Idadi
ya Watanzania imechupa kutoka milioni 34.4 mwaka 2002 hadi takriban milioni 45
mwaka 2012, alitangaza Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete hapo Jumatatu (tarehe 31
Disemba).
Matokeo
ya sensa ya watu na makaazi ya mwaka 2012, iliyoanza mwezi Agosti, yalionesha
kwamba kuna watu 44,929,002 nchini Tanzania, alisema Kikwete kwenye viwanja vya
Mnazi Mmoja mjini Dar es Salaam.
Baada
ya kutangaza matokeo hayo, Rais Kikwete aliwatolea wito Watanzania kuzingatia
uzazi wa mpango kwani kasi ya ukuwaji wa idadi ya watu ni kubwa mno kwa uchumi
wa nchi kuweza kuikimu.
“Kiwango
cha uzazi ni 2.6, lakini ndani ya miaka kumi tu idadi ya watu imeongezeka kwa
milioni 10.5,” alisema Kikwete. “Tunapaswa kuzingatia uzazi wa mpango,
vyenginevyo naweza kuona hatari inayolinyemelea taifa letu.”
Alisema
utabiri unaonesha kwamba mwaka 2016 Tanzania itakuwa na watu milioni 51. Serikali
inapaswa kuirekebisha mipango yake na kutenga fedha, alisema, kwa sababu
asilimia 63 ya watu wako chini ya miaka 30, jambo linalomaanisha kwamba
kutahitajika shule zaidi, hospitali zaidi na huduma ziada nyengine kwa kizazi
kijaacho.
Waziri
wa Fedha William Mgimwa alisema kwamba matokeo hayo ya sensa yatachapishwa
kitaifa na kutumwa kwenye mitandao ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya
Kiuchumi ya Kusini mwa Afrika na Kitengo cha Takwimu cha Umoja wa Mataifa.
Serikali ilitumia jumla ya
shilingi bilioni 140 (dola milioni 88.5) kufanya sensa hiyo, ambayo ni ya tano
tangu uhuru mwaka 1961. Sensa nyengine itafanyika mwaka 2022.
No comments:
Post a Comment