To Chat with me click here

Monday, February 18, 2013

DALILI ZA KIFO CHA CCM HIZI HAPA



CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake vinaelekea katika kifo, lakini viongozi, makada, mashabiki na wanachama wake hawataki kusikia utabiri wa chama chao kuelekea kuzimu.

Hawataki kusikia hilo licha ya kuziona dalili kila uchao na uchwao. Wanazisadiki kauli za mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete kuwa wanaoitabiria kifo CCM wataanza kufa wao wakiiacha.

Si vibaya leo kwa uchache nikawagutusha wanachama wa CCM dalili za kifo cha chama chao.

Udini ni dalili ya kwanza inayoonekana kulitafuna taifa letu, maana hivi sasa Watanzania tumefikia hatua ya kuuana, kuharibiana mali, kukimbiana kisa itikadi za dini.

Leo hii tumesikia wenzetu wa Geita wameuana kisa ni kugombania uchinjaji wa vitoweo (ng’ombe, mbuzi, kondoo). Serikali ipo lakini haijachukua hatua madhubuti zilizotakiwa.

Miaka yote huko nyuma tulikuwa tukila nyama ya mnyama aliyechinjwa na ndugu zetu bila kupata madhara yoyote, lakini sasa tunauana kwa sababu ya kina fulani wamechinja, tunapotea.

Umoja wetu na upendo vilivyotufanya tuishi pamoja sasa vinatoweka kisa, watawala wetu waliamua kutumia mwamvuli wa dini kuingia madarakani na wakaendelea hadi hivi sasa tunapoona matokeo hasi.

CCM ilipandikiza, ikaulea na sasa taifa linaathirika na udini ilioufanya katika kampeni za mwaka 2005 na 2010.

Bado sijasahau Rais Kikwete alivyoitwa ‘Chaguo la Mungu’ na viongozi wa dini.

Rais wetu leo hii hana ubavu wa kukabiliana na vurugu za kidini zinazotokea mara kwa mara, kisa anahofia chama chake kukosa kura mwaka 2015.
Udini unavyozidi kushamiri ndiyo CCM inavyokaribia kuingia kaburini, muda ndiyo utakaozungumza.

Dalili nyingine ya anguko la CCM ni maandamano ya wakazi wa Mtwara, walioamua kuandamana hivi karibuni kupinga ujenzi wa bomba la gesi kutoka mkoani kwao kwenda Dar es Salaam. Hoja yao ni kutaka rasilimali zao ziwanufaishe wao kwanza.

Dhahabu, almasi, tanzanite, mbuga za wanyama na rasilimali nyingine zipo katika maeneo ambayo wananchi wanaishi maisha ya dhiki sana, huku wale wanaoitwa wawekezaji wakifaidika nazo.

Katika mazingira haya, CCM haitoweza kuishi miaka mingi hata wakibadilisha viongozi wa sekretarieti, kamati kuu mara 100. Hasira za wananchi dhidi ya watawala wanaotumia rasilimali za taifa kwa manufaa yao ndizo zitakazoharakisha kifo cha CCM, makada ni lazima walijue hilo.

Dalili nyingine ya kifo cha CCM ni upandaji wa gharama za maisha ambapo hivi sasa kilo moja ya unga inakaribiana na ya mchele, maharage. Sukari ni bidhaa adimu kwa Watanzania licha ya kuwa na viwanda vya kuzalisha bidhaa hiyo visivyopungua vitano.
Wananchi wanahoji kwanini gharama za maisha zipande kiasi hicho ilihali wanayo bahari, mbuga za wanyama, madini na vivutio mbalimbali vinavyoliingizia taifa mamilioni ya fedha?


Wanajiuliza kwanini watoto wa vigogo wanasoma katika shule za mtakatifu fulani au nje ya nchi badala ya kusoma katika shule za kata zilizojengwa kwa mbwembwe na nguvu kubwa?

CCM imeua elimu yetu, kiwango cha ujinga sasa kimeongezeka zaidi kuliko ilivyokuwa miaka 30 iliyopita. Mitaala ya kufundishia utata mtupu. Bunge linambiwa vingine serikali inatenda vingine.

Wabunge wa CCM wameamua kufa na chama chao, wanaamua kupuuzia hoja za msingi zinazogusa maslahi ya wananchi, kisa zimetolewa na wabunge wa upinzani.

Wananchi hivi sasa wanajua nani anayewatetea, wanajua Bunge linavyojipanga kuilinda CCM, ndiyo maana linafanya mchakato wa kuzuia matangazo ya moja kwa moja (live) yahusuyo vikao vya Bunge, hiki ni kichekesho.

Kamwe CCM haiwezi kunusurika kifo kwa kulitumia Bunge kuzima hoja za wapinzani kwa hila, kifo hakiwezi kuepukika kwa chama kinachopuuzia madai ya msingi ya wapiga kura.

CCM inafikiri mambo ya msingi ni kuandaa mikutano ya hadhara kujibu makombora ya wapinzani, kinajidanganya. Wananchi wanataka kujua kodi wanazokamuliwa na rasilimali zao zinakwenda wapi. Dalili za kuelekea kifo zimo ndani ya CCM, wanachama wake hivi sasa hawapikiki chungu kimoja, makundi yameshamiri kisa, urais 2015. Nafasi hiyo sasa inauzwa.

Asiye na fedha ndani ya CCM hana chake, Kikwete hakuwa na fedha mwaka 2005, lakini alitafuta wenye fedha wakamsaidia kuingia madarakani. Chaguzi zilizofanyika hivi karibuni zimethibitisha jambo hilo. Ni kiongozi gani wa CCM anaweza kutoka mbele ya umma akajinasibu hakupita kwa rushwa? Kama yeye hakutoa, basi timu yake ya kumsaidia ilifanya jambo hilo.
Leo hii CCM inaendekeza ubaguzi, inadiriki kuwaita wenzao ‘wa kutoka eneo fulani’ na wasipewe uongozi wa nchi.

Hayati Mwalimu Julius Nyerere alitukataza tusibaguane, leo hii saratani ya ubaguzi inalimaliza taifa. Kila kukicha tunashuhudia maandamano ya waendesha pikipiki, wananchi kufunga barabara, wanafunzi kugoma kuingia madarasani, madaktari kugoma, vyote hivi vinafanyika kwa sababu utawala wa CCM umeshindwa kuiendesha nchi.

Migomo na maandamano hayo ni dalili ya kifo cha CCM, asiyeamini avute subira. Misri na Tunisia mambo yalianza hivi hivi. Muda ndiyo utawathibitishia watu kuwa kifo cha CCM kimewadia.

No comments:

Post a Comment