To Chat with me click here

Thursday, February 7, 2013

HAKIELIMU YAIBANA SERIKALI

Ms. Elizabeth Misokia
Katika hatua nyingine, serikali imetakiwa kuacha ubabe wa kupangua hoja zinazotolewa na watalaamu wa masuala ya elimu, ambao wanafanya utafiti na kuainisha upungufu uliopo katika sekta hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na wanaharakati wa masuala ya elimu, ambao wameunga mkono hoja iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni na Mbatia, aliyetaka Bunge lichunguze udhaifu uliopo katika sekta ya elimu nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la HakiElimu linalojishughulisha na masuala ya elimu, Elizabeth Misokia, aliwaaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa Tanzania ni ya Watanzania wote na kwamba, kitendo cha serikali kukosoa tafiti za watalaamu na kuzitupa, hakilengi kuijenga nchi na kuinua kiwango cha elimu nchini.

“Serikali isitumie nguvu nyingi kukosoa tafiti mbalimbali zinazofanywa na watalaamu kuhusu elimu, badala yake izifanyie kazi ili kuziboresha,” alisema Misokia.

Alisema sera ya elimu ya mwaka 1995 haieleweki inasema nini kuhusu elimu na kwamba, hata mitaala ya kufundishia nayo haileweki kwa walimu wanaoitumia kufundishia.

Misokia alisema sekta ya elimu nchini inakabiliwa na matatizo mengi, ukiwamo uhaba wa walimu, walimu kukata tamaa kutokana na serikali kuwapuuza, kushindwa kuwalipa madai yao ya siku nyingi pamoja na kufanya kazi katika mazingira magumu.

Matatizo mengine yanayoikabili sekta ya elimu, ni pamoja na wakaguzi kushindwa kufika katika shule mbalimbali kwa ajili ya kuzikagua. Alisema kati ya mwaka 2000 hadi 2002 elimu ya shule ya msingi ilipanuliwa, lakini hakuna juhudi zozote za kuwapo sera moja ya elimu itakayoisimamia kikamilifu.

Aliomba serikali kutengeneza kwanza sera yenye nguvu kuhusu elimu kabla ya kuanza kuandaa mitaala inayofanana nchini kote ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu inayofanana na iliyo bora.
 

No comments:

Post a Comment