To Chat with me click here

Tuesday, January 15, 2013

MAKINDA, JAJI MKUU WATEMA CHECHE


Spika wa Bunge, Anne Makinda akiongea katika mkutano na Tume ya Mabadiliko ya Katiba jana, ambapo mhimili huo wa dola uliwasilisha maoni yake kwa Tume kuhusu Katiba Mpya. Wengine ni watumishi wa Bunge walioongozana naye. Picha Omega Ngole

MIHIMILI miwili ya Dola; Bunge na Mahakama, jana ilitoa maoni yake kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, huku Spika wa Bunge, Anne Makinda akitaka kuwe na mabunge mawili na kupendekeza kuwa Spika wa Bunge na mawaziri wasiwe wabunge.

Wakati Spika Makinda akitoa maoni hayo, Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman amesisitiza umuhimu wa Mahakama kutoingiliwa na wanasiasa na akapendekeza usawa katika upatikanaji wa haki kwa wananchi wote wa Tanzania.

Makinda akiwa na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah na viongozi wengine wa mhimili huo, alisema ni muhimu kuwe na Bunge la kuchaguliwa na wananchi na jingine la Seneti litakalotokana na wataalamu mbalimbali na viongozi wa zamani wenye uzoefu na walioitumikia nchi.

Alisema ni muhimu kukawa na aina hiyo ya mabunge pamoja na utaratibu wa wabunge kutokuwa mawaziri ili kulinda demokrasia ya kweli nchini.

“Tunataka Spika wa Bunge asiwe mbunge na pia mawaziri wasiwe wabunge. Wakuu wa mikoa na wilaya nao wasiwe wabunge. Pia tunataka Ibara ya 67 ya Katiba ya sasa ifanyiwe marekebisho ili kulinda demokrasia,” alisema Spika Makinda na kuongeza;

“Ibara hiyo inasema ili mtu awe mbunge lazima atokane na chama cha siasa, sasa Katiba Mpya ikataze kuwavua uanachama wabunge ambao wamechaguliwa na wananchi hata kama wanatokana na vyama vya siasa.”

Spika Makinda alisisitiza kwamba Bunge la Seneti litasaidia kuondoa mambo ya itikadi za vyama bungeni kama ilivyo sasa na kujali maslahi ya taifa katika kila jambo.

Spika asiwe mbunge
Makinda alisema umefika wakati Spika wa Bunge asitokane na wabunge na kwamba kama atachaguliwa kuwa Spika akiwa mbunge, ajiuzulu nafasi moja ili kuweza kulitumikia Bunge kiukamilifu.

Alisema Spika wa Bunge ni mwenye kazi nyingi hivyo ni vyema akapunguziwa majukumu hayo ili kutoa nafasi za kuendesha na kusimamia vizuri shughuli za Bunge.

“Tumependekeza Katiba Mpya itamke kwamba nafasi ya Spika wa Bunge haitatokana na ubunge na kama nafasi hiyo akipewa mbunge, atalazimika kujiuzulu nafasi moja,” alisema na kuongeza:

“Tumependekeza hivyo kutoa nafasi ya maspika wa Bunge kufanya kazi zao kikamilifu kwani nafasi hiyo ina mambo mengi sasa, ni vyema mabadiliko hayo yakatokea ili kuwapa nafasi wananchi wanaowachagua wabunge wao kutumikiwa kikamilifu,” alisema.

Mawaziri wasiwe wabunge

Makinda alisema ili kuhakikisha mgawanyo wa madaraka unaonekana kikamilifu wamependekeza Katiba Mpya ikataze mawaziri kuwa wabunge.

“Tumetaka kuondoa mgongano wa kimadaraka. Sisi tumependekeza kwamba Katiba Mpya ikataze mawaziri kuwa wabunge,” alisema Makinda na kuongeza:

“Mfano ni kwamba mbunge ana shida ya kupata fedha za maendeleo na waziri naye ana shida hiyohiyo katika jimbo lake, lazima atajijali yeye kwanza kwa kuwa ndiye anayepanga bajeti.”

Pia alisema wamependekeza Katiba Mpya ikataze wakuu wa mikoa na wilaya kuwa wabunge na kwamba wabunge wachaguliwe na wananchi tu.

Uhuru wa Mahakama
Jaji Mkuu Othman alisema Mahakama imewasilisha mapendekezo yake 12 kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, moja likiwa ni Katiba yenyewe kuwa msingi wa kutawala nchi.

“Katiba iwe ndiyo kitu bora chenye hadhi ya juu na kinapaswa kuwa chombo pekee cha kuongoza nchi na kusiwepo na mwanya wowote wa mtu au mhimili fulani kuikiuka. Tunataka Katiba ibaki kama dira ya kuongoza nchi kwa kuzingatia utawala wa sheria,” alisema Jaji Mkuu.

Pia alisema Katiba ijayo inatakiwa kusimamia utoaji haki sawa kwa wananchi wote. Jaji Mkuu alisema Katiba haina budi kutambua haki ya wananchi kupata haki katika mambo mbalimbali ikiwamo kuabudu na kuishi.

Katika hoja hiyo ya upatikanaji wa haki, Jaji Mkuu alisema kuna mikoa 12 na wilaya 25 nchini ambako hakuna Mahakama Kuu na Mahakama za Wilaya.

Alisema wananchi wanalazimika kutafuta haki zao kwenye mikoa na wilaya nyingine, tatizo ambalo Katiba Mpya inapaswa kuliondoa ili kuwafanya wananchi wote kuwa na fursa sawa katika kupata haki.

“Pia tumependekeza Katiba Mpya ilinde kwa hali na mali mhimili wa Mahakama kwa kuwa siyo wa kisiasa. Mahakama ni mhimili huru na haufungamani na upande wowote na hiyo ndiyo nguvu ya Mahakama. Isiwe na mambo ya kisiasa, upendeleo au kufungamana na upande mmoja,” alisema Jaji Mkuu.

Aidha, Jaji Mkuu alisema wamependekeza Rais aendelee kuwa mteuzi wa majaji nchini kwa kuwa ndiye mkuu wa nchi. Alisema atafanya uteuzi huo kwa kufuata ushauri atakaopewa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na si vinginevyo.

“Katiba ya sasa inasema kuwa Rais atafanya uteuzi kwa kushauriana na Mahakama, lakini sisi tumependekeza asishauriane na Mahakama, bali ateue kwa kufuata ushauri atakaopewa na Tume ya Utumishi ya Mahakama,” alisema.
Alisema haki za binadamu zinapaswa kupanuliwa na kulindwa katika Katiba ijayo. Alisema ilivyo sasa haki za kisiasa na kiraia ndizo zinazoonekana kupewa kipaumbele zaidi kuliko haki nyinginezo kama vile za uchumi na kijamii.

Tume ya Mipango
Kwa upande mwingine, Tume ya Mipango imependekeza Katiba Mpya iwe na ibara itakayoelezea uwajibishwaji na uwajibikaji wa viongozi wa Serikali.

Katibu wa Tume ya Mipango, Dk Philip Mpango alisema wametaka Katiba Mpya iwe na ibara itakayoelezea uwajibikaji wa viongozi wa Serikali pamoja na uwajibishwaji ili kuhakikisha wanawatumikia wananchi ipasavyo.

No comments:

Post a Comment