AHADI
za ujenzi wa barabara za lami zilizopata kutolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati
akiomba kura mwaka 2010, zimezua balaa na kuibua mzozo bungeni.
Hali
hiyo ilitokana na swali la Mbunge wa Buhambwe, Felix Mkosamali (NCCR- Mageuzi),
kuhoji utekelezaji wa ahadi ya Rais Kikwete ya kujenga barabara ya
Nyakanazi-Kibondo-Kigoma katika kiwango cha lami.
Pia
alihoji ahadi ya Rais Kikwete ya ujenzi wa barabara ya Kibondo Mjini yenye
urefu wa kilomita 1.5 na ujenzi wa barabara ya kimataifa ya kutoka Kibondo
–Mabamba mpaka wa Burundi.
Akijibu
swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge alisema serikali bado iko
mbioni kutekeleza ahadi hizo kutegemea na upatikanaji wa fedha. Alisema
ahadi za rais zitatekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha kwani mwisho wa
ahadi zake ni mwaka 2015.
Kutokana
na majibu hayo, Mkosamali aliuliza swali la nyongeza na kutumia maneno
yaliyotafsiriwa kama ni kashfa kwa Rais Kikwete. “Mhesmiwa
Naibu Spika, sikubaliani na majibu mepesi ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Hivi
unataka kusema ahadi za Rais Kikwete kujenga barabara ya Kibondo ilikuwa ya
uongo? Ina maana alisema uongo ili kupata sifa ya kuchaguliwa kuwa rais?”
Swali
hilo la nyongeza ambalo hata hivyo lilijibiwa vizuri na Naibu Waziri wa Ujenzi,
lilimkera Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi ambaye alisimama na kuomba mwongozo wa spika akipinga lugha iliyotumiwa
na Mkosamali dhidi ya Rais Kikwete.
“Mheshimiwa
Naibu Spika, mbunge aliyeuliza swali la msingi kuhusu ahadi za rais, wakati
akiuliza swali la nyongeza, alitumia maneno makali dhidi ya rais kinyume cha
kanuni za Bunge. “Anasema
rais alisema uongo au alisema uongo ili achaguliwe, sio maneno ya kistaarabu
kutumika hasa kwa rais.
“Mheshimiwa
Naibu Spika, kanuni ya 61 (2) inasema mbunge hatatumia kumdhihaki rais au
kulishawishi Bunge kuamua jambo fulani dhidi ya rais.
“Nimesimama
sio kutaka aombe radhi, bali kuwakumbusha vijana wawe makini na matumizi ya
lugha, hasa lugha ya kuudhi. Mwongozo wangu ni kutaka uwakumbushe wabunge
matumizi mazuri ya lugha, ni hilo tu,” alisema na kuketi.
Mbunge
wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) ambaye ni mnadhimu kambi ya
upinzani bungeni, kwanza alimtaka Waziri Lukuvi afute kauli yake kwamba kuna
vijana kwa madai kuwa ndani ya Bunge hakuna vijana.
”Pili,
Waziri Lukuvi amemwelewa vibaya mbunge maana hajasema rais muongo. Alitaka
kujua kama ahadi ya rais ni ya uongo. Na tatu mbunge hakutaka kushawishi Bunge
kuchukua hatua dhidi ya rais,” alisema Lissu.
David
Kafulila, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), naye alisimama na kuongeza
kuwa waziri amepotosha umma na huo ni uchochezi. Mkosamali
naye alisimama na kusema kuwa hajamtukana rais bali alitaka kujua kama ahadi
hiyo ni ya uongo au la.
Akitoa
mwongozo wake, Naibu Spika aliwataka wabunge kutumia lugha ya kistaarabu. Mbali
ya swali la Mkosamali, wabunge wengine waliohoji ahadi ya ujenzi wa barabara
katika maeneo yao ni Ester Bulaya (Viti Maalumu), Paul Rwanji (Manyoni
Magharibi), wote CCM na Said Arfi wa Mpanda Kati (CHADEMA), ambao nao waliohoji
ahadi za Rais Kikwete za ujenzi wa barabara katika maeneo yao.
No comments:
Post a Comment