Mhe. Zitto Kabwe |
WABUNGE wa CHADEMA; Zitto Kabwe (Kigoma
Kaskazini) na John Mnyika (Ubungo), wamewachochea wabunge wenzao wasihudhurie
semina iliyoandaliwa leo na Wizara ya Nishati na Madini. Sababu waliyoitoa
wabunge hao juu ya ushawishi huo ni kuwa serikali imeanza ugawaji wa vitalu
vipya vya mafuta na gesi kwenye bahari kuu na Ziwa Tanganyika Kaskazini.
Hata hivyo, hatua hiyo imeonekana
kuwagawa wabunge, ambapo baadhi wamepinga na wengine kuunga mkono. Kupitia
taarifa zao kwa vyombo vya habari walizozituma kwa nyakati tofauti, Zitto na
Mnyika wamepinga uamuzi wa serikali wa kuanza mzunguko wa nne wa ugawaji wa
leseni za utafutaji na ugunduzi wa gesi nchini.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari, Zitto ameonesha kushangazwa na uamuzi huo wa serikali, kwani Tanzania
bado haijawa na sera ya gesi asilia na kwamba ndiyo kwanza wabunge wamepewa
rasimu ya sera hiyo kwa ajili ya kutoa maoni yao.
“Kesho Jumamosi wabunge tumealikwa
kwenye semina kuhusu sera ya gesi asilia. Tumegawiwa tayari nakala zetu, tena
zipo kwenye lugha ya kimombo,” alisema Zitto na kuongeza; “Jambo la kushangaza
ni kwamba wakati sera ya gesi asilia ipo kwenye rasimu na ndiyo kwanza wabunge
tumeletewa kutoa maoni, serikali tayari imetangaza tena kugawa vitalu vya
mafuta na gesi kwenye bahari kuu na Ziwa Tanganyika Kaskazini.”
Mhe. John Mnyika |
Pia katika taarifa hiyo Zitto ameelezea
kushangazwa na hatua hiyo ya serikali ambayo alisema inakwenda kinyume cha
maamuzi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayozuia ugawaji mpya wa
vitalu hadi sera ya gesi asilia na sheria ya gesi vikamilike.
“Haraka hii ya serikali kugawa vitalu
bila sera wala sheria inatoka wapi? Nitashangaa sana wabunge kukimbilia posho
za semina hii na kuhalalisha maamuzi yasiyozingatia maslahi ya taifa kwa vizazi
vya sasa na vijavyo,” alisisitiza Zitto.
Zitto amewataka wabunge na wananchi
kuupinga uamuzi huo wa serikali.
“Uamuzi wa kugawa vitalu vipya bila
kwanza kuwepo kwa sera na sheria mpya unapaswa kupingwa kwa nguvu zote. Tafuta
mbunge wako, mwambie asikubali maamuzi haya ya serikali. Tumalize kwanza sera
na sheria ndiyo tugawe vitalu vipya. Gesi sio viazi, haiozi,” imesisitiza
taarifa hiyo.
“Taifa letu lipo kwenye mchakato wa
kuandika katiba mpya huku kukiwa na kumbukumbu chungu za miaka zaidi ya 20 ya
kupata hasara kubwa baada ya kufungua mianya ya ufisadi na unyonywaji katika
sekta ya uchimbaji madini na rasilimali zingine muhimu,” ilisema taarifa yake
kwa vyombo vya habari.
Taarifa hiyo inapendekeza kuwa ingekuwa
vema kwa serikali kusubiri kwanza kukamilika kwa mchakato wa kupata katiba mpya
ili kuhakikisha kuwa udhaifu wa kikatiba, kisera, kisheria, kiuongozi na
kitaasisi umerekebishwa.
“Hivyo, badala ya kukimbilia kutangaza
mzunguko mwingine huku tayari taifa likiwa kwenye lindi la ufisadi na unyonyaji
kupitia mikataba iliyotangulia ya gesi asili; nguvu za wananchi zielekezwe
katika kutaka katiba mpya kuwa na vifungu vitakavyolinda rasilimali muhimu kama
mafuta, gesi madini na mali asili nyingine,” imesisitiza taarifa hiyo.
Hivi karibuni Wizara ya Nishati na
Madini kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imetoa taarifa
ya kuzinduliwa kwa mzunguko wa nne wa utoaji leseni za utafiti na ugunduzi wa
gesi asilia nchini. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na baadhi ya vyombo vya
habari, na tovuti ya TPDC ni kwamba utoaji leseni za utafiti na uzinduzi huo
utaanza mwezi Oktoba, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, leseni
zitakazotolewa zitahusisha utafiti katika Ziwa Tanganyika lililopo magharibi
mwa Tanzania, na ndani ya kina kirefu cha maji ya Bahari ya Hindi kwa upande wa
mashariki na kusini mwa bahari hiyo. Itakumbukwa kwamba hapo awali wizara
ilitangaza kutokuingia mikataba yoyote ya utafiti na uvumbuzi wa gesi asilia
hadi pale sera ya mafuta na gesi itakapokuwa tayari.
Msimamo wa CHADEMA kuhusu sekta ya
mafuta na gesi uko wazi ambapo inataka kwanza kuandaliwa kwa sera na sheria ya
mafuta na gesi kabla ya kuingia mikataba mipya ya utafutaji na ugunduzi wa
nishati hizo.
Baadhi ya wabunge wamelidokeza Tanzania
Daima kuwa kutohudhuria semina hiyo ni kujikosesha fursa ya kujua
kitakachowasilishwa na serikali.
Walibainisha kuwa wasipohudhuria semina
hiyo hawatakuwa na uwanja mpana wa kupinga kile wanachokiona si sawa.
Waziri Muhongo anena
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo alisema Tanzania inatumia sheria ya gesi asilia na mafuta ya
mwaka 1980.
“Watu waache kupotosha..., si kweli
kuwapo maamuzi ya Bunge ya kutogawa vitalu vipya vya utafutaji wa gesi asilia
na mafuta bali kinachofanyika ni kuiboresha sera na sheria ya gesi asilia ili
kuitengenisha na mafuta,” alisema.
Alisema kuwa utafutaji huo haukuanza
leo na kwamba anayegundua ndiye anatafuta sana.
Profesa alifafanua kuwa kwa sasa
wanafanya maboresho ya kulijenga upya Shirika la Mafuta (TPDC) lililoanzishwa
mwaka 1969. “Hawa Watanzania wanaotoa taarifa za uongo kwenye mitandano na
kutaka kupotosha watu, wanaikosesha nchi maendeleo. Maana hayo makampuni ya
mafuta wanayoyapiga vita ndiyo hayo yanatafuta mafuta Msumbiji na Kenya,
kwanini sisi tukatae?” alihoji.
Alisema kuwa kama nchi isingekuwa na
sera ya gesi na mafuta hata hao wawekezaji wasingekubali kuwekeza kwenye nchi
ambayo haina sheria. Waziri Muhongo alisema kuwa leo watafanya semina kwa
wabunge wote mjini hapa kuhusu sera hiyo ya gesi, na hivyo kuwataka wote wenye
dukuduku walete hoja zao wapate ufafanuzi.
No comments:
Post a Comment