SIKU
moja baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kumtangaza Dk Willibrod Slaa
kuwa ndiye mgombea wa urais mwaka 2015 kwa tiketi ya chama hicho, makada wa
chama hicho wamegawanyika baadhi wakimponda na wengine kumuunga mkono.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya makada wa chama hicho walisema mwenyekiti
wao amekosea kumtangaza mgombea kabla ya wakati, huku wanaomuunga mkono
wakisema hajakosea kwa sababu hatua hiyo itasaidia kuondoa makundi ndani ya
chama hicho.
Juzi,
Mbowe akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Karatu mkoani Arusha,
alisema Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa atapewa fursa ya kuwania tena
urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, huku mwenyewe akijiweka kando kuwania
nafasi hiyo
Hata
hivyo, Dk Slaa alipoulizwa iwapo ana nia ya kuwania nafasi hiyo alihoji: “Kwani
mwaka 2010 nilijitangaza mwenyewe,? Iwapo wanachama wa Chadema watanipendekeza
nitafikiria kufanya hivyo.” Mwasisi wa chama hicho Edwin Mtei, Wajumbe wa
Kamati Kuu; Profesa Mwesiga Baregu na Dk Kitila Mkumbo, Naibu Katibu Mkuu Zitto
Kabwe, Mwenyekiti wa Bavicha John Heche na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
walitoa maoni yanayopingana kuhusu kauli hiyo ya Mbowe.
Wanaounga mkono
Mtei alisema anaunga mkono kauli ya Mbowe akisema kiongozi huyo hajakosea kumtangaza Dk Slaa kuwania urais mwaka 2015.
Mtei alisema anaunga mkono kauli ya Mbowe akisema kiongozi huyo hajakosea kumtangaza Dk Slaa kuwania urais mwaka 2015.
“Ninaunga
mkono Dk Slaa kuwania tena nafasi ya urais mwaka 2015. Mwenyekiti amemtangaza
baada ya kupata baraka ya vikao vya chama,” alisema Mtei.
Ingawa Mtei hakuwa tayari kusema ni kikao gani kilichopitisha jina la Dk Slaa kuwania nafasi hiyo, alisisitiza: “Kuna vikao vya Kamati Kuu vimefanyika hivi karibuni, vinaweza kuwa vimefanya uamuzi huo. Mwenyekiti hawezi kuzungumza jambo bila baraka za vikao vya chama.”
Hata
hivyo, kauli hiyo ya Mtei inapingana na ile aliyoitoa Oktoba 6, mwaka huu baada
ya Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kutangaza kutogombea tena
ubunge badala yake kusema anataka kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Mtei
alisema hatua ya Zitto kutangaza kuwania urais mapema kungesababisha
mzozo na mpasuko ndani ya chama hicho.
Mtei alisema amekuwa akimshauri Zitto mara kwa mara kuhusu hatua yake hiyo akimtaka kuwaunganisha wana Chadema na siyo kuwagawa au kuwavuruga.
“Hakuna
shida kuonyesha hisia, lakini unatengeneza mzozo mkubwa sana ukitangaza sasa.
Mimi nimeshamshauri sana Zitto, ahakikishe anakiunganisha chama na siyo
kukigawa wala kukivuruga.”
Alisema
mbunge huyo kutangaza kutogombea tena ubunge na badala yake kujipanga kuwania
urais mwaka 2015 kumekuja mapema mno na kuonya kuwa itaibua mzozo ndani ya
Chadema.
Mtei
ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu enzi za utawala wa
Mwalimu Julius Nyerere, alisema kwamba wakati mwafaka ukiwadia, Chadema
kitaamua ni nani mwenye sifa za kugombea urais huku akisema kina
utaratibu wake wa kuwapata wagombea mbalimbali wa uongozi.
Hata
hivyo, Zitto jana alikataa kuzungumzia suala hilo akisema: “Nimesikia hata mimi
kwenye vyombo vya habari ila sina cha kuzungumza kuhusu hilo.”
Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche alisema kauli hiyo Mbowe siyo yake binafsi, bali ni ya wananchi.
Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche alisema kauli hiyo Mbowe siyo yake binafsi, bali ni ya wananchi.
“Ni
kauli na maoni ya Watanzania wanaomwamini Dk Slaa kuwa anaweza kumudu
kuliongoza taifa hili kama walivyoonyesha kwa kumpigia kura nyingi kuliko
mgombea yeyote wa upinzani katika nafasi ya urais (mwaka 2010),” alisema Heche.
Heche
alisema ingawa ndani ya Chadema kuna viongozi wengi wenye uwezo wa kuliongoza
taifa, nyota ya Dk Slaa bado inang’ara.
Msimamo
wa Heche uliungwa mkono na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye alisema
ni sahihi Dk Slaa kugombea urais mwaka 2015.
Lema
alisema katika historia ya chaguzi za vyama vingi nchini, hakuna mgombea wa
upinzani aliyewahi kupata kura nyingi kama Dk Slaa mwaka 2010 akadai kwamba
ndiyo maana hivi sasa CCM kinafanya kila njama kumdhoofisha.
Lema
alisema hatua ya kumtangaza Dk Slaa kuwa mgombea wa urais mwaka 2015, itaondoa
harakati za chinichini zilizokuwa zikifanywa na watu ndani na nje ya Chadema
kuwagombanisha viongozi wakuu wa chama hicho, hasa Mbowe na Dk Slaa.
Wanaopinga
Wakati Mtei akieleza kuwa Mbowe amepata Baraka za chama, Profesa Baregu alisema kutangazwa kwa jina la Dk Slaa kuwania urais ni maoni binafsi ya mwenyekiti huyo.
Wakati Mtei akieleza kuwa Mbowe amepata Baraka za chama, Profesa Baregu alisema kutangazwa kwa jina la Dk Slaa kuwania urais ni maoni binafsi ya mwenyekiti huyo.
“Hayo ni maoni yake, lakini vikao vya chama ndivyo vyenye uamuzi wa mwisho kuteua jina la mgombea urais na havijakaa,” alisema Profesa Baregu.
Alipoulizwa
maoni yake kuhusu sababu za Mbowe kumtangaza mgombea urais sasa kabla ya
wakati, Profesa Baregu alisema: “Mbowe atakuwa amefanya hivyo kwa sababu watu
wengi walikuwa wanadhani kwamba yeye pia anawania nafasi hiyo ya urais.”
“Hivyo ili kuweka mambo sawa ameamua kutangaza mapema kuwa hatawania urais na kwamba Dk Slaa ndiye anayefaa kuwania nafasi hiyo,” alisema.
Profesa
Baregu alisema haoni tatizo kwa wanachama wa Chadema kutangaza nia mapema kwa
sababu hiyo ni haki yao kwa mujibu wa katiba… “Hata kama watu wengi watatangaza
nia ya kuwania urais, siyo jambo baya katika ujenzi wa demokrasia, lakini
uamuzi wa mwisho ni wa vikao vya chama.”
Kauli
ya Profesa Baregu kuhusu vikao iliungwa mkono na Dk Mkumbo ambaye alisema
kwamba anachojua vikao vya chama ndivyo vyenye uamuzi wa mwisho kuhusu uteuzi
wa wagombea wa ngazi ya urais.
Dk
Mkumbo alionyesha shaka kama kweli Mbowe alimtaja Dk Slaa kuwa ndiye
atakayewania nafasi hiyo akisisitiza: “Ninachofahamu ni kwamba yeye ametangaza
kuwa hatagombea nafasi hiyo.”
No comments:
Post a Comment