RAIS
Jakaya Kikwete alitoa salamu zake za mwaka mpya kwa kuzungumzia mambo
mbalimbali ya kitaifa, huku akibainisha kuwa Bunge la Katiba, litakaa Novemba
mwaka huu kupitisha mapendekezo ya Katiba Mpya.
Katika
hotuba yake hiyo, Rais Kikwete alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imekamilisha hatua ya kwanza ya kukusanya maoni ya mtu mmojammoja nchi nzima na
hatua inayofuata ni ya kukusanya maoni ya makundi maalumu.
“Kazi
hiyo ya kukusanya maoni ya makundi maalumu, itaanza Januari 2013. Natoa wito
kwa makundi hayo nayo kushiriki vizuri kwenye hatua hii muhimu. Baada ya hatua
hiyo kukamilika, Tume itaandaa Rasimu ya Katiba ambayo wanategemea itakuwa
tayari Mei, 2013.”
Rais
Kikwete alisema Tume itatangaza muundo na namna ya kuwapata wajumbe wa Mabaraza
ya Katiba na baada ya kuwapata rasimu hiyo ya Katiba itawasilishwa kwenye vikao
vya Mabaraza hayo vitakavyofanyika kati ya Juni na Agosti, 2013.
“Baada
ya kukamilika kwa vikao vya Mabaraza ya Katiba, Tume itakamilisha Rasimu ya
Katiba ambayo itachapishwa kwenye Gazeti la Serikali kama yalivyo matakwa ya
sheria. Aidha, itachapishwa katika magazeti ya kawaida kwa wananchi kusoma.
Novemba,
2013 rasimu hiyo itawasilishwa kwenye Bunge Maalumu kujadiliwa na kupitishwa. Baada
ya Bunge Maalumu kupitisha itapelekwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kupitia
kura ya maoni,” alisema.
Rais
Kikwete alieleza kama kila kitu kitakwenda kama inavyotarajiwa, Katiba Mpya
iliyotokana na maoni na matakwa ya wananchi itapatikana ifikapo mwaka 2014.
“Mwaka
huo Muungano wetu utakuwa unatimiza miaka 50, hivyo hiyo itakuwa zawadi ya tunu
kubwa. Tukifanikiwa kupata Katiba Mpya wakati huo, tutafanya Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015 kwa kutumia Katiba hiyo,” alisema.
Huduma za treni kusambaa Dar
Katika
hatua nyingine, Rais Kikwete amewaahidi wakazi wa Dar es Salaam kuwa Serikali
itapanua usafiri wa treni kwa kuanzisha safari nyingine kutoka katikati ya Jiji
kwenda maeneo ya pembezoni.
Alisema
kazi hiyo iliyopangwa kuanza mwaka huu, inalenga kufikisha huduma za treni
maeneo ya Tegeta, Kibaha na Mbagala Rangi Tatu, huku kukiwa na maboresho
stahiki kwa treni zilizokwishaanza kazi
Rais
Kikwete alisema tayari mshauri mwelekezi ameshateuliwa kufanya upembuzi
yakinifu kwenye maeneo hayo… “Tunataka huduma hiyo iweze kufika Tegeta, Kimara,
Luguruni, Kibaha Mbagala Rangi Tatu na Kongowe. Tuliamua kuanza na reli iliyopo
lakini nia yetu ni kufanya vile hasa inavyotakiwa iwe kwa usafiri wa treni
mijini.”
Hivi
sasa usafiri wa treni unaanzia katikati ya Jiji hadi Ubungo na Tazara hadi Pugu
Mwakanga.
Alisema
mbali na kuanzisha treni hizo, Serikali pia inajipanga kuanza ujenzi wa
barabara za juu kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar
es Salaam.
“Ujenzi
huo utaanza mwaka katika maeneo ya Tazara na Ubungo na matayarisho
yamekwishaanza,” alisema.
Suala la gesi
Rais
Kikwete pia alizungumzia mgogoro wa gesi ulioanza kufukuta kwa wakazi wa Mkoa
wa Mtwara kuizuia isisafirishwe kwenda Dar es Salaam akisema, si sahihi kwani
rasilimali za nchi ni kwa ajili Watanzania wote.
“Sharti
la kutaka gesi isisafirishwe kwenda kokote halikubaliki. Rasilimali
inayopatikana popote ni mali ya Taifa zima,” alisema Rais Kikwete.
Alisema
wakazi wa Mikoa ya Mtwara na Lindi watanufaika na uchumi wa gesi sawia na
Watanzania wengine na wala wasifikirie kuwa rasilimali hiyo ni yao peke yao.
No comments:
Post a Comment