WADAI AMEMWONGEZEA
UMAARUFU LEMA, CHADEMA
VIGOGO wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wakiwemo wabunge, wamemjia juu Mkuu wa Mkoa (RC) wa Arusha, Magessa Mulongo kwa
jinsi alivyoshughulikia kesi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
(CHADEMA).
Wabunge hao waliliambia gazeti hili
mjini Dodoma kuwa kesi ya uchochezi iliyofunguliwa na serikali dhidi ya Lema
kwa shinikizo la mkuu huyo, itaiathiri kwa kiasi kikubwa CCM.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alisema
kuwa amefuatilia kwa makini chanzo cha kesi ya Lema na hatimaye kukamatwa na
polisi mithili ya gaidi, na kubaini kuwa hulka za utendaji kazi wa baadhi ya
viongozi wa serikali zinawapa sifa na umaarufu zaidi CHADEMA.
“Mimi sitaki kuingilia kesi, lakini
ukiangalia kuanzia ile inayoitwa video ya vurugu za Chuo cha Uhasibu Arusha na
jinsi Mkuu wa Mkoa alivyofika eneo la tukio na kuondoka, utabaini udhaifu
mkubwa wa kiongozi huyo ambao leo unamfanya Lema aonekane shujaa.
“Leo tunaingia kwenye uchaguzi mdogo wa
madiwani pale Arusha, tunaweza tukashinda, lakini tutafanya kazi ya ziada kwa
sababu tu ya udhaifu wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha,” alisema Lugola.
Mbunge mwingine ambaye aliomba jina
lake lihifadhiwe, alisema alichokifanya Mulongo ni sehemu ya tatizo kubwa la
viongozi wa serikali kujihusisha na ukereketwa wa kisiasa.
“Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi
kusema kuwa kuna kiongozi, tena hakumtaja jina, kwamba anapendwa kubebwa,
alisema mwacheni abebwe. Alisema vile kuwazuia polisi kukabiliana na watu wanaopenda
kumbeba kiongozi huyo.
“Mkuu wa Mkoa Arusha na wengine
wanaokabiliana na wapinzani kwa nguvu kubwa bila sababu, hii inawaongezea
umaarufu,” alisema mbunge huyo kutoka moja ya majimbo ya kanda ya kati.
“Niliposoma ujumbe wa simu ya mkononi
wa Lema ambao alidai umetoka kwa Mkuu wa Mkoa, nilishangaa sana. Sijui kwanini
amefanya vile,” alisema kigogo huyo.
Aprili 24 mwaka huu, Mulongo aliliamuru
Jeshi la Polisi mkoani Arusha kumkamata Lema kwa madai kuwa aliwachochea
wanafunzi wa chuo hicho cha IAA kumzomea na kumrushia mawe. Lema alizingirwa
nyumbani kwake na maofisa wa polisi kitengo cha upelelezi na wale wa doria
Ijumaa saa 5.30 usiku kisha kuchukuliwa hadi Kituo Kikuu cha Polisi kuhojiwa na
kuwekwa rumande siku tatu hadi Jumatatu wiki hii alipofikishwa mahakamani.
Hata hivyo, madai ya Mulongo kuwa Lema
alichochea wanafuzni hao yanakinzana na ushahidi wa video unaoonesha kuwa
mbunge huyo alitumia kila aina ya ushawishi kuwasihi wasiandamane kufuatia
mwenzao Elly Kago (22) kuuawa na watu wasiojulikana jirani na chuo.
Mapema kabla ya kukamatwa, Lema
aliitisha mkutano na waandishi wa habari akidai kutishiwa na Mulongo kupitia
ujumbe wa maandishi wa simu.
“Umeruka kihunzi cha kwanza,
nitakuonyesha kuwa mimi ni serikali, ulikojificha nitakupata na nitakupa
kesi ninayotaka mimi,’’ ulisomeka ujumbe huo uliotumwa kupitia simu namba 0752
960276 ambayo Lema alidai ni ya Mulungo.
ATISHA WAANDISHI
Wakati CCM wakiendelea kumlalamikia
Mulongo kwa hatua zake dhidi ya Lema, kiongozi huyo jana aliwageukia waandishi
wa habari wa Arusha akiwataka wawe makini kipindi hiki, akidai kuwa nao
wanatumika na wanasiasa. Akihutubia katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi,
alisema kuwa ikibainika wanatumika nao watafikishwa katika vyombo vya sheria.
“Mimi nilikuwa Mkuu wa Wilaya Bagamoyo,
hivi hivi wakawa hawanielewi na ikafika wakati wakanielewa kwani kuna miongoni
mwao tulitaka kuwafikisha katika sheria, lakini tukayaacha kwa kuwa sisi ndio
walezi,” alisema.
Mulongo aliongeza kuwa vitu ambavyo
vinaandikwa si kweli kabisa, na kwamba wataendelea kufuatilia kwani baadhi ya
waandishi wanashirikiana na wanasiasa kuwachafua viongozi wa serikali. Alisema
baadhi ya waandishi mkoani Arusha wamekuwa wakifanya kazi zao kwa ushabiki wa
kisiasa na kuandika mambo ambayo hawana uhakika nayo.
“Unapoingia katika mkakati wa
kudhalilisha kiongozi wa serikali unakuwa umeiweka roho yako rehani, kuweni
makini,” alisema.
Aidha alivionya vyama vya wafanyakazi
mkoani Arusha kutoruhusu kutumiwa na watu kwa malengo ya kisiasa na pia waajiri
waache kufanya kazi bila kufuata taratibu na sheria.
No comments:
Post a Comment