To Chat with me click here

Monday, February 4, 2013

NAIBU WAZIRI JANUARY MAKAMBA AVAMIWA NA MAJAMBAZI



USIKU wa kuamkia jana majambazi wamevamia nyumbani kwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba. January alisema wakati majambazi hao wanavamia katika nyumba yake iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam, kati ya saa tisa na saa 10 alfajiri ya jana, yeye alikuwa jimboni kwake Bumbuli kuhudhuria msiba.

“Baada ya Bunge kuahirishwa nilienda jimboni kuhudhuria msiba wa mzee mmoja maarufu kule kwetu, kwa hiyo sikuwapo nyumbani wakati tukio hilo linatokea.

“Nyumbani alibaki mke na watoto wangu, majambazi wanne waliingia ndani lakini cha ajabu hawakuiba kitu chochote kwa sababu chini sebuleni kulikuwa na laptop, ipad na samani nyingine.

“Si hivyo tu, bali walifanikiwa kupanda juu na kuingia katika ofisi yangu ya nyumbani, nako pia hawakuchukua chochote.

“Kwa bahati nzuri mke wangu alifanikiwa kubonyeza kitufe na alarm ya kampuni ya ultimate security, ikaanza kulia ndipo majirani nao wakatokea kutoa msaada, lakini majambazi hao wakafanikiwa kukimbia. Baada ya kukimbia waliacha kamba sebuleni na tape ya kuzibia midomo,” alisema January.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema majambazi hao walifanikiwa kuingia katika nyumba hiyo baada ya kumfunga kamba mlinzi.

Alisema baada ya kumdhibiti mlinzi walifanikiwa kuingia ndani ya nyumba hiyo kupitia madirishani.

“Walipomfunga kamba mlinzi, waliingia ndani kupitia katika madirisha yenye vioo vya aluminium na wengine walibaki nje. Kwa bahati nzuri kelele za majirani na zile za waliokuwa ndani ya nyumba hiyo zikawakimbiza.

“Hawakufanikiwa kuiba chochote na wala kumjeruhi mtu yeyote, ilibidi wakimbie tu kuokoa maisha yao maana nyumba ya January waliyoingia ni ghorofa halafu ina uzio, sasa kama wangeendelea kubaki maana yake wangekutwa na siku hizi raia wakiwakamata majambazi kinachofuata ni kuwaua.

“Polisi walifanikiwa kufika eneo la tukio na kwa kuwa majambazi hao waliwahi kukimbia, tumeshindwa kutambua walikuwa na silaha za aina gani,” alisema Kenyela.

Alisema wameshaanza kufanya msako mkali kuhakikisha majambazi hao wanawakamata.

“Tumeshaanza kufanya msako na tutawakamata wote waliovamia nyumba hiyo, siku hizi jeshi letu limeimarika mno na tutawakamata hao na wahalifu wengine wanaofanya vitendo viovu katika maeneo mbalimbali,” alisema Kenyela.

No comments:

Post a Comment