Profesa J akipokea Kadi ya CHADEMA toka kwa Mhe. Mbilinyi a.k.a SUGU |
MSANII maarufu wa hip hop nchini,
Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay, au Jay wa Mitulinga, pamoja na msanii wa
kundi la Mapacha, Levison Kasulwa wamekabidhiwa rasmi kadi za kujiunga na Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mjini Dodoma jana.
Zoezi hilo lilifanyika katika hoteli ya
Desert Palm, ambako walikabidhiwa kadi hizo na Mbunge wa Mbeya Mjini, ambaye
pia ni Waziri Kivuli, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph
Mbilinyi ‘Sugu’.
Akizungumza baada ya kukabidhi kadi
hizo, Sugu alisema wasanii hao wameamua uamuzi wa busara, kwani CHADEMA ni
chama cha kutetea haki za wanyonge na wasanii kwa ujumla.
Sugu alisema yeye alipofikia uamuzi wa
kujiunga na CHADEMA, alipokelewa na kupewa ushirikiano mkubwa na makamanda wote
ambao sio wasanii, hali inayoonesha kuwa chama hicho hakina ubaguzi kwa mtu
yeyote.
“Naamini kamanda licha ya kujiunga
huku, lakini utaendeleza muziki na utashirikiana kwa hali na mali kupeleka
mbele gurudumu la chama na Watanzania kwa ujumla,” alisema Sugu.
Waziri kivuli huyo aliongeza kuwa kama
angeambiwa amshauri Profesa Jay, angemwambia arudi nyumbani Mikumi akawatumikie
wananchi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Ubungo, John
Mnyika, akizungumza katika hafla hiyo, alisema yeye ni mmoja kati ya watu
waliowashawishi wasanii hao wawili, Profesa Jay na Sugu kujiunga na CHADEMA.
Alisema baada ya kuwashawishi, Mbilinyi
ilimchukua miaka mitano kufikia uamuzi wa kuwa mwanachama, wakati Profesa Jay
imemchukua miaka sita hadi jana alipoamua kufikia uamuzi huo, kitendo ambacho
kinaonesha dhahiri kuwa kuchukua kwao muda mrefu ni kwa dhati na wala
hakutetereki.
“Mtu yeyote anayefanya uamuzi kwa muda
mrefu, anakuwa amefanya uamuzi sahihi na wa uhakika na anakuwa anajiamini
katika uamuzi huo,” alisema Mnyika.
Naye Profesa Jay, alisema atailinda kwa
gharama yoyote CHADEMA na atakuwa tayari kushirikiana na wapiganaji wenzake
ambao ni makamanda ndani ya chama hicho, katika kuhakikisha inasonga mbele na
kuendelea kutetea haki za Watanzania.
“Mimi Profesa Jay ni kama daraja,
nawahamisha watu wa upande huu na kuwapeleka upande mwingine wa sarafu,”
alisema.
Kaselwa wa Mapacha, alisema ameamua kwa
moyo wake mwenyewe na wala hajashinikizwa na yeyote kujiunga na chama hicho.
ILI TUENDELEE TUNAHITAJI VITU VINNE, KWANZA WATU, PILI ARDHI, TATU SIASA SAFI, NNE UONGOZI BORA - PROF J
No comments:
Post a Comment