To Chat with me click here

Monday, February 11, 2013

CHADEMA IMEMSHTAKI SPIKA MAKINDA



VIONGOZI wa ngazi ya juu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamemshitaki Spika wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Anne Makinda kwa wapigakura, kutokana na kitendo chake cha kushindwa kusimamia maadili ya Bunge hilo.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo katika viwanja wa Tandika Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam, viongozi hao walisema kwamba Makinda ameshindwa kuliongoza bunge hilo, badala yake anafanyakazi ya kukwamisha hoja binafsi zinazotolewa na wabunge wa upinzani zenye lengo a kuboresha maslahi ya wananchi.

"Nilishangazwa na uongo wa Spika Makinda bungeni akieleza kuwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe alisimama kwa kifungu 53 (c) wakati alisimama kwa kutumia kifungu 51(c) akipendekeza kuondolewa bungeni kwa hoja binafsi ya Mnyika"alisema Katibu Mkuu wa Chama hicho Dk Willibrod Slaa.    

Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe alisema kwamba  namna mijadala ya Bunge inavyoendeshwa, namna Spika anavyobeba ajenda za Serikali katika kujenga Bunge kibogoyo na namna anavyofanya maamuzi kwa kukurupuka, inahitaji hatua za kuokoa misingi ya uwajibikaji wa nchi.

"Ni lazima Spika wa Bunge adhibitiwe kwa kuondolewa katika nafasi hiyo haraka iwezekanavyo. Spika lazima ajue kwamba Mamlaka yapo kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la wananchi liitwalo Bunge. Anna Makinda lazima adhibitiwe, vinginevyo nchi itaumia"alisema Zitto.

Naye Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alisema kwamba, kazi yao ni kufanya kile walichotumwa na watanzania, na baada ya hapo wanarudisha majibu ya kazi zao, "Sisi kazi yetu ni kutekeleza kile mlichotuagiza tukakifanye na baada ya hapo tunarudisha majibu kwenu, haya ndiyo majibu ya kazi tuliyoifanya katika Bunge hili, mtaamua wenyewe cha kufany kwani tulisema kwamba tutakuja kumshtaki kwenu na tumefanya hivyo, sasa zamu yenu kutoa hukumu juu yao"alisema Mbowe

No comments:

Post a Comment