Meli zinapakua makontena katika bandari ya Dar es Salaam tarehe 29 Disemba, 2012. |
Mamlaka
ya Bandari Tanzania (TPA) imeongeza ukusanyaji wa mapato katika bandari ya Dar
es Salaam kutoka shilingi bilioni 28 mwezi Novemba hadi shilingi bilioni 50
(dola milioni 18 hadi dola milioni 31) katika mwezi wa Disemba, kufuatia kusimamishwa
kwa muda maofisa 16 wa bandari wanaotuhumiwa kwa mwenendo usiofaa.
Maofisa
hao wa bandari, wakiwemo wakurugenzi wa ngazi za juu, walisimamishwa kwa muda
mwezi Disemba baada ya Wizara ya Usafirishaji kuanzisha uchunguzi wa ndani kwa
lengo la kutoa mwitikio wa malalamiko ya wateja kuhusu kucheleweshwa katika
bandari hiyo, kwa mujibu wa Waziri wa Usafirishaji Harrison Mwakyembe.
Maofisa
wa bandari wengine wasiopungua sita walisimamishwa mwezi Agosti. Uchunguzi huo,
ambao bado unaendelea, uligundua kuwa waajiriwa wa bandari walibadilisha
mwelekeo wa biashara kutoka katika bandari kwenda kwa kampuni ndogo za
usafirishaji na utoaji mizigo wanazomiliki, ukiukaji wa moja kwa moja wa
mkataba wao wa ajira.
"Wateja
wanakimbia bandari yetu kwa sababu ya ucheleshaji wa kukusudia unaofanywa na
waajiriwa wasio na maadili ambao wanaongeza gharama za kufanya biashara,"
Mwakyembe aliiambia Sabahi. "Hii ni kinyume na mikataba yao ya ajira na
wana mgongano wa maslahi na mwajiri wao [serikali]."
Miongoni
mwa viongozi wa bandari wa ngazi ya juu waliosimamishwa ni Mkurugenzi Mkuu wa
TPA Ephraim Mgawe, Mkurugenzi wa Mipango Florence Nkya, Mkurugenzi wa Uhandisi
Bakari Kilo, Mkurugenzi wa Mifumo ya Utawala Maimuna Mrisho, Mkurugenzi wa
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Ayub Kamili, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Hamad
Koshyuma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Julius Fuko, na Meneja wa Bandari Cassian
Ng'amilo.
Mashtaka
rasmi bado hayajatolewa dhidi ya viongozi waliosimamishwa na bado hawajajibu
tuhuma zozote hadharani. Mwakyembe alisema Bodi ya Wakurugenzi ya TPA itakutana
hivi karibuni kutoa uamuzi wa mwisho kuhusiana na ajira yao.
Kwa
kawaida, makampuni ya kupokea na kusafirisha mizigo hutoza shilingi 640,000
(dola 400) kuondoa kontena lenye futi 20 hadi 40 kutoka bandarini ndani ya siku
saba. Makontena ambayo hayajalipiwa ndani ya muda huo uliyotengwa hutozwa fedha
za ziada.
Mwakyembe
alisema wateja wanalalamika kwamba kulipia na kutoa kontena katika bandari ya
Dar es Salaam kumekuwa kukichukua hadi wiki nane, wakati inachukua siku saba tu
katika bandari ya Mombasa nchini Kenya.
Wateja
wanataka bidhaa kuondolewa bandarini katika kipindi kifupi kadri iwezekanavyo,
Mwakyembe alisema, na pale ambapo kuna ucheleweshaji bandari ya Dar es Salaam,
wanahamishia mizigo yao katika bandari nyingine, ambako kunasababisha serikali
ya Tanzania kupoteza mapato.
Mwakyembe
alisema makampuni binafsi yanayomilikiwa na viongozi tangu wakati huo
yamesimamishwa na biashara imerejea bandarini, na kuchangia ongezeko la mapato
ya Disemba.
Makampuni ya kuagiza na kusafirisha bidhaa nje yakaribisha marekebisho
Vincent
Nyerere, anayemiliki kampuni ya kuagiza bidhaa, alikubaliana na kusimamishwa
kwa viongozi wa bandari, lakini alisema bado jitihada zaidi zinatakiwa ili
kuboresha biashara bandarini, kwa kuwa bado inaenda taratibu.
Alisema
aliagiza makontena manne kutoka China mwezi Novemba -- mawili yaliingizwa
kupitia bandari ya Mombasa na mawili kupitia Dar es Salaam. Makontena
yaliyopitia Mombasa yaliondolewa ndani ya siku tisa, wakati yale yaliyopitia
Dar es Salaam yaliendelea kukwama katika bandari ya Dar es Salaam hadi tarehe 7
Januari.
"Lengo
langu lilikuwa ni kuuza bidhaa katika wiki la kati ya Krismasi na mwaka mpya
lakini sasa kama nikipata bidhaa hizo zote nitazifanyia nini?" aliiambia
Sabahi. "Bandari [ya Dar es Salaam] imeua kabisa biashara yangu."
Nyerere
alisema kama bandari ingekuwa na utaratibu mzuri na kufanya kazi kwa ufanisi,
ingeweza kuzalisha hadi shilingi bilioni 100 (dola milioni 63) kwa mapato ya
mwezi.
Haron
Ishimwabula, ambaye kampuni yake ya usafirishaji nje na uingizaji wa bidhaa
inahudumia Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Malawi na Zambia,
alisema kwamba kwa sababu ya kutofanya kazi kwa ufanisi katika bandari ya Dar
es Salaam, anatumia bandari ya Mombasa ili kuingizia bidhaa kwa haraka hata
kama inaongeza gharama katika biashara yake.
Mchumi
Benson Mahenya, mkurugenzi wa Andrew's Consulting Group, alisema serikali
inapoteza mapato mengi sana kwa bandari shindani katika nchi za eneo hili. Kwa
kuwa ni eneo la kimkakati, bandari inaweza kuzalisha hadi asilimia 60 katika
bajeti ya taifa, aliiambia Sabahi, lakini kwa sababu ya kutokuweko kwa ufanisi
mapato yanayotarajiwa kupatikana hayafikiwi.
Mahenya
alipongeza jitihada za Mwakyembe kuboresha utendaji wa bandari na kuwaomba kila
mmoja kuunga mkono mabadiliko yanayokusudia kuondoa ufisadi.
Hata
hivyo, alisema mfumo wa uchukuzi katika bandari pia unahitaji maboresho. Kwa
mfano, badala ya kutumia magari makubwa ya mizigo, mfumo wa reli unapaswa
kuhuishwa kwa ajili ya shehena kubwa na usafirishaji wa haraka wa bidhaa kutoka
bandarini, alisema Mahenya.
Mwakyembe
alisema maboresho ya utendaji bandarini ni endelevu na wizara yake itaendelea
kukagua njia za kuboresha ufanisi. Alisema wizara hiyo inazingatia kufanya kazi
katika bandari kwa saa 24 ili kuondoa shehena ya kontena ambazo zinatakiwa
kutolewa.
No comments:
Post a Comment