Aliyekuwa msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwakwe. |
Dar
es Salaam.
Aliyekuwa msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa amesema Rais
Jakaya Kikwete aliteleza kueleza msimamo wake na ambao baadaye ulibainika kuwa
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati akizindua Bunge Maalumu la Katiba, Machi
21.
Tendwa,
ambaye alistaafu Agosti mwaka jana na nafasi yake kuchukuliwa na Jaji Francis
Mutungi, alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini
kwake jijini Dar es Salaam.
Tendwa,
ambaye alikuwa Msajili kwa miaka 13, alisema akiwa kiongozi mkuu, Rais Kikwete
alipaswa kutoa mwongozo wa uendeshaji wa Bunge Maalum la Katiba.
“Sikuwapo
nchini, lakini kwa kadri ninavyoelezwa, kama hiyo ni kauli yake, basi
alijisahau kusemea msimamo wa chama chake, (CCM) na sera yake ya serikali mbili
katika bunge hilo,” alisema.
“Rais
ni mtendaji, alipaswa kutoa guidelines (miongozo) ya jinsi ambavyo Bunge Maalum
la Katiba linatakiwa kufanya. Alichokisema, aliteleza.
“Alijisahau
na kurudi kwenye chama kwa sababu hiyo ndiyo sera ya chama chake, ” alisema
Tendwa.
“Na
siyo yeye tu (Kikwete) kwani nimemsikia hata Dk Shein (Rais wa Zanzibar na
mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi), akisema kuwa msimamo wa CCM ni serikali
mbili,” aliongeza Tendwa.
“Nimemsikia
Makamu wa Pili wa Rais (Balozi Seif Ali Iddi) akisema hivyo na Rais
wangu (Kikwete) katika mikutano mbalimbali ya hadhara, naye amelisema hilo.”
Madai
ya kuibeba CCM
Tendwa
ambaye katika uongozi wake wa miaka 13 alikuwa akituhumiwa mara kwa mara na
vyama vya upinzani kuwa anakibeba chama tawala, alisema: “Nadhani na yeye (Rais
Kikwete) kasema. Nadhani alijisahau kuwa ni kiongozi wa taifa.”
“Rais
ni mtendaji na mimi nasema aliteleza. Turudi katika hoja kwa kujadili rasimu
iliyoko mezani.”
Kauli
hiyo imekuja kipindi ambacho baadhi ya viongozi wakiwamo wa vyama vya siasa
nchini, Dk Wilbroad Slaa (Chadema), Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim
Seif Shariff Hamad na pia aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Jaji Joseph Warioba, pia kumkosoa Rais Kikwete.
Kwa
nyakati tofauti, wameeleza kuwa Kikwete ndiye mtu pekee anayeweza kutuliza
mvutano ulioibuka katika mchakato huo unaoendelea kwenye Bunge la Katiba.
Ulikoanzia
mzozo
Machi
21, wakati akifungua Bunge Maalum la Katiba, Rais Kikwete aliipinga
Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba, akigusia
mambo saba ya msingi yaliyomo katika rasimu hiyo na kutaka yatazamwe kwa kina,
kubainisha kuwa mengine hayawezi kutekelezeka.
Miongoni
mwa mambo hayo ni muundo wa Muungano kuwa wa serikali tatu uliopendekezwa
katika rasimu hiyo.
Kikwete,
ambaye alisema anatoa maoni yake binafsi, alipinga waziwazi pendekezo la
serikali tatu na kuegemea katika muundo wa serikali mbili unaoungwa mkono na
CCM, huku akifafanua kuwa idadi ya watu waliopendekeza muundo wa serikali tatu
ilikuwa ndogo.
Walilosema
wengine
Julai
7, wakati akizungumza katika kipindi cha Dakika
45 kinachorushwa na televisheni ya ITV, Maalim Seif alimtupia
lawama Rais Kikwete kuwa amechangia kuukoroga mchakato wa katiba kwa kufuata
msimamo wa chama chake, badala ya maoni ya wananchi yaliyomo katika rasimu ya
pili ya katiba.
Maalim
Seif, ambaye alilenga kauli iliyotolewa na kiongozi huyo wa nchi wakati
akifungua Bunge la Katiba, alisema kauli ya Rais Kikwete imeondoa imani ya
wananchi kuhusu kupatikana kwa katiba inayotokana na maoni yao.
Alisema
mchakato huo hivi sasa unamtegemea Rais pekee, huku akisisitiza kuwa hakuna
binadamu aliyekamilika na kumshauri kutafuta uwezekano wa kuweka mambo sawa,
ili kujenga tena imani kwa wadau wote.
Julai
4, Dk Slaa, wakati akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jijini
Dar es Salaam, alimtaka Rais Kikwete kujitokeza hadharani kutafuta suluhu ya
kupata mwafaka wa mchakato wa Katiba Mpya kwa kuwa hakuna mamlaka nyingine
zaidi inayoweza kuunusuru.
Naye
Jaji Warioba kwa nyakati tofauti amemshauri Rais Kikwete kuchukua hatua
zitakazoondoa matatizo katika Bunge la Katiba ili kuwezesha mchakato huo
kukamilika.
Alisema
ni muhimu kiongozi huyo mkuu wa nchi kuweka kando tofauti za mawazo na mitazamo
ili kupata Katiba Mpya kwa masilahi ya Taifa.
Mwanzoni
mwa wiki, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya na naibu waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Godfrey Zambi alifichua kuwa msimamo wa serikali mbili unaoonyeshwa
na wabunge wa chama hicho ni maagizo ya Kikwete.
Awashauri
Ukawa
Kuhusu
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Tendwa aliwashauri wajumbe wote
wanaounda umoja huo kurejea bungeni ili kujadili vipengele vinavyogusa maslahi
ya wananchi na kuweka kando sura ya kwanza na sita zinazohusu muundo wa
Serikali.
Aliwataka
wajumbe wanaounda Ukawa kuacha kususia vikao na kutoka kwenye Bunge
la Katiba kama walivyofanya tangu Aprili 16 na kusema kuwa busara zaidi ndizo
zinazotakiwa kutumika kupitia majadiliano kwa lengo la kumaliza mgogoro
uliopo na kuwezesha mchakato kuendelea.
Alisema
rasimu siyo katiba bali ni andiko linaloweza kubadilishwa na kuvunjwa vunjwa,
hivyo wajumbe wa Ukawa warudi bungeni na kuandaa rasimu ya katiba itakayokwenda
kupigiwa kura na wananchi.
“Unatoka
nje na unasema hurudi, wewe ni nani? Kunahitajika hapa uvumilifu wa kisiasa.
Watu hawa (Ukawa) na wengine wanatakiwa kuaminiana katika mchakato huu. Warudi
bungeni wajadili vifungu vya katiba vinavyowagusa wananchi.
“Wasijadili
pekee muundo wa Muungano, wajadili vifungu vinavyohusu wananchi, kisha
iandikwe rasimu itolewe kwa wananchi kwa muda mwafaka na wao waende
huko wawaelimishe ili wafanye uamuzi sahihi.
“Hoja
ya msingi iwe upigaji kura uwe wa serikali mbili au tatu kwa kuwa vifungu
vingine vimekwishaafikiwa,” alisema Tendwa.
Aliongeza
kuwa inashangaza kuona tangu wajumbe hao watoke bungeni ofisi ya msajili wa
vyama vya siasa haikutakiwa kuendelea kukaa kimya kuhusu Ukawa wanaojitangaza
kinyume cha kanuni na sheria.
“Ofisi
hiyo (ya msajili) imekuwa kimya, haisemi lolote kuhusu Ukawa. Hawana uhalali wa
kisheria na mamlaka. Kwa hiyo msiwakuze bure bila sababu ya msingi kwani hatujui
wameanzia wapi, mizizi yao ipo wapi,” alisema.
Kuhusu
lugha inayotumiwa na wajumbe kwenye Bunge la Katiba, Tendwa alisema ni ya
mitaaani na wakati mwingine watoto hutumia lugha nzuri kuliko ya wabunge hao.
“Lugha
ya matusi kuingizwa bungeni ni aibu. Hata watoto hawafanyi hivyo, lakini
wabunge tunaowategemea kabisa ndio wamekuwa wakitumia maneno ya kibabe na
kejeli. Wanatakiwa kujifunza kuwa wanapoingia bungeni lazima lugha za mitaani
waziache nje,” alisema.
Bunge
la Katiba linatarajiwa kuendelea tena Agosti 5, huku kukiwa na wasiwasi kama
wajumbe wa Ukawa watarejea au la baada ya kususia vikao hivyo.
Mwenyekiti
wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta tayari ameitisha kikao cha Kamati ya
Mashauriano chenye wajumbe 27 kitakachofanyika jijini Dara es Salaam Julai 24
kwa lengo la kuinusuru katiba hiyo na kuwashawishi Ukawa kurejea bungeni.
Wakati
akistaafu, Tendwa alisema anajivunia kuifanya ofisi ya Msajili iwe ya kisasa,
akisema aliteuliwa bila ya kupewa adidu za rejea na alitegemea kuwa ofisi hiyo
ingekuwa na wanasheria, lakini alijikuta mtu pekee mwenye taaluma hiyo.
No comments:
Post a Comment