WANACHAMA
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kata ya Gongo la Mboto Dar es
Salaam, wamemtaka diwani wa kata hiyo ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Ilala,
Jerry Silaa, kutoa ufafanuzi kuhusu kiasi cha sh milioni 100 kilichotengwa kwa
ajili ya matengezo ya barabara katika bajeti ya 2011/2012.
Akizungumza
juzi kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na wanachama hao, Katibu wa Jimbo
la Ukonga, Juma Mwaipopo, alieleza kuwa fedha hizo zilitengwa na Halmashauri ya
Ilala katika kipindi hicho ambazo hadi sasa hazijafahamika zilikokwenda.
Alifafanua
kuwa katika bajeti hiyo halmashauri ilitenga sh bilioni 93 kwa matumizi ya
jimbo hilo, zikiwemo sh milioni 100 kwa kata sita zilizo Gongo la Mboto ambazo
zingetumika kwa ajili ya upanuzi na matengenezo ya barabara pamoja na kusambaza
huduma ya maji kwa wananchi, jambo ambalo hadi sasa ni kitendawili.
Alisema
bado tatizo la huduma ya maji safi katika kata hiyo ni kitendawili ambacho
kimeshindikana kupatiwa ufumbuzi na serikali.
“Tunahitaji
kuwa na maamuzi ya pamoja juu ya Silaa, kwa sababu hatujui tumetoka wala
tunaelekea wapi hadi sasa? Inawezekana hajui kazi yake kwa sababu hatuna
maendeleo wala mabadiliko katika kata yetu, Watanzania tudai haki ambazo serikali
ilituahidi itazitekeleza bure,” alisema Mwaipopo.
Naye
Mbunge wa Jimbo la Nyamagana (CHADEMA), Ezekia Wenje, alitumia fursa hiyo
kueleza kuwa diwani huyo ameshindwa kutekeleza majukumu yake hasa kwa kushindwa
kukutana na wananchi wake walau kwa mwaka mara moja ili kutoa ufafanuzi juu ya
mapato na matumizi ya fedha yanavyotumika.
Alipopigiwa simu kujibu
tuhuma hizo diwani huyo alikata na kutuma ujumbe mfupi wa maneno: “Niko sehemu
tata; naomba unitumie ujumbe wa maneno (sms).”
No comments:
Post a Comment