Dr. Slaa |
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema Rais Jakaya Kikwete anapaswa kuomba
hekima kwa Mwenyezi Mungu kutokana na matukio yanayotokea sasa nchini.
Alisema hali inayotokea sasa ni matokeo ya wananchi
kupuuzwa na kutokusikilizwa katika suala zima la uwekezaji unaofanyika sehemu
mbalimbali za nchi.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana katika kijiji cha
Giroda Babati vijijini, wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika ziara yake
ya siku tisa ya ujenzi wa Chama mkoani Manyara.
Kabla ya kutoa kauli hiyo Dk. Slaa aliwaomba
wananchi wasimame kwa muda wa dakika moja, kuomboleza vifo vilivyotokea mkoani
Mtwara. Aliongeza kuwa kuendelea kuwapuuza wananchi wa Mtwara ni kuendelea
kucheza na jipu linalopaswa kutumbuliwa na kwamba njia sahihi ni kukaa na
kuwasililiza wananchi katika uwekezaji na kufikia muafaka pasipo kutumia nguvu.
Alisema wanachotaka wananchi wa Mtwara ni kujua
namna watakavyonufaika kwa kile alichoeleza kuwa katika uwekezaji wowote
wanufaikaji wa kwanza wanapaswa kuwa wananchi. Alisisitiza kuwa katika hali ya
Mtwara kulihitajika busara za kawaida za kutatua msingi wa tatizo badala ya
wananchi kupigwa mabomu, risasi na kisha kukamatwa.
“Ni jambo la aibu kuwapiga mabomu wananchi wanaodai
kunufaika na rasilimali za nchi yao hapa kunahitajika elimu ya kuwafahamisha
haki zao ni zipi na siyo mabomu,” alisema Slaa.
No comments:
Post a Comment