AMTAKA ASITUMIE MALI ZA
SERIKALI KWA KAZI ZA CCM
MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amemtaka Rais Jakaya Kikwete,
kuacha kutumia mali za serikali kwa ajili ya kufanya shughuli za Chama chake
cha Mapinduzi (CCM).
Angalizo
hilo la Zitto limekuja wakati Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM,
akitarajiwa kuwasili mkoani Kigoma wakati wowote kwa ajili ya sherehe za
maadhimisho ya miaka 36 ya chama hicho.
Rais
pia atatumia nafasi hiyo kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo
iliyotekelezwa na serikali kuu na halmashauri.
Akihutubia
mkutano wa hadhara jana mjini hapa, Zitto alimtaka Rais Kikwete kama anakuja
kwenye shughuli za CCM aje kwa gharama za chama chake na si kwa gharama za
serikali.
“Rais
anakuja kwenye shughuli za CCM, ndege atakayopanda ni ya serikali. Tunasema
kama unakuja kwenye shughuli za CCM njoo kwa gharama za CCM,” alisema.
Zitto
ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, aliongeza kuwa Rais Kikwete
asichanganye kazi za CCM na kazi za serikali na kuongeza kuwa hana kinyongo
naye kwa kuwa vitu alivyofanya mkoa wa Kigoma vinaonekana kulinganisha na
marais waliotangulia.
“Sisi
hatuna kinyongo naye, maanake Nyerere alipita hakuna kitu, Mwinyi amepita hamna
kitu, Mkapa alipita hamna, yeye kaja kuna vitu tumeviona, hatuna kinyongo naye
lakini asije kwa gharama za serikali kwa mambo ya CCM, asichanganye kwa kuwa si
utawala bora.
“Haiwezekani
miradi ya maendeleo ya halmashauri kama ile stendi ya mabasi ya daladala ya
kituo cha stesheni, ni mradi wa halmashauri, Rais anakuja kuzindua hatukatai
lakini kama anakuja kwa shughuli za CCM amalize mambo yao kwanza arudi Dar es
Salaam halafu aje kiserikali atufungulie miradi,” alisema.
Aliwataka
madiwani wa CHADEMA kutotoa ushirikiano kama Rais anakuja kwa shughuli za CCM
kufungua miradi ya maendeleo kwa sababu itakuwa ni propaganda ya CCM.
“Hatuwezi
kuruhusu mkuu wa nchi kutumia fedha za nchi kufanya kazi ya CCM na usalama wa
taifa mlioko hapa mpeleke taarifa,” aling’aka.
Katika
hatua nyingine Zitto pia amemtaka mkuu wa mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali mstaafu
Issa Mchibya asiende kukagua miradi ya maendeleo akiwa na katibu wa CCM kwa
gari la serikali na kwamba kuanzia leo wataanza kufanya ufuatiliaji.
No comments:
Post a Comment