WAZIRI NCHIMBI AJITOSA
KUMSAFISHA KINANA
Mhe. Mch. Msigwa |
MSEMAJI Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani
wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa, amewalipua vigogo wa
serikali na makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akidai kuwa wana maslahi
yanayotilia shaka katika sekta ya uwindaji wa kitalii na kusababisha kuwapo kwa
ujangili.
Kama alivyofanya mwaka jana na hata
kwenye mikutano yake mingi ya hadhara, Msigwa alimtaja tena Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana, na mkewe, kwamba anamiliki kampuni ya Sharaf Shipping Co,
Ltd ambayo meli yake inadaiwa kunaswa na kontena la shehena ya meno ya tembo.
Hata hivyo, hotuba ya Msigwa ilikatizwa
kwa mwongozo wa mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM), akihoji kitendo
cha mbunge mwenzake kudai ofisi ya Spika ni kaburi la kuzika haki. Hata hivyo
Spika Anna Makinda aliwataka wawe wavumilivu kwani yako maneno mengine mengi
kama hayo.
Hata hivyo Msigwa aliendelea kusoma
maoni ya kambi ya upinzani kuhusu makadirio ya matumizi na mapato ya Wizara ya
Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha wa 2013/14.
Huku wabunge wa CCM wakimwangalia kwa
makini na wengine kutikisa vichwa kumpinga, Msigwa alimtaja mfanyabiashara na
kada wa CCM, Mohsin Abdallah.
Msigwa ambaye alikuwa akikariri taarifa
ya kamati ya waziri wa zamani wa wizara hiyo, Antony Diallo, aliwataja
makada waandamizi wengine wa CCM wenye maslahi ya aina hii kuwa ni kampuni ya
Coastal Wilderness (Tz) Ltd., ambayo wakurugenzi wake wanatajwa kuwa ni Napono
Edward Moringe Sokoine na Namelok Edward Moringe Sokoine; Enzagi Safaris (Tz)
Ltd., yenye wakurugenzi Makongoro Nyerere, Muhamed Seif Khatib na Saidi Kawawa;
na Hunting Safaris yenye wakurugenzi, Chande Kawawa na Hassan Kawawa.
Kampuni zingine ni M.S.K. Tours &
Hunting Safari Co. ya Muhamed Seif Khatib.
Msigwa alisema mengi ya makampuni haya
yalipewa vitalu vya uwindaji wakati hayana uzoefu wala mtaji wa kuendesha
biashara ya uwindaji wa kitalii katika vitalu hivyo.
Alisema matokeo yake ni kwamba
makampuni hayo yalishindwa kusimamia uhifadhi wa wanyamapori katika vitalu vyao
na kusababisha tatizo la ujangili kushamiri katika vitalu hivyo.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka serikali kutoa kauli mbele ya Bunge lako tukufu ni kwa nini serikali
hii ya CCM imekuwa ikitoa vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa makada waandamizi
wa CCM ambao wanajulikana kuwa hawana weledi wala uwezo wa kibiashara wa
kuendesha biashara ya uwindaji wa kitalii na hivyo kusababisha tatizo la
ujangili kuwa kubwa zaidi na kuleta hasara kwa taifa letu!” alisema.
Akiwa amerejea bungeni baada ya adhabu
ya siku tano, Msingwa alisema serikali imeanza kufedheheshwa katika mikutano ya
kimataifa ya uhifadhi kwa sababu CCM imeamua kukumbatia makada wake waandamizi
aliodai wanajihusisha na ujangili.
Alitolea mfano Mkutano wa 16 wa Nchi
wanachama wa Mkataba wa Biashara ya Kimataifa ya Wanyama Walio Hatarini
Kutoweka (CITES) uliofanyika Bangkok, nchini Thailand mwezi uliopita.
Bonyeza "Read More"
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inataka kujua ni fedheha ya aina gani kimataifa itakayoiamsha serikali hii ya
CCM katika usingizi wake wa pono ili iweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya
makada wa CCM wa aina hii?”alihoji Msigwa.
Kuhusu Kinana, Msigwa alisema kampuni
yake ya wakala wa meli ya Sharaf Shipping Co. Ltd, si tu kwamba imehusishwa na
usafirishaji haramu wa pembe za ndovu kutoka Tanzania bali pia inadaiwa kutoa
ajira haramu kwa wageni.
Alisema wakati shehena ya meno hayo ya
tembo inakamatwa nchini Vietnam, nyaraka zilizoambatana na shehena hiyo
zilionyesha kwamba kibali cha kusafirisha shehena hiyo kilisainiwa na raia wa
India anayeitwa Samir Hemani mnamo Novemba 13, 2008.
Alisema wakati raia huyo wa kigeni
anasaini kibali cha kusafirisha shehena ya meno ya tembo kwa niaba ya wateja wa
Kinana na mkewe, kibali chake cha kuishi Tanzania kilikuwa kimeisha tangu Mei
7, 2008.
Msigwa alimshambulia Waziri wa
Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, na kumtaka ajiuzulu kwa madai
kuwa ameshindwa kulinda rasilimali za nchi na kusababisha wanyamapori kutoweka
kwa kuuawa na majangili.
Alimshambulia pia Spika Anna Makinda
kuwa Bunge lake limekuwa kaburi la kuzikia utekelezaji wa maazimio mengi
kuhusu kashfa mbalimbali zilizogubika utendaji wa Ofisi ya Waziri wa Maliasili
na Utalii na utekelezaji wa majukumu yake kisheria.
NCHIMBI AJIBU MAPIGO
Hoja za Msigwa zilimlazimu Waziri wa
Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuomba nafasi ya kwanza kuchangia hotuba
ya Waziri Kagaeshiki na hivyo kutumia muda huo kurusha makombora mazito kwa
CHADEMA kwa kuwaita kuwa ni genge la uongo ndani ya Bunge.
“Kabla sijaendelea, nitumie nafasi hii
kuipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri na katika hotuba hii ya
Waziri Kagasheki imejidhihirisha wazi kwa kipindi hiki kifupi kuwa wamekamata
watuhumiwa wa ujangili 354 na zipo mahakamani kesi 283, bunduki 435
zimekamatwa.
“Ukiona mtu anasimama na kusema
serikali haijafanya kazi, basi upeo wake wa kufikiri ni mdogo,” alisema
Nchimbi.
Waziri huyo alijielekeza kwenye baadhi
ya hoja zilizolengwa dhidi ya Kinana ambapo alisema Msigwa ameamua kusema uongo
ili kulipotosha Bunge na Watanzania kwa ujumla kwamba katibu huyo alikamatwa na
meno ya tembo nje.
“Nimejaribu kufuatilia kwa umakini
kujua kwamba kifungu hicho alikimaanisha, alikielewa, alikitafakari au
aliandikiwa tu kisha akaenda kukisoma. “Baada ya kutafakari kwa kina nimegundua
kwamba hakuwa na nia mbaya bali alikuwa ameandikiwa tu na kuisoma,” alisema.
Nchimbi alitumia muda huo kufafanua
majumu ya kati ya Shipping Agency na Clearing and Fowarding.
“Kampuni ya shipping agency duniani
kote ni kumwakilisha mwenye meli, agenti hawezi kuwa mwenye meli ila
anamwakilisha mwenye meli, kuna shughuli mbalimbali zinazofanyika kwenye meli. “Kuna
mambo ya kuhudumia watumishi kwenye meli, kuwapelekea chakula watumishi, kufanya
usafi, kupelekea mahitaji muhimu lakini wapo watu wanaofanya ‘clearing and
fowarding’ na Kiswahili chake ni kupeleka na kutoa.
“Hawa ndio wanaopeleka mizigo bandarini
na kule ndiko kuna utaratibu wa upekuzi kwa hiyo huko hahusiki mtu wa shipping
agency, sina mashaka hata kidogo kuwa Mchungaji Msigwa analijua hili ila
amelifumbia macho kwa makusudi na kwa maslahi yasiyokubalika kwa taifa,”
alisema.
Wakati akiendelea kuchangia, Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), aliomba mwongozo wa Spika kutaka
kutoa ufafanuzi, lakini Spika alikataa. “Mliposema ninyi, wenzenu walinyamaza,
mtulie hivyo hivyo, naomba uendelee hakuna cha taarifa, endelea Mheshimiwa
Nchimbi na nyie mnanyamaza kama walivyonyamaza wenzenu,” alisema Makinda.
Nchimbi aliendelea kusema kumekuwepo
uvumi ambao unafanywa kwa Kinana kwamba anamiliki meli
iliyotumika kusafirisha pembe za ndovu.
Alisema baada ya uchunguzi wa
kutosha kuhusu kesi hii, ikabainika na watuhumiwa wakashtakiwa kwa uhujumu
uchumi kwa kufunguliwa kesi namba 3 na 4 ya mwaka 2006.
Nchimbi aliwataja watuhumiwa hao
kuwa ni Eradius Tesha, Shaban Abura, Eric, Issa Abubakar na Omar Hussein. “Mh
Spika, hawa ndiyo waliopelekwa mahakamani na uchunguzi ulijidhihirisha kuwa
hawa ndiyo watuhumiwa wa kesi hiyo na kambi ya upinzani inalijua hili,”
alisema.
Alisema wakati kesi iko Kisutu,
ulihitajika ushahidi kutoka nchi ya Vietnam na nchi hiyo imesema haina
ushirikiano na Tanzania katika mambo ya jinai.
“Hivi sasa tunazungumza na ubalozi wa
China watupe kibali cha kufanya upelelezi ili kesi hiyo iweze kuendelea na kwa
msingi huo Mahakama ya Kisutu inataka ushahidi huo ili kesi iendelee na hili
wapinzani wanalijua,” alisema.
No comments:
Post a Comment