwetu.

Ndio maana Rais Kikwete hakutoa matamshi ya kuwashurutisha wananchi kutoa maoni na mapendekezo yanayotakiwa na chama chake wala Serikali. Na wala serikali zote mbili –Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya  Mapinduzi Zanzibar hazikuwa na na msimamo wake katika suala la kupata Katiba mpya, wametuachia wananchi tuamue.
 
Ingekuwa Serikali ina maoni yake katika suala hili au ingetaka sera ya chama tawala ndio kiwe msingi wa kuandika Katiba mpya ingefanya hivyo na mambo kadhaa yangetokea;

Mosi, utoaji maoni ungekuwa ni wa kiini macho na kwamba Katiba hiyo isingekuwa imebeba matakwa ya wananchi bali maslahi ya watawala na kikundi fulani cha watu.

Suala la pili, hii ingedhihirisha kuwa wananchi bado lepe la usingizi halijawatoka, woga umetawala miongoni mwao na wanadhani Serikali ni mali ya watawala na kwamba mamlaka ya uendeshaji nchi haitoki kwao.

Hata hivyo, ukweli ni kuwa mamlaka ya uendeshaji nchi ni kwa wananchi wenyewe, lakini kwa kutokufahamu namna ya jinsi Serikali inavyopaswa kuendesha mambo yake au kwa sababu ya kutokujiamini kunakoambatana na utashi wa maslahi binafsi, baadhi ya watu wanaweza kuyumbishwa na wanasiasa au makundi maslahi.

Wapo wanasiasa na hata makundi maslahi yalijaribu kutaka kujipenyeza kwenye akili za wananchi, lakini hawakuweza kuwashawashi waliowengi na badala yake tumeona namna watu walivyotoa mawazo yao katika Tume ya Jaji Warioba.

Ni busara ya kawaida kwa wananchi tukaelewa kwamba vyama vyetu vya siasa havina mamlaka ya kuifanyia Katiba ya nchi mabadiliko, zile enzi za mfumo wa chama kimoja zimeshapitwa.

No comments:

Post a Comment