To Chat with me click here
Showing posts with label WIZI. Show all posts
Showing posts with label WIZI. Show all posts

Saturday, August 31, 2013

JESHI LA POLISI LAINGIA KATIKA KASHFA NZITO!


IGP Saidi Mwema

Gazeti la Mwananchi limeweka wazi kwamba upanga wa dhahabu aliokabidhiwa Mwema kama ishara ya kuwa mwenyekiti wa jeshi kwa kipindi cha mwaka ameshindwa kuukabidhi kwa mwenyekiti mpya na iligundulika kuwa uliibiwa siku nyingi na ilibidi akabidhi upanga feki na kuahidi kwamba ataurudisha baada ya mwezi mmoja ikishindikana Tanzania itabidi itengeneze upanga mwingine wa dahabu.


Jeshi la Polisi limeingia katika kashfa nzito baada ya mkuu wake, Inspekta Jenerali Said Mwema, kuibiwa upanga wa dhahabu ambao ni mali ya Shirikisho la Wakuu wa Majeshi ya Polisi wa nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO).

Upanga huo wenye uzito wa takriban kilo tatu na wenye thamani ya zaidi ya fedha za Tanzania Sh600 milioni, ni kielelezo kwa nchi inayokabidhiwa uongozi wa SARPCCO.

Mwaka jana Tanzania ilikuwa mwenyekiti wa SARPCCO, ambapo upanga huo ulikabidhiwa kwa IGP Mwema na Jenerali Magwashi Victoria ‘Riah’ Phiyega, ambaye ni Kamishna wa Taifa wa Polisi wa Afrika Kusini aliyekuwa amemaliza muda wake kwa wakati huo.

Hilo ni tukio la pili la wizi la mali zinazohusu ofisi ya IGP, ambapo mwaka jana ndani ya ofisi hiyo kuliibwa kompyuta ndogo (laptop), ikiwa na taarifa muhimu za kipolisi. Hadi sasa hakuna taarifa za kupatikana kwa kompyuta hiyo.

IGP Mwema alikabidhiwa upanga huo Septemba 5, 2012, katika mkutano saba wa SARPCCO uliofanyika Zanzibar na kuhudhuriwa na wakuu wa majeshi ya Polisi kutoka nchi 13, pamoja na mashirika ya kimataifa.

Upanga huo ambao unakwenda sambamba na bendera ya SARPCCO, ni moja ya vielelezo vya nchi iliyochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa shirikisho hilo, ambaye moja kwa moja anakuwa ni Mkuu wa Jeshi la Polisi katika nchi husika.

Kwa mujibu wa taratibu za SARPCCO, vielelezo hivyo hutakiwa kuwekwa ofisini kwa kiongozi husika, ikiwa ni alama ya kila mgeni atakayeingia ofisini hapo kutambua uwepo wa wadhifa huo wa kimataifa.

Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa IGP aligundua kutoweka kwa upanga huo wiki iliyopita, wakati akijiandaa kwenda kuukabidhi kwa mwenyekiti mpya wa SARPCCO, ambaye ni IGP wa Namibia.

Taarifa za ndani ya jeshi hilo zilibaini kuwa, IGP alilazimika kuondoka bila upanga huo alipokwenda Namibia wiki iliyopita kuhudhuria mkutano wa nane wa SARPCCO, uliofanyika Jumapili iliyopita mjini Windhoek.

Kwa mujibu wa uchunguzi, IGP Mwema alikabidhi upanga unaofanana na huo ambao siyo wa dhahabu, alioazimwa kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi la Namibia, Inspekta Jenerali, Luteni Jenerali Sebastian Ndeitunga, na kukabidhiwa kama ishara ya kukabidhiwa uenyekiti wa SARPCCO kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Uchunguzi ulibaini kuwa IGP Mwema alitoa ahadi ya kurejesha upanga halisi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, au Serikali ya Tanzania italazimika kutengeneza mwingine kulipa uliopotea.

Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa kashfa hiyo ametupiwa Mkuu wa Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa pamoja na dereva wake, ikidaiwa kuwa upanga huo baada ya kupokewa na IGP Mwema, Septemba mwaka jana uliwekwa kwenye gari la kamishna huyo.
  

Thursday, March 14, 2013

POLISI WATANO KIZIMBANI WIZI WA SH. MILIONI 150

Baadhi ya askari polisi wanaotuhumiwa kuiba Sh. milioni 150 baada ya kuziokoa katika tukio la ujambazi eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam wakifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Askari watano wa Jeshi la Polisi wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na shtaka la wizi wa Sh. milioni 150.

Washtakiwa hao walikwenda kuzuia tukuo la ujambazi wa kupora katika duka moja eneo la Kariakoo, lakini wakatuhumiwa kuiba fedha zilizoporwa na majambazi hao kisha kuzidondosha.

Washitakiwa hao walisomewa mashtaka yao jana mbele ya Hakimu Mkazi,  Emmilius Mchauru.

Washtakiwa hao ni Stafu sajenti D. 8845 Dancan Mwasabila (43),  Koplo E.9288  Geofrey (39), Koplo E. 5585  Rajabu Nkumkwa (46), Koplo E.29249 Kawanani  Humphrey (34)  na Koplo E. 5548 Kelvin Mohamed(44).

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Bernad Kongola, alidai kuwa Desemba 18, 2012 katika eneo la Kariakoo Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao kwa pamoja waliiba fedha taslimu Sh. milioni 150, mali ya Mire Artan Ismail.

Washtakiwa wote walikana shtaka hilo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na haukuwa na pingamizi ya dhamana dhidi yao.

Hakimu Mchauru alisema washtakiwa wanatakiwa kusaini hati ya dhamana ya  Sh. milioni tano, kuwasilisha fedha taslimu Sh. miloin 15 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo ya fedha.

Mbali na masharti hayo ya dhamana, pia kila mshtakiwa alitakiwa  kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika  ambao kila mmoja wao angesaini bondi ya Sh. milioni tano.

Hata hivyo, mshtakiwa wa kwanza hadi wane walitimiza masharti hayo na mshtakiwa wa tano amekwenda mahabusu hadi Machi 27, mwaka huu itakapotajwa tena.

Monday, February 4, 2013

NAIBU WAZIRI JANUARY MAKAMBA AVAMIWA NA MAJAMBAZI



USIKU wa kuamkia jana majambazi wamevamia nyumbani kwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba. January alisema wakati majambazi hao wanavamia katika nyumba yake iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam, kati ya saa tisa na saa 10 alfajiri ya jana, yeye alikuwa jimboni kwake Bumbuli kuhudhuria msiba.

“Baada ya Bunge kuahirishwa nilienda jimboni kuhudhuria msiba wa mzee mmoja maarufu kule kwetu, kwa hiyo sikuwapo nyumbani wakati tukio hilo linatokea.

“Nyumbani alibaki mke na watoto wangu, majambazi wanne waliingia ndani lakini cha ajabu hawakuiba kitu chochote kwa sababu chini sebuleni kulikuwa na laptop, ipad na samani nyingine.

“Si hivyo tu, bali walifanikiwa kupanda juu na kuingia katika ofisi yangu ya nyumbani, nako pia hawakuchukua chochote.

“Kwa bahati nzuri mke wangu alifanikiwa kubonyeza kitufe na alarm ya kampuni ya ultimate security, ikaanza kulia ndipo majirani nao wakatokea kutoa msaada, lakini majambazi hao wakafanikiwa kukimbia. Baada ya kukimbia waliacha kamba sebuleni na tape ya kuzibia midomo,” alisema January.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema majambazi hao walifanikiwa kuingia katika nyumba hiyo baada ya kumfunga kamba mlinzi.

Alisema baada ya kumdhibiti mlinzi walifanikiwa kuingia ndani ya nyumba hiyo kupitia madirishani.

“Walipomfunga kamba mlinzi, waliingia ndani kupitia katika madirisha yenye vioo vya aluminium na wengine walibaki nje. Kwa bahati nzuri kelele za majirani na zile za waliokuwa ndani ya nyumba hiyo zikawakimbiza.

“Hawakufanikiwa kuiba chochote na wala kumjeruhi mtu yeyote, ilibidi wakimbie tu kuokoa maisha yao maana nyumba ya January waliyoingia ni ghorofa halafu ina uzio, sasa kama wangeendelea kubaki maana yake wangekutwa na siku hizi raia wakiwakamata majambazi kinachofuata ni kuwaua.

“Polisi walifanikiwa kufika eneo la tukio na kwa kuwa majambazi hao waliwahi kukimbia, tumeshindwa kutambua walikuwa na silaha za aina gani,” alisema Kenyela.

Alisema wameshaanza kufanya msako mkali kuhakikisha majambazi hao wanawakamata.

“Tumeshaanza kufanya msako na tutawakamata wote waliovamia nyumba hiyo, siku hizi jeshi letu limeimarika mno na tutawakamata hao na wahalifu wengine wanaofanya vitendo viovu katika maeneo mbalimbali,” alisema Kenyela.