MAJONZI na huzuni kubwa imetawala
kwa wakazi wa Kijiji cha Nyangahe, Wilaya ya Uyui, mkoani Tabora, kutokana na
tukio la kuuawa kinyama kwa Mwenyekiti wao wa Serikali ya kijiji, Mussa Chotta
na mkewe Mariam Mhoja ambao walikatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili na
watu wasiofahamika.
Mwenyekiti huyo alichaguliwa
katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 mwaka huu kwa
tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na waliuawa usiku wa kuamkia jana wakiwa
nyumbani kwao katika Kitongoji cha Bukili.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu
Katibu wa CCM wilayani humo, Bagaile Lumolla, alisema tukio hilo limetokea
katika Kijiji Cha Nyangahe, Kata ya Bukumbi.
Alisema chanzo cha tukio hilo
bado hakijajulikana ambapo baadhi ya wananchi waliohojiwa, walilihusisha tukio
hilo na itikadi za kisiasa.
Mtoto wa marehemu, Masumbuko
Chotta, alisema watu waliofanya unyama huo walikuwa watatu na baada ya kufanya
mauaji hayo walitokomea porini.
Alisema siku ya tukio, yeye na
wadogo zake walikuwa wamelala ambapo ghafla wakasikia kishindo kikipigwa
mlangoni na baada ya kuingia ndani walifanya mauaji ya wazazi wao wakiwa
wamefunika nyuso zao.
"Baada ya kuingia ndani
walikwenda moja kwa moja chumbani kwa baba na mama wakaanza kuwashambulia kwa
kuwakata na mapanga na kusababisha vifo vyao.
"Wakati wakiendelea kufanya
unyama huo, nilijaribu kupiga kelele kuomba msaada kwa majirani lakini mmoja wa
watu hao alinitandika kofi na kuanguka chini na kapoteza fahamu," alisema
Chotta.
Jeshi la Polisi wilayani humo
lilithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini alipotafutwa Kaimu Kamanda wa
Polisi mkoani humo, Juma Bwire ili aweze kulitolea maelezo hakupatikana baada ya
msaidizi wake kusema alikuwa kwenye kikao.
No comments:
Post a Comment