MWENYEKITI
wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza kusudio la chama chake kuanzisha
‘Libeneke’ alilosema Serikali itashindwa kulizima na kudai kufanyika kwa
uchaguzi mdogo katika kata tano za Jiji la Arusha zilizowazi kwa zaidi ya mwaka
mmoja sasa.
Kata
za Kimandolu, Themi, Kaloleni na Elerai ziko wazi tangu Agosti 7, mwaka juzi
baada ya waliokuwa madiwani, Estomih Malla, Reuben Ngowi, Charles Mpanda na
John Bayo na wa viti maalum, Rehema Mohamed kufukuzwa uanachama wa
Chadema kwa kosa la kukaidi maagizo ya kamati kuu kuhusu mwafaka wa mgogoro wa
Umeya.
Kata
ya Sombetini yenyewe iko wazi baada ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Alphonce
Mawazo kuhamia Chadema akitoka CCM.
Mbowe
alisema chama chake kitachukua mkondo wa shinikizo kwa Serikali na NEC baada ya
kubaini mbinu za kuchelewesha makusudi uchaguzi katika kata hizo kwa kile
kinachoaminiwa ni hofu ya CCM kuwa kata hizo zitatwaliwa na Chadema.
Akizungumza
Arusha jana, wakati wa hafla fupi ya kupokea hati za kiwanja chenye ukubwa wa
hekari tatu kutoka kwa Kampuni ya Mawala Trust kwa ajili ya ujenzi wa hospitali
maalumu ya Mama na Mtoto, Mbowe alisema wananchi wa kata hizo wana haki ya
uwakilishi na Chadema itawasaidia kuidai.
Alisema
chama chake pia kitaendesha kampeni ya kudai uchaguzi mdogo Sengerema na
Buchosa alikosema pia kuna kata ziko wazi baada ya waliokuwa madiwani kupitia
tiketi ya CCM kuhamia Chadema zaidi ya mwaka mmoja uliyopita.
“Tunataka
uchaguzi mdogo ufanyike katika kata hizi kulingana na matakwa ya sheria.
Tushinde Chadema, CCM, TLP, NCCR-Mageuzi au CUF sawa. Muhimu wananchi wapate
haki ya uwakilishi kwenye vikao vya baraza la madiwani,” alisisitiza Mbowe.
Baada
ya kuvuliwa uanachama, Mallah na wenzake wanne walifungua kesi kupinga uamuzi
huo katika mahakama ya hakimu mkazi Arusha, ambapo walishindwa na kukata rufaa
Mahakama Kuu kabla ya kuamua kuifuta kwa hiari Septemba 5, mwaka huu.
Waliokuwa
madiwani hao ambao walikuwa wakitetewa na Wakili Severin Lawena, hivi sasa
wameamriwa kuilipa Chadema fidia ya zaidi ya Sh15 milioni, baada ya Hakimu
Mfawidhi, Charles Magessa kukubaliana na ombi la madai yaliyowasilishwa na
Wakili Method Kimomogoro anayekiwakilisha Chadema na Mbowe aliyekuwa mdaiwa wa
pili katika kesi ya msingi.
No comments:
Post a Comment