KIONGOZI
wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amembana Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, akitaka serikali iwachukulie hatua watendaji waliozembea
kudhibiti vurugu za mzozo wa gesi Mtwara.
Mbowe
pia alimhenyesha Pinda akimtaka alihakikishie Bunge ni lini serikali itakuwa
tayari kuweka wazi mikataba kadhaa ikiwamo ya mafuta na gesi asili ili kuondoa
upotoshaji wa miradi hiyo kama ilivyotokea Mtwara.
Akiuliza
swali hilo bungeni jana mjini hapa, Mbowe alisema kwa kuwa vurugu hizo
zimetokana na uzembe wa kisiasa na viongozi wakiwamo wa vyombo vya dola
kushindwa kubaini na kudhibiti ghasia hizo mapema, kwanini wasichukuliwe hatua
kwa uzembe huo.
Akijibu
maswali hayo, Pinda alirejea kauli yake ya mara kwa mara tangu alipotoka
kusuluhisha mzozo huo Mtwara, akisema vyama vya siasa vimechangia sana kukuza
na kupotosha ukweli wa mradi huo.
Alisema
wanasiasa walitumia mzozo huo kujiimarisha kisiasa na kujijenga kwa ajili ya
uchaguzi unaokuja. "Suala
la kuwawajibisha watendaji hao liko chini ya waziri mkuu na rais,
tutaliangalia,” alisema Pinda.
Hata
hivyo, Pinda alisema jambo la msingi si kutafuta mchawi, kwani tatizo la Mtwara
ni la wote, na siku zijazo kutakuwa na ushirikishwaji wa jamii katika kutoa elimu
ili kuepuka madhara kama yaliyotokea Mtwara.
Kuhusu
kuweka wazi mikataba ili kuondoa upotoshaji, Pinda alisema mikataba hiyo haina
siri na inaweza kuwekwa wazi kupitia mifumo ya kibunge.
Hata
hivyo, Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), hakuridhika na majibu hayo na katika maswali yake ya nyongeza
alimtaka waziri mkuu kutamka wazi bila kumng’unya maneno kama serikali iko
tayari kuweka mikataba hiyo wazi.
Pia
alihoji ni kwa nini serikali iko tayari kutekeleza kero za wananchi pale
inapobanwa kwa presha na maandamano kama ilivyotokea Mtwara.
Katika
hoja hiyo, Pinda alisema serikali haiko tayari kuweka wazi mikataba hiyo
kupitia magazeti, kwani mingine ina taratibu zake lakini iko tayari kuweka wazi
kupitia mifumo ya kibunge.
Kuhusu
serikali kusikiliza kero za wananchi baada ya presha za maandamano, Pinda
alisema maandamano si njia sahihi ya kuwasilisha madai ya wananchi. "Ndugu
yangu Mbowe anajaribu kuleta hoja ambayo haina mashiko. Mimi siamini kuwa
maandamano ndiyo njia sahihi ya kuwasilisha malalamiko ya wananchi,” alisema
Pinda.
Mapema
kabla ya maswali kwake, Pinda alitoa taarifa ya kueleza kuhusu vurugu za Mtwara
pamoja na madhara yaliyojitokeza, ambapo hata hivyo alirudia kile alichowaeleza
waandishi wa habari juzi.
Alisema
kulikuwa na upotoshaji mkubwa kwamba bomba hilo la gesi lingeishia Bagamoyo
ambako inajengwa bandari ya kusafirishia gesi hiyo nje na kumhusisha Rais
Jakaya Kikwete, jambo ambalo si la kweli kabisa.
Waziri
Mkuu Pinda aliwatangazia wabunge uharibifu wa mali na hasara iliyopatikana
kutokana na vurugu hizo, sambamba na kuorodhesha majina ya watu waliochomewa
nyumba, magari na mali nyingine.
Pia
alitaja majengo na ofisi za serikali zilizochomwa moto pamoja na magari, ambapo
uharibifu huo umesababisha hasara ya mabilioni ya fedha, akisema serikali
itaangalia namna ya kuwafidia.
Wakati
akitaja majina ya watu waliochomewa nyumba na mali zao, Mbunge wa Viti Maalumu,
Mariam Kasembe, alitokwa machozi ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Hali
hiyo ilifanya baadhi ya wabunge wanaokaa jirani naye kumtoa nje ya ukumbi na
kumbembeleza huku wakimpa pole. Mbunge
huyo ni mmoja wa wabunge waliochomewa nyumba, magari na mali nyingine. Wengine
ni Anna Abdallah na Hawa Ghasia, ambao nyumba zao ziliteketezwa kabisa.
Tume ya Spika yayeyuka
Spika
wa Bunge, Anne Makinda, ametengua uamuzi wake wa kutaka kuunda kamati ya Bunge
kwa ajili ya kuchunguza sakata la vurugu za Mtwara. Akitangaza
uamuzi huo jana, Makinda alisema baada ya taarifa ya waziri mkuu kuhusu mzozo
huo, hakuna haja ya kuunda tume hiyo.
"Kwa
vile taarifa ya serikali imejitosheleza, Bunge hatuna sababu tena ya kuunda
tume. Nampongeza waziri mkuu kwa kazi aliyoifanya na niwapongeze wananchi wa
Mtwara kwa kuelewa na kudumisha amani,” alisema.
Mnyika awapinga
Waziri
Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amesema hajaridhika na taarifa ya
waziri mkuu pamoja na uamuzi wa Spika kuhusu mgogoro wa gesi mkoani Mtwara.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo,
alisema kuwa taarifa zinadhihirisha kwamba nchi imefika hali hiyo kutokana na
udhaifu wa serikali na ombwe la kiuongozi na kiusimamizi ikiwamo wa kibunge.
Alisema
kuwa taarifa ya waziri mkuu ilijibu baadhi tu ya madai ya wananchi lakini pia
imefafanua sehemu ndogo ya masuala ambayo aliyahoji bungeni Julai 27, mwaka
jana, lakini serikali ikakwepa kutoa ufafanuzi.
“Taarifa
hiyo itawezesha kutuliza mgogoro kwa muda lakini haijengi msingi wa ufumbuzi
endelevu. Sikubaliani na uamuzi wa spika wa kubadili uamuzi wake wa awali
alioutangaza wa kuunda kamati kufuatia maelezo ya waziri mkuu yasiyokuwa na
vielelezo vyovyote, kwa kuwa kufanya hivyo ni kulinyima Bunge fursa ya
kuisimamia serikali ambayo ndiyo chanzo cha migogoro kuhusu gesi asili,”
alisema.
Alisema
kuwa ikiwa Spika amebadili uamuzi wa kuunda kamati ya kwenda Mtwara alipaswa
aunde Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ili ipitie vielelezo kubaini usahihi
wa maelezo hayo ya waziri mkuu bungeni katika hali ya sasa.
Mnyika
aliongeza kuwa waziri mkuu hajatoa maelezo kamili kuhusu mipango ya matumizi ya
gesi asili katika eneo la viwanda Bagamoyo na ujenzi wa Bandari ya Mbegani.
“Spika
wa Bunge atumie mamlaka yake kuelekeza kamati mojawapo ya kudumu ya Bunge
kushughulikia suala la gesi asili kama nilivyoomba katika barua zangu kwake za
Oktoba 2012 na Januari 2013, ambazo hadi sasa hazijapatiwa majibu,” alisema
Mnyika.
No comments:
Post a Comment