To Chat with me click here

Friday, February 8, 2013

VYAMA: KANUNI ZA BUNGE ZIFUMULIWE


Siku chache baada ya Bunge kugubigwa na vurugu, Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kimeazimia kuanzishwa kwa mchakato wa kuboresha kanuni za Bunge ili kuongeza ufanisi, uwajibikaji na uhuru katika kazi za chombo hicho pamoja kuhakikisha  kuwa kunakuwa na mfumo imara wa kuendesha Bunge la mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Katika kikao hicho kilichofanyika jana mjini hapa, ambacho pia kilimshirikisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kiliazimia pia ufumbuzi huo upatikane kwa kuwashirikisha wahusika wote ili kupata mwelekeo wa pamoja.

Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia, alisema kikao hicho kiliazimia changamoto hizo ikiwamo zilizotokea bungeni Jumatatu wiki hii, zikishughulikiwa kwa nia njema na kwa kuzingatia haki, zitakuwa shule ya kuongeza kasi ya uwajibikaji ndani ya Bunge.

Alisema pia waliazimia mamlaka zinazohusika zishughulikie mapema masuala mengine yenye kuibua changamoto nyingine mathalani, uboreshaji wa daftari la wapiga kura, uboreshaji wa mchakato wa kupata Katiba mpya na kuhakikisha kuwa kuna haki na wajibu katika shughuli za vyama vya siasa.

Kikao hicho ambacho kilishirikisha vyama vyote vyenye wabunge, kiliazimia kuandaliwa kwa utaratibu wa kuyahusisha makundi mengine ya wadau mbalimbali kama vile taasisi za dini, asasi za kiraia na mchakato wa mabadiliko ya Katiba unaoendelea uwezeshe kuwa na Katiba Mpya yenye mgawanyo bora wa mamlaka baina ya mihimili ya dola na uhuru katika uendeshaji wa mihimili.

“Tuliazimia mchakato wa mabadiliko ya Katiba unaoendelea uwezeshe kuwa na Katiba mpya yenye mgawanyo bora wa mamlaka baina ya mihimili ya dola na uhuru katika uendeshaji wa mihimili,” alisema Mbatia na kuongeza:

“Tuliazimia kuwapo kwa uvumilivu wa kisiasa baina ya vyama vya siasa na wanachama wake katika kutekeleza majukumu yao mbalimbali kwa ajili ya kudumisha amani, mshikamano, amani na maendeleo endelevu ya Taifa kwa manufaa ya wananchi wote.
 Mbatia alisema maazimio hayo yatawasilishwa katika vyama vya siasa ili yaanze kufanyiwa kazi.

 Vyama vilivyoshiriki katika kikao hicho ni CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi, TLP, UDP, CUF na UPDP.

CHADEMA YAJIANDAA KUWANG’OA SPIKA, NAIBU 
Wakati TCD, ikipendekeza hayo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeomba kumbukumbu rasmi za Bunge kuhusiana na rufaa na miongozo iliyoombwa katika tangu kuanza kwa Bunge la 10 ili kiandae na kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Spika pamoja na Naibu wake.

Hayo yalisemwa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, mjini Dodoma jana.
“Tumeiandikia ofisi ya Spika kuomba watupatie kumbukumbu rasmi za Bunge ili kuandika hoja ya kutokuwa na imani na Spika na Naibu wake,” alisema Mnyika.

Alisema haiwezekani kuandika hoja hiyo bila kupata kumbukumbu hizo rasmi za Bunge.

Miongoni mwa ushahidi wa miongozo na rufaa zilizowasilishwa katika ofisi ya Spika ni ya kiti  kwa kukataa kuliwezesha Bunge kujadili hali ya huduma katika hospitali za umma na jaribio la kutaka kuuawa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka.

Nyingine ni kutoridhishwa na uamuzi wa Naibu Spika wa kukataa mgomo wa walimu na yatokanayo na mgomo huo kujadiliwa bungeni, malalamiko dhidi ya uamuzi wa Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Muhagama, kwa kudai kuwa Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, anao ushahidi kuwa Mbunge wa Iramba Magharibi, Lameck Mwigulu Nchemba (CCM), ni mmoja wa watuhumiwa wa kesi za Epa na kumtaka kuwasilisha ushahidi.

Uamuzi kuhusiana na uthibitisho kuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), juu ya kauli ya uwongo unaodaiwa kutolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, bungeni wakati akijibu maswali Februari 10, mwaka juzi.

Maamuzi mengine yanayodaiwa kutotolewa uamuzi na Spika, ni kauli ya Mbunge wa Meatu (Chadema), Meshack Opulukwa, ambaye alisema bungeni kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo alihongwa gari ili ampatie mwekezaji kitalu cha uwindaji kwenye pori la akiba ili wananchi wahamishwe eneo hilo.

Ushahidi mwingine ambao haujatolewa uamuzi ni wa Mbunge wa Viti Maalum, Magdalena Sakaya (CUF), ambaye alitakiwa na Kiti kuwasilisha uthibitisho wa kauli yake kuwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo, aliingia katika zizi la mfugaji na kutoa mbuzi kisha kumchinja bila ridhaa ya mmliki.

Aidha, Mnyika alisema leo anatarajia kuwasilisha rufaa yake ya kutokuwa na imani na Naibu Spika, Job Ndugai.
 
HOJA YA MBATIA ‘YAFA’
Katika tukio lingine, kamati iliyoundwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuchunguza usahihi  wa mitaala ya elimu ya awali, msingi na sekondari iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, imebaini mitaala iliyowasilishwa ni sahihi.

Kamati hiyo iliunda kuchunguza mara baada ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) kuwasilisha Hoja Binafsi ya udhaifu katika elimu na kudai kuwa serikali haina mitaala ya elimu tangu mwaka 1961. Kamati hiyo ilitangazwa juzi na Naibu Spika, Job Ndugai, na kuwashirikisha wabunge sita  ambao ni  Mbunge wa Viti Maalum Magreth Sitta, (CCM), Mbunge wa Viti Maalum, Benadeta Mushashu,  (CCM),  Mbunge wa Karatu, Israel Natse, (Chadema).

Wengine ni Mbunge wa Kibiti, Abdul Marombwa, (CCM), Mbunge wa Chwaka, Yahya Kassimu Issa (CCM) na Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF).

Akitangaza matokeo ya uchunguzi uliofanywa na kamati hiyo bungeni jana, Spika Makinda alisema ili kujiridhisha kamati hiyo ilipitia nyaraka mbalimbali elimu ya awali, msingi na sekondari.

“Ili kujiridhisha kama mitaala hiyo ni halali, kamati ilipitia nyaraka halisi za mitaala hiyo kutoka serikalini na nyaraka za serikali zilizoidhinisha kutumika kwa mitaala hiyo,” alisema.

Alizitaja nyaraka hizo kuwa ni sheria ya elimu ya mwaka 1975, waraka wa elimu namba 16 wa mwaka 1997, waraka namba tisa wa mwaka 2004, waraka namba 10 wa mwaka 2004, waraka namba mbili wa mwaka 2005, waraka namba moja ya mwaka 2006 na waraka namba mbili wa mwaka 2006. Spika alisema pia Waziri Kawambwa na wataalam mbalimbali walitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizojitokeza ndani ya kikao cha kamati hiyo.

Alisema: “Kutokana na uchambuzi huo, kamati ilibaini kuwa nakala zilizowasilishwa na serikali zilikuwa ni sahihi na ni mitaala rasmi ya elimu ya awali, msingi na sekondari.”

Alisema nakala hizo zitagawiwa kwa wabunge kwa kuwa mwanzo iliwabidi kuzishikilia kwa kuwa hawakuwa na uhakika wa uhalali wake.

Hali hiyo iliwafanya wabunge wa CCM kushangilia kwa kupiga makofi mfululizo huku kambi ya upinzani ikiwa imetulia.

Hata hivyo, baada ya Spika kumaliza kusoma taarifa ya kamati hiyo, wabunge saba walisimama wakiomba mwongozo hata kabla ya kumalizika kwa zoezi la kubadilisha kiti lilokuwa likifanywa kati ya Makinda na Mwenyekiti, ambaye ni Mbunge wa Ilala, Musa Azzan Zungu.

Waliosimama kuomba mwongozo ni Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM); Mbatia, Mbunge wa Kasulu Mjini, Mosses Machali (NCCCR-Mageuzi);  Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi); Mbunge Biharamulo Magharibi, Antony Mbassa (Chadema);  Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keisy (CCM).

“Taratibu za mbunge kusimama zimeainisshwa katika kanuni, na taratibu, mbunge akisimama Spika amuone, sijakaa mmesimama,mamlaka ya kiti hiki hayana tofauti na mamlaka nyingine nje ya Bunge hili, alisema Zungu.”

MBATIA HAJARIDHIKA

Hata hivyo, Zungu alimruhusu Mbatia kutoa mwongozo wake, ambaye alitumia kanuni ya 37 (4) ambayo inasema “baada ya hati kuwasilishwa bungeni na Waziri, Mwanasheria Mkuu  wa Serikali ama mbunge anaweza kutoa hoja Bunge lijadili hati hiyo.”

Mbatia alisema  Oktoba 30,  mwaka jana aliomba kupatiwa mitaala ya elimu na Waziri aliahidi bungeni kuwa atawasilisha mitaala ya mwaka 2005 ambayo ilitokana na mitaala ya mwaka 1997, lakini  mtaala uliopelekwa bungeni ni mtaaala wa mwaka 2005 uliotokana na  mtaala wa mwaka 1998.

Alisema hivyo mtaala wa mwaka 2005 uliotokana na mtaala wa mwaka 1997 ambao haujawasilishwa mezani (bungeni).

“Suala la elimu ya sekondari ni suala la Muungano, mtaala uliowasilishwa mezani wa elimu ya sekondari ni wa Tanzania Bara na si wa Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania,” alisema Mbatia. Alisema pia mitaala uliowasilishwa mezani hauna namba ya uthibitisho wa kiwango cha kimataifa kama ilivyo katika muktasari.

Pia alisema miktasari yote inaonyesha kuwa muidhinishaji wa mitaala ni Kamishna wa Elimu kwa mujibu wa sheria ya elimu ya mwaka 1975, lakini yote inaonyesha muidhinishaji ni ofisa mkuu kiongozi wa elimu.

Aliomba kutoa hoja bunge lijadili mitaala iliyowasilishwa, lakini Zungu alisema amepokea mwongozo huo na kwamba angeutolea uamuzi baadaye.

Hata hivyo, baada ya muda Keisy aliomba mwongozo kwa Spika, na kusema Mbatia alipokuwa akizungumza katika mjadala wa hoja yake binafsi, alisema kama Waziri Dk. Kawambwa atawasilisha mitaala sahihi yuko tayari kujiuzulu nafasi yake.

Kessy alimnukuu Mbatia akisema atajiuzulu kwa heshima ya chama chake na kwa manufaa ya wananchi na kwamba hata kama akijiuzulu, serikali haitakuwa imepoteza kitu chochote.
Alisema kwa kuwa Waziri ameshawasilisha mitaala hiyo, basi Mbatia ajiuzulu ili kulinda heshima yake.

Hata hivyo, Zungu alimtaka kukaa na kisha kuendelea na shughuli nyingine za Bunge.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge, Mbatia alisema hawezi kujiuzulu kwa kuwa mitaala iliyowasilishwa bungeni siyo sahihi. ”Siwezi kujiuzulu kwa sababu serikali imeshindwa kuleta mitaala halali,” alisema.

No comments:

Post a Comment