SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, kutangaza kutogombea
urais mwaka 2015 na kwamba badala yake anajielekeza kupanga na kutekeleza
mikakati kuhakikisha chama chake kinaingia Ikulu, Watanzania wamemuunga mkono
wakisema ni mkomavu kisiasa.
Mbowe alihutubia mkutano jimboni Karatu
juzi na kusema kuwa kazi yake itakuwa kusimamia kupata viongozi bora wa
kupeperusha bendera ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Kauli hiyo ya Mbowe ilimaliza uvumi
uliokuwepo kuwa huenda angegombea, ila aliweka bayana kuwa mgombea wao wa mwaka
2010, Dk. Willibrod Slaa, bado anatosha kugombea wadhifa huo kutokana na kazi
nzuri aliyoifanya ya kuwapatia wabunge wengi.
Msimamo huo wa Mbowe, jana ulitawala
katika mijadala ya wananchi kwenye mazungumzo ya kawaida na mitandao ya
kijamii, huku wengi wakimuunga mkono na kudai si king’ang’anizi wa madaraka.
Wananchi hao katika mitandao ya kijamii
walikwenda mbali zaidi wakiwataka hata viongozi wakuu wa vyama vingine vya
upinzani, ambao wamewahi kuwania nafasi hiyo bila mafanikio makubwa,
kutengeneza mkakati wa kuwaandaa wagombea wengine wanaokubalika zaidi yao.
Miongoni mwa viongozi waliotajwa
kupoteza mvuto ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim
Lipumba na Katibu wake Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, ambao wamegombea kiti
hicho bila mafanikio mara nne mfululizo tangu mwaka 1995.
Akizungumza na Tanzania Daima, Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alimpongeza Mbowe
kwa hatua ya hiyo.
Dk. Bana alisema kuwa, Mbowe ameonesha
ukomavu wa kutokuwa king’ang’anizi wa madaraka, jambo alilodai ni jema la
kujipima mwenyewe na akatoa msimamo usiotiliwa shaka.
“Mbowe kwa sasa ni mwanasiasa pekee
aliyeonesha upeo wa hali ya juu, na kweli anafaa kuwa kiongozi wa chama
anachokiongoza, na tumemshuhudia akiongoza kwa ukomavu sio katika chama tu ila
hata kambi rasmi ya upinzani bungeni,” alisema.
Aliongeza kuwa, kama anaweza aangalie
wagombea mbalimbali kuwaandaa mapema na si kuwakurupua kama walivyofanya wakati
wa uchaguzi mkuu wa 2010 kwa kumkurupua Dk. Slaa.
Naye mhadhiri mwingine wa chuo hicho,
Bashiru Ally, alisema kuwa CHADEMA kimeonesha mfano, na hivyo CCM waige kwani
suala la mbio za urais kupitia CCM limekuwa ni vita hadi limetikisa nchi.
“Watu wamechafuliana majina,
wanakamiana kisa urais. CCM wanaumwa ugonjwa wa kutaja majina badala ya sifa za
wagombea, kila siku ukiwauliza kama wanagombea au hawatagombea, watu hujibu
majibu ya mkato, subiri nitaoteshwa au huwezi kuvuka daraja kabla ya
kulifikia,” alisema.
Alisisitiza kuwa, kweli wanampongeza
Mbowe na sasa wanamshauri atengeneze mchakato wa wazi wa kupata mgombea ambaye
ataungwa mkono na Watanzania wengi.
“CHADEMA sasa kinakua kwa kasi,
haijulikani ni kwanini japo watu wengi wanahusisha na uungwaji mkono na vijana
na wasomi mbalimbali, hivyo ni wakati wa kuwafunda vijana wake ili wajue sifa
za uongozi,” alisema.
Bashiru alisisitiza kuwa, vijana
wanapaswa kujulishwa kuwa ujana si sifa ya mtu kuwa rais, kwamba kuna sifa
zaidi ya ujana zinahitajika.
Katika mchango wake kwenye mtandao wa
kijamii, mhadhiri mwandamizi wa UDSM, Dk. Azavery Lwaitama alisema kuwa Mbowe
ametoa kauli ya kumuunga mkono Dk. Slaa ambaye kura zake zilichakachuliwa mwaka
2010.
“Kwa Mbowe kusema kuwa hatakuwemo
katika kinyang’anyiro cha kugombea urais ndani ya CHADEMA, hivi ndani
ya CCM kungekuwa hakuna ukomo wa urais si ningekuwa nasikia maoni
kama haya kuwa mgombea wa 2010 ndiye huyo wa 2015?” alihoji.
Aliongeza kuwa, hivi karibuni wakati
wa uchanguzi wa UVCCM ililazimishwa kuwa mwenyekiti atoke Zanzibar na
kwamba vile vile kwa Spika Anne Makinda ililazimishwa ili kumwengua Samuel
Sitta.
“Tumpongeze Mbowe kwa kuondoa ubinafsi
na kumtangaza mwenzake kuwa anatosha kwani si alishinda 2010 bwana, lakini kura
zikachakachuliwa na wale wale ambao wamekuwa wanapanga na kutekeleza
mipango ya kishetani ya kumuua Dk. Slaa ili kuuzima umaarufu wake na
kuisambaratisha CHADEMA,” alisema.
Dk. Lwaitama aliongeza kuwa, CCM
kwenyewe tayari Januari Makamba ameishatangaza kuwa lazima mgombea awe kijana
na kwamba hata Rais Jakaya Kikwete aliishatangaza kuwa atakapotoka anataka
akabidhi urais kwa mtu mwenye umri mdogo kuliko yeye.
“Nadhani tuwaache CHADEMA wapeane
maelekezo wao kwa wao. Na tumpongeze Mbowe kwa kutanguliza masilahi ya
chama chake na taifa kwa ujumla badala ya masilahi ya kwake binafsi,”
alisema.
Alifafanua kuwa, sasa propaganda za
CCM kwamba Mbowe naye anautaka urais zimetunguliwa hivyo na labda
sasa zitabaki za Zitto Kabwe kuusaka urais.
Kwamba ikitokea Zitto akatamka kama
alivyotamka Mbowe, basi nazo zitapeperushwa na upepo zibaki sasa
propaganda za kumchafua Dk. Slaa.