To Chat with me click here

Friday, January 4, 2013

CHUNGU NA TAMU YA VIGOGO 2012


BAADHI ya vigogo wa kisiasa hawatasahau yaliyowapata mwaka jana kutokana na mabadiliko makubwa yaliyoigusa medani hiyo na kusababisha kuanguka ama kwa kura au kung’olewa katika nafasi walizokuwa wakizishikilia.

Wakati baadhi wakiugulia kwa machungu hayo, kwa upande mwingine lipo kundi la wale wanaosherehekea neema iliyowajia mwaka huohuo, baada ya nyota zao kung’ara kisiasa na kujikuta wakikwaa nafasi za uongozi, pengine ambazo hawakuzitarajia.

Miongoni mwa matukio yaliyowatikisa wanasiasa ni hatua ya Rais Jakaya Kikwete kupangua Baraza la Mawaziri, kutenguliwa kwa baadhi ya matokeo ya chaguzi za wabunge na uchaguzi wa ndani wa CCM ambao uliwaweka kando baadhi ya vigogo wa chama hicho.

Kadhalika, yapo matukio yenye sura ya kipekee ambayo yanawagusa wanasiasa kama Godbless Lema ambaye alianguka kisiasa kwa ubunge wake kutenguliwa na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha mwanzoni mwa mwaka jana, lakini akaibuka tena shujaa baada ya kurejeshewa nafasi hiyo na Mahakama ya Rufani, Desemba 2012.

Tukio kubwa ambalo lilitikisa siasa za Tanzania ni lile la mabadiliko katika Baraza la Mawaziri ambayo yaliwaweka kando mawaziri sita ambao walikuwa wakiziongoza wizara nyeti zinazosimamia rasilimali za nchi na huduma za afya na uchukuzi.

Waliong’olewa ni Mustafa Mkulo (Fedha), William Ngeleja (Nishati na Madini), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Omari Nundu (Uchukuzi), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara) Dk Haji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii). Pia panga hilo liliwakumba waliokuwa Naibu Mawaziri, Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Dk Athuman Mfutakamba (Uchukuzi).

Kuanguka kwa Mkulo, Ngeleja na Maige kulitokana na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyozihusisha wizara zao na ufisadi. Dk Mponda na Dk Nkya, waling’olewa kutokana shinikizo la madaktari ambao walifanya mgomo uliotikisa sekta ya afya nchini.

Kwa upande wake, Nundu naibu wake, Dk Mfutakamba waling’olewa kutokana na kashfa ya ujenzi wa gati bandarini ambao uliwagawa kiasi cha kutofautiana bungeni, wakati Dk Chami naye aliponzwa na ugomvi na aliyekuwa naibu wake, Lazaro Nyalandu. Hata hivyo Nyalandu alipona baada ya kuhamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Walioula
Mabadiliko hayo yalikuwa neema kwa wateule wapya wakiwamo wale ambao hawakuwahi kuwa wanasiasa kama ilivyo kwa Profesa Sospeter Muhongo ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini.

Profesa Muhongo alipewa naibu wawili; George Simbachawene (Nishati) na Stephen Masele (Madini) ambao walikuwa wabunge.

Wabunge wengine walioula ni Dk William Ngimwa ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na kupewa naibu wawili ambao nao hawakuwa katika duru za kisiasa; Saada Mkuya Salum na Janeth Mbene. Ni wakati huohuo ambao Mwenyekiti wa NCCR -Mageuzi, James Mbatia aliteuliwa na Rais kuwa mbunge.

Mbunge wa Handeni, Dk Abdallah Kigoda naye aliteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, katika mabadiliko ambayo pia yalishuhudia baadhi ya waliokuwa naibu mawaziri wakipanda vyeo na kuwa mawaziri kamili.

Hao ni Dk Harrison Mwakyembe aliyeteuliwa kuongoza Wizara ya Uchukuzi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza.

Kabla ya uteuzi huo, Dk Mwakyembe alikuwa naibu katika Wizara ya Ujenzi, Kagasheki katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Chiza alikuwa naibu katika wizara hiyohiyo kama ilivyokuwa kwa Dk Mukangara aliyekuwa Habari na kupandishwa kuchukua nafasi ya Dk Emmanuel Nchimbi ambaye alihamishiwa Mambo ya Ndani, kuchukua nafasi ya Shamsi Vuai Nahodha aliyehamishiwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Nahodha alichukua nafasi ya Dk Hussein Mwinyi ambaye alihamishiwa Afya.
Katika mabadiliko hayo wabunge wengine waliteuliwa kuwa naibu mawaziri ambao ni Angela Kairuki (Katiba na Sheria), Januari Makamba (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Dk Seif Selemani Rashid (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Binilith Mahenge (Maji), Dk Charles Tzeba (Uchukuzi) na Amos Makala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo).

Mawaziri wengine waliohamishwa ni George Mkuchika, Profesa Jumanne Maghembe, Profesa Mark Mwandosya, Hawa Ghasia, Celina Kombani na Sofia Simba.

Naibu mawaziri waliohamishwa ni Gregory Teu, Pereira Ame Silima, Adam Malima, Charles Kitwanga na Gerson Lwenge.

Uchaguzi CCM
Uchaguzi wa ndani wa CCM nao ulisababisha mtikisiko kwa baadhi ya vigogo wa kisiasa akiwamo, aliyekuwa Katibu Mkuu, Wilson Mukama ambaye aling’olewa katika mabadiliko ya sekretarieti yaliyofanywa baada ya uchaguzi huo.

Tukio kubwa katika uchaguzi huo lilikuwa kurejea katika siasa za CCM kwa aliyepata kuwa Katibu Mkuu wake, Philip Mangula ambaye alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti (Bara), kuchukua nafasi ya Pius Msekwa ambaye tayari alikuwa ameomba kutoendelea na wadhifa wake.

Kadhalika Abdulrahman Kinana aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM huku aliyekuwa Mtunzahazina wa chama hicho, Lameck Mwigulu Nchemba akipanda cheo na kuwa Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara).

Katika mabadiliko ya Sekretarieti, pia Zakia Meghji aliteuliwa kuwa Mtunzahazina wakati aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk Asha-Rose Migiro aliteuliwa kuwa Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa chama hicho.

Katika ngazi za mikoa na jumuiya za chama hicho, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita aliangushwa huku Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga naye akiangushwa katika kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) kupitia Wilaya ya Ilala.

Matukio mengine
Mwaka jana, Bunge lilipoteza wabunge wawili ambao ni aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki (CCM), Jeremiah Sumari na aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Regia Mtema.

Kifo cha Sumari kilisababisha kufanyika kwa uchaguzi mdogo mwanzoni mwa Aprili ambao ulimwingiza bungeni, aliyekuwa mgombea wa Chadema, Joshua Nassari baada ya kumshinda Sioi Sumari wa CCM kwa kura zaidi ya 6,000. Cecilia Pareso wa Chadema, aliingia bungeni kuchukua nafasi ya Mtema.

Hata hivyo, wabunge wawili wa CCM; Aeshi Hilal (Sumbawanga Mjini) na Dk Dalaly Kafumu (Igunga) wameingia mwaka mpya wakiwa nje ya Bunge baada ya matokeo yaliyowapa ushindi kutenguliwa na Mahakama Kuu, uamuzi ambao wameupinga katika Mahakama ya Rufani.

No comments:

Post a Comment