KAMANDA
mpambanaji wa Chadema kutokea Babati Jackson Wilson Makala (pichani juu),
amekanusha vikali habari zilizosambaa kwa watu tofauti waliokaribu nae
zikimhusisha na sekeseke la kuwavua uanachama wa Baraza la Vijana Chadema
ambalo limeleta sintofahamu dhidi yake baada ya gazeti moja la kila siku
kumuandika jana kuwa nae ni miongoni mwa vijana waliosimamishwa kwa muda katika
baraza hilo (BAVICHA kwa makosa tofauti ya utovu wa nidhamu.
Katika
mawasiliano yake na Blog hii, jioni ya leo Makala ameeleza kusikitishwa na
upotoshwaji huo ambao anadai kwa kiasi fulani umemuathiri kwa kuzingatia
uaminifu ambao amejijengea miongoni mwa viongozi na wanachama wengine wa chama
chake, na watanzania kwa ujumla.
“Napenda
kutoa maelezo mafupi kuhusu habari iliyoandikwa na gazeti la jana (jina
linahifadhiwa). Mimi Jackson Wilson Makala sijasimamishwa uanachama na Baraza
la Vijana Chadema (BAVICHA) kama ilivyotaarifiwa na gazeti hilo. Nimewasiliana
na Mhariri wa habari wa gazeti… na amekiri kuwa walifanya makosa makubwa katika
habari ile.
Ukweli
ni kwamba Baraza la vijana CHADEMA taifa jana mchana limetoa tamko la ufafanuzi
kuhusu maamuzi ya Kamati Tendaji ya BAVICHA na hakuna popote lilipotaja jina la
Jackson Wilson Makala kuwa amesimamishwa uanachama.
NAPENDA
KUKANUSHA KUWA HABARI ZILE NI ZA UONGO NA HAZINA UKWELI WOWOTE! CHADEMA IS MY LIFE STYLE!” anamaliza kutoa ufafanuzi wake.
Sehemu
ya habari hiyo iliyoleta utata kwa kumtaja Bw Makala kimakosa kuwa miongoni mwa
vijana waliosimamishwa Chadema ilisomeka hivi ikirejea kikao cha Kamati Tendaji
iliyoketi Januari 5, 2013 “Kikao hicho pia kilichukua uamuzi mgumu wa
kuwasimamisha uanachama kwa muda wa mwaka mmoja, Gwakisa Mwakisando (Mbeya),
Wilson Makala (Babati) na Joseph Kasambala (Mbeya)”
TAARIFA
RASMI YA BAVICHA
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA MAAMUZI YA KAMATI TENDAJI YA BARAZA LA VIJANA
CHADEMA (BAVICHA)
Ndugu waandishi wa habari, baadhi yenu mnafahamu
kuwa Baraza la Vijana la Chadema Taifa (BAVICHA), limefanya kikao cha kawaida
cha Kamati Tendaji, juzi 5 Januari 2013, katika Hotel ya Mbezi Garden jijini
Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine, kilijadili masuala matatu
mazito.
Kwanza, Kamati Tendaji ilijadili kwa kina suala la
kuporomoka kwa elimu nchini, ambapo serikali imepunguza alama za viwango vya
kufaulu, jambo ambalo limesababisha mamia ya wanafunzi waliochaguliwa kutokuwa
na sifa.
Pili, Kamati Tendaji ilijadili jinsi Bavicha
itakavyoshiriki katika maandalizi ya utekelezaji wa maazimio ya Kamati Kuu ya
Chadema yalioeleza kuwa mwaka 2013 ni mwaka wa nguvu ya umma. Tatu, Kamati Tendaji ilijadili kwa kina “Tuhuma za
usaliti na njama za kuvuruga chama, kutukana viongozi wakuu wa chama na
kuvuruga wanachama wa Chadema na Baraza kwa ujumla.”
Ndugu waandishi wa habari, vipo baadhi ya vyombo
vya habari jana na leo vimeripoti kwa upotoshaji mkubwa wa baadhi ya masuala
yaliyojadiliwa na kikao hicho.
Kwa mfano, gazeti moja la kila siku limemtaja
mwanachama wetu mmoja kuwa ndiye aliyekuwa mtoa taarifa wetu muhimu na kusema
mbunge mmoja wa CHADEMA alijadiliwa katika kikao hicho kuwa ni miongoni mwa
kundi hili la MASALIA na kufika mbali zaidi kwa kusema, “…sasa amekalia kuti
kavu.”
Lakini ukweli wa kilichojadiliwa kikaoni ni huu
ambao tunaueleza sasa:
Kwanza, kuhusu ajenda ya kuporomoka kwa elimu:
Kamati Tendaji imeagiza kuwa utafiti uliofanywa na BAVICHA katika ngazi ya
sekondari, ambao umegundua madudu mbalimbali, uongezwe hadi shule za Msingi na
taarifa yake ililetwe kwenye kikao kijacho cha Kamati Tendaji.
Kwenye ajenda ya pili: Kamati ya Utendaji BAVICHA,
ilipokea na kujadili agizo la Kamati Kuu ya Chama iliyoeleza kuwa mwaka 2013 ni
mwaka wa nguvu ya umma.
Katika ajenda ya tatu juu ya tuhuma za usaliti na
njama za kuvuruga chama, kutukana viongozi wakuu wa chama na kuvuruga wanachama
wa CHADEMA, na Baraza, Kamati ya Utendaji ilipokea taarifa ya Kamati Ndogo ya
Kamati Tendaji iliyoundwa Septemba mwaka jana kwenye kikao chake kilichofanyika
mjini Morogoro. Kamati ilipewa muda wa mwezi mmoja kukamilisha kazi hii.
Katika hili, watuhumiwa wakuu walikuwa ni kama
ifuatavyo:
Juliana Shonza, Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa Habib Mchange, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA, Mtela Mwampamba, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA, Gwakisa Burton Mwakasendo, mwanachama wa BAVICHA na
CHADEMA
Joseph Kasambala, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA
Aidha, baada ya Kamati iliyoundwa kuwahoji baadhi
ya watuhumiwa na wanachama wengine mbalimbali, ilibaini kwamba wapo baadhi ya
wanachama wa BAVICHA ambao wameshiriki kwa namna moja au nyingine katika tuhuma
hizi. Hao ni pamoja na Ben Saanane – maarufu kama Eight Oclock.
Katika orodha hiyo, wakatajwa pia Exaud Mamuya
lakini kamati ikashindwa kumpata Mamuya kwa kuwa hakukuwa na mawasiliano ya
kutosha.
Ndugu waandishi wa habari, hizi sasa ni tuhuma za
kila mmoja:
Ndugu
Juliana Shonza:
Alituhumiwa akiwa katika nafasi yake ya Makamu
Mwenyekiti wa BAVICHA, amekuwa akishirikiana na baadhi ya watu kupanga njama na
kufanya usaliti dhidi ya Baraza, Chama na vijana wenzake wapenda mabadiliko
nchini.
Amekuwa akifanya mikutano na vikao vya siri, kwa
manufaa ya CCM, akiwakusanya vijana wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali
waliosimamishwa masomo au kufukuzwa vyuoni kwa kutimiza wajibu wao wa kudai
haki zao za msingi na uwajibikaji wa serikali na ambao ni wanachama wa CHASO.
Juliana alifanya kazi yake hiyo kwa ushawishi wa
hongo, ili wakubali kuitisha mkutano na waandishi wa habari, watoe matamko
machafu dhidi ya CHADEMA na viongozi wake wakuu, akiwamo Dk. Willibrod Slaa na
Freeman Mbowe.
Mfano dhahiri hapa ni kikao alichofanya Baa ya
Highland iliyoko maeneo ya Makumbusho, majira ya saa 9 hadi saa 11, ambapo
aliwaita viongozi wa CHASO, akawashawishi kuwa watakuwa na maisha mazuri,
watarudishwa vyuoni na kutunzwa vizuri hapa mjini kama anavyoishi yeye, endapo
tu watakubali kufanya press conferences na kuisema CHADEMA kuwa inawavuruga
vijana walioko vyuoni.
Tarehe 6, Desemba, 2012 Hotel MIC, kuanzia saa 10
hadi saa 12, aliwaita baadhi ya vijana ambapo yeye na wenzake walipanga njama
za kukichafua chama na kutukana viongozi, kwa manufaa ya CCM.
Ifuatayo hapa chini ni moja ya sms ambazo Juliana
Shonza alikuwa akiwaandikia vijana katika ushawishi wake wa usaliti kwa
mapambano haya ambayo chama chetu kinafanya, kuwapigania Watanzania maskini na
wanyonge katika nchi yao;
“jembe chukua bodaboda basi jamaa washatia timu
hela yako yakulinda mfuko wako utaikuta tumempa eddo mnaetoa naye tamko
tutalindana tu jembe usijali.”
Huu ni moja tu kati ya ushahidi mwingi, wa meseji,
simu, sauti, video, picha na vikao kadhaa katika maeneo mbalimbali,
unaomwingiza Shonza na wenzake wengine katika sifa mbaya ya usaliti wa chama,
baraza na viongozi wake na wanachama wenzao na umma wa Watanzania kwa ujumla.
Hapo alikuwa akimwandikia mmoja wa viongozi wetu
ili ashiriki katika press conference ambayo yeye Makamu Mwenyekiti kwa
kushirikiana na wenzake wengine, walikuwa wameiandaa kwa nia ya kuchafua chama,
kulichafua baraza, kutukana viongozi waandamizi pamoja na kuvuruga na
kuchonganisha wanachama wa CHADEMA.
Matokeo ya kikao hicho cha MIC Hotel, yalionekana
siku moja baada ya kikao hicho, ambapo mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Edo
Mwamalala, aliyeshiriki kikao hicho cha MIC Hotel, aliitisha mkutano na
waandishi wa habari, akijitambulisha kuwa ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CHADEMA,
cheo ambacho hakuwa nacho.
Aidha, Shonza amekuwa akikutana na kufanya vikao
vya siri na wenzake, wakipanga njama za kufanya kazi na majukumu ya CCM
kuhujumu BAVICHA pamoja na CHADEMA. Mikakati ya kuvuruga baraza, kuchonganisha
wanachama na kutukana chama na viongozi wakuu, kwa siri na hadharani, imekuwa
ikipangwa katika vikao hivi.
Amebainika kukiuka kipengele cha 10.1(x) cha
Maadili ya Viongozi, cha Katiba toleo la mwaka 2006, kinachomtaka kiongozi
yeyote asitoe tuhuma zozote juu ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao
halali, kwa kuzingatia taratibu na kanuni za chama.
Ameonesha ubaguzi wa kikabila na kikanda kupitia
maandiko yake kwenye mtandao kwa kutumia jina lake, anapungukiwa na sifa muhimu
na mahsusi za kuwa kiongozi, kwa mujibu wa kipengele cha 10.1(iv) kinachomtaka
kiongozi yeyote asijihusishe na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini au
ukanda vinavyolenga kuleta ubaguzi ndani ya chama.
Kwa kushiriki vikao vya kuanzisha chama kipya
kinachoitwa CHAUMMA, kushiriki katika makundi yaitwayo MASALIA na PM7 ambayo
yote yalikuwa na lengo la kuvuruga chama na wanachama, kukosanisha na kutukana
viongozi wa chama, ndugu Shonza amevunja kipengele cha 10.1(i),(viii)(ix) na
ibara ya 10.2(iv).
Kwa kushiriki vikundi hivyo hapo juu, wajumbe wa
Kamati ya Utendaji ya BAVICHA wamejiridhisha pasi na shaka kuwa Shonza haendani
na katiba, falsafa, sera na maadili ya chama makini na tumaini la watu,
CHADEMA. Hivyo kwa mujibu wa ibara ya 5.1.4 na 5.1.5 anakosa sifa za kuwa
mwanachama wa Baraza la Chama.
Kwa kutoa tuhuma za uongo dhidi ya wanachama na
viongozi wenzake, ameendelea kuvunja kanuni za uendeshaji kazi za chama ibara
ya 10.1(viii).
Amehusika katika kuanzisha, kujihusisha na kuratibu
moja kwa moja kundi la vijana waliokuwa wakizunguka mikoani na kushawishi
viongozi wa vijana kutoa matamko kwa kutumia jina la CHADEMA kufanya kazi na
majukumu ya CCM ya kukichafua chama, kugombanisha wanachama na kumtukana Katibu
Mkuu kwa kutumia propaganda za CCM.
Kamati Ndogo ilimuita Ndugu Shonza ili kumhoji.
Lakini aligoma kwa madai kuwa haitambui kamati hiyo na wala hajui kuwa kuna
mgogoro, jambo ambalo limetushangaza wengi kwa kuwa Ndugu Shonza alikuwapo
katika kikao cha Morogoro kilichounda Kamati hii.
Ndugu Shonza pia hakuhudhuria kikao cha Kamati
Tendaji cha juzi kwa madai kuwa amebanwa na shughuli za familia. Baada ya
kupitia maelezo yote hayo, Kamati Tendaji iliamua yafuatayo:
Ndugu Juliana Shonza, amepoteza sifa na uhalali wa
kuwa mwanachama wa Chadema kwa kukiuka ibara ya 5.3.4 na ibara ya 10.1(ix) ya
katiba ya CHADEMA na hivyo imeamua kumuondoa katika nafasi yake ya makamu
mwenyekiti na kumfuta uwanachama wake.
Hivyo basi, kwa maamuzi hayo ya Kikao cha Kamati ya
Utendaji ya BAVICHA, kuanzia juzi tarehe 5 Januari 2013, Ndugu Juliana Shonza,
si mwanachama wa BAVICHA na hivyo moja kwa moja amepoteza sifa za kuwa kiongozi
wa baraza na kwa nafasi yake aliyokuwa nayo ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara.
Habib
Mchange:
Huyu alituhumiwa kutoa tuhuma za uongo, zikiwemo za
mauaji, kinyume na maadili ya Wanachama (kipengele cha 10.3(3); kuunda vikundi
vinavyojulikana kwa majina ya MASALIA na PM7 – Pindua Mbowe.
Pia Ndugu Mchange alituhumiwa kuwavuruga wanachama,
kuwachonganisha na kuwatukana viongozi, kisha kushiriki vikao vya kuanzisha
chama kingine cha siasa cha CHAUMMA.
Alituhumiwa pia kupotosha maamuzi halali ya vikao
vya chama na Baraza hivyo kuendelea kukipaka chama matope.
Kamati ilimuita Mchange, na kumhoji juu ya tuhuma
zinazomkabili. Hakufika. Badala yake, aliandika barua kueleza kuwa hana imani na
kamati:
Aidha, pamoja na Mchange kugoma kuhojiwa na Kamati
Ndogo ya Kamati Tendaji, Sekretarieti ya Kamati Tendaji Taifa, ilimuita Ndugu
Mchange kuhudhudhuria mkutano wa Kamati Tendaji ili kujibu tuhuma
zinazomkabili.
Mwaliko huu ulifanywa kwa njia ya barua na simu.
Njia hizo ndio zilizotumika kualika wahusika wote wakiwamo wajumbe wa Kamati
Tendaji,
Ndugu waandishi wa habari, baadhi yenu mnafahamu
kwamba Ndugu Mchange alikuwa miongoni mwa wanachama wa BAVICHA waliotaka
kuwania nafasi ya uenyekiti wa taifa wa baraza hili. Jina lake liliondolewa na
Kamati Kuu ya CHADEMA, kutokana na kukosa maadili ya uongozi.
Kamati Tendaji baada ya kusikiliza hoja yake hii,
ikajiridhisha kuwa mtuhumiwa ameamua kuibuka hoja hiyo ili kutaka Kamati
Tendaji isimjadili ili aendeleze mradi wake wa kukichafua chama akiwa ndani ya
chama.
Hivyo Kamati Tendaji imefanya yafuatayo: Imempata
na hatia ya kuvunja ibara ya 10.3(iii) na kwenda kinyume na kanuni za
uendeshaji wa chama ibara ya 10.3(4), kinyume na Maadili ya Wanachama (kipengele
cha 10.3(3); uendeshaji wa chama ibara ya 10.3(4) na kwamba mambo yote haya
yanadhihirisha kuwa Ndugu Mchange hayuko tayari kushirikiana na viongozi wake
kama mwanachama, hivyo kukiuka katiba ya chama ibara ya 5.3.4 na kuafikiwa
uamuzi wa kumfukuza uwanachama wa Bavicha na Chadema.
Mtela
Mwampamba:
Huyu ametuhumiwa kutoa tuhuma nzito za uongo
hadharani, zikiwemo za mauaji, kinyume kabisa na Maadili ya Wanachama
(kipengele 10.3(3).
Kuvunja katiba ya chama ibara ya 5.3.4 na Kanuni za
Uendeshaji kazi za chama Ibara ya 10.3(4) kwa kupotosha maamuzi halali ya vikao
vya chama na baraza na kukipaka matope chama pamoja na kudhihirisha kuwa hayuko
tayari kushirikiana na viongozi wake kama mwanachama.
3.Amevunja Katiba ya CHADEMA ibara ya 5.3.3 na
5.3.4 kwa kutoa kauli za kichochezi dhidi ya chama, kuwachonganisha wanachama
na kuwatukana viongozi.
4.Kwa kujiunga na vikundi vinavyoitwa MASALIA NA
PM7 na baadae kushiriki vikao vya kuanzisha chama cha CHAUMMA, Ndugu Mwampamba
amevunja ibara ya 10.3(iii).
5.Kinyume na ibara ya 5.3.3 na 5.3.4 ya Katiba ya
CHADEMA na Ibara ya 4.3(g) na (i) ya kanuni za BAVICHA, zinazopinga ubaguzi wa
aina yoyote ile, Ndugu Mwampamba ameonesha hisia za ubaguzi wa kikabila na
kikanda.
Gwakisa
Burton Mwakasendo:
Huyu amekuja kwenye kikao na kukiri kutenda makosa
yake ambayo takriban yote ni sawa yanayowahusu watuhumiwa waliotangulia hapo
juu. Mbele ya kikao cha Kamati ya Utendaji alikiri kushiriki vikao, akisema
kuwa ‘lakini’ alilazimika ‘kuikimbia’ dhambi kwa kuondoka katika baadhi ya
mikutano na watu hao, wakati mwingine hata nyumbani kwake hakuweza kulala
akihisi ‘dhambi’ hiyo anayoikimbia itamfuata nyumbani.
Kamati Tendaji, iliamua kumpa adhabu ya kuwekwa
chini ya uangalizi kwa mwaka mzima, katika wakati wote huo amezuiwa kugombea
nafasi yoyote ndani ya BAVICHA na onyo kali la barua.
Ben
Saanane:
Huyu pamoja na kwamba hakuwa miongoni mwa
watuhumiwa alipewa adhabu ya onyo kali na uangalizi wa miezi 12, kutokana na
makosa yafuatayo. Kutoa tuhuma nzito, zinazomhusu pia Kiongozi wa juu
mwandamizi wa chama, Ben amekiuka Maadili ya Wanachama (kipengele 10.3(3).
Kukiri kuwa mmoja wa waanzilishi wa vikundi
vinavyoitwa MASALIA na PM7 na kisha kushiriki vikao vya kuanzisha chama kingine
cha CHAUMMA, amevunja ibara ya 10.3(iii), kwa nia ya kuvuruga chama na kutukana
viongozi wake:
Mbele ya Kamati Tendaji, Ben alikiri makosa na
akaomba radhi.
Aidha, Ben alitoa ushirikiano mkubwa kwa Kamati
Ndogo jinsi ya kupatikana kwa taarifa na ushahidi wa namna wanachama wa BAVICHA
walivyokuwa wanafanya kazi za kundi hili la MASALIA na PM 7 na hasa juu ya
majina wanayotumia katika mitandao mbalimbali ya kijamii, wakifanya juhudi za
kuivuruga CHADEMA, kuvuruga BAVICHA, kutukana viongozi na kuwavuruga wanachama,
lakini kikubwa wakionesha kila dalili ya tabia ya usaliti.
Exaud
Mamuya:
Huyu hajapata nafasi ya kusikilizwa kwenye vikao.
Hivyo suala lake litaendelea kufanyiwa kazi na uongozi wa BAVICHA.
Aidha, kikao cha Kamati ya Utendaji pia kilipitisha
kwa kauli moja, moja ya maazimio ya BAVICHA Mkoa wa Mwanza, waliopendekeza
kufukuzwa uanachama kwa aliyekuwa Katibu wa Mkoa wa Mwanza, Salvatory Magafu,
kwa tuhuma za kukiuka Kanuni ya 10.1(xii) kwa kutoa tamko kwenye vyombo vya
habari kwa nia ya kumfarakanisha Katibu Mkuu na wanachama wa CHADEMA na umma wa
Watanzania, ikiwa ni sehemu ya uratibu wa kundi lililokuwa likiendeshwa na
watuhumiwa wengine hapo juu.
Kamati ya Utendaji pia ilimkuta na makosa ya
kiuongozi katika tuhuma zilizowasilishwa vikaoni na kufanyiwa kazi na Kamati
Ndogo, Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Mbeya, Joseph Kasambala na hivyo amepewa
adhabu ya onyo kali.
Hitimisho
Tunaomba kuwahakikishia vijana wenzetu wa CHADEMA
na wengine wote wapenda mabadiliko nchini, hakuna kijana mwanachama wa BAVICHA,
atafanya kazi za kuhujumu baraza na chama kwa ujumla na kusaliti matumaini
pekee ya Watanzania, akifanya kazi za mahasimu wetu, kisha akaachwa.
Ni lazima na muhimu tuoneshe kuwa tuna uthubutu kwa
kuchukua hatua kadri inavyotakiwa, pale panapotakiwa. Tuliopewa dhamana za
uongozi, tutatimiza wajibu kuhakikisha hakuna mtu ataonewa wala kupunjwa haki
yake katika kusimamia utendaji na utoaji utumishi bora wa baraza kwa wanachama
wake na chama kwa ujumla.
Daima tutasimamia katiba ya chama, maadili, kanuni,
taratibu, itifaki na miongozo ya mabaraza. Baraza hili halitakuwa tayari kuwa
sehemu ya kuruga matumaini makubwa ya Watanzania waliyonayo juu ya CHADEMA.
Baraza liko imara. Wanachama wetu wasifadhaishwe na
upotoshaji unaofanywa na wasaliti kuwa tumevurugika au ‘kumechafuka’. Hatuwezi
kuchafuka wala kuvurugika kwa kuchukua maamuzi dhidi ya watu wabinafsi
wanaotaka kukwamisha mapambano ya awamu ya pili, kupigania mabadiliko ya kweli
ya kimfumo na kiutawala, kwa ajili ya Watanzania.
Historia inatuonesha kuwa mara zote ambapo
mapambano yamefikia hatua ya juu ya kutimiza malengo, ndipo ambapo wasaliti
hujitokeza. Hivyo vikwazo hivi vya baadhi yetu kuanza kugeuka nyuma ni dalili
za mwisho mwisho kuwa ushindi unakaribia. Ni lazima kama vijana tuendelee
kujenga imani na matumaini ya Watanzania waliyonayo juu ya CHADEMA kutukabidhi
dola mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment