To Chat with me click here

Friday, February 8, 2013

TENDWA AKWAA KISIKI CHADEMA


Msajili wa Vyama vya Siasa Ndg. John Tendwa

Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, amekwaa kisiki kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya chama hicho kumwandikia barua kwamba hakiko tayari kutoa maoni kuhusu vurugu zilizotokea hivi karibuni mjini Dodoma kwa sababu hana mamlaka ya kushughulikia makosa ya kijinai.

Tamko hilo la Chadema limekuja siku moja baada ya Tendwa kueleza kuwa ofisi yake itachukua suala hili kwa kuvihusisha vyama husika ili ipate ukweli na undani wake na ichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Jumapili iliyopita, viongozi na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chadema, walipigana hadharani wakigombea uwanja wa kufanyia mikutano mjini Dodoma. CCM walikuwa wanataka kufanya mkutano wa maadhimisho ya miaka 36 ya kuzaliwa kwake.

Wakati vurugu hizo zinatokea, walikuwapo wabunge wawili wa CCM.

Kufuatia kauli  ya Tendwa, Chadema kilimwandikia barua Tendwa, kuwa hakiko tayari kutoa maoni kuhusu vurugu hizo kwa kuwa ni kosa la kijinai.

Katika barua hiyo yenye kumbukumbu Na. C/ADM/MSJ/04/04 iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Willibroad Slaa, imeeleza kuwa suala la vurugu zilizotokea Dodoma, ni la kijinai, hivyo Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka ya kushughulikia makosa ya namna hiyo.

Barua hiyo ya Chadema iliyoandikwa Februari 6, mwaka huu na kusainiwa na Idara ya Sheria ya chama hicho, kwa niaba ya Katibu Mkuu wake, ni majibu ya barua ya msajili, aliyomwandikia Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Slaa, akimtaka atoe maoni yake juu ya vurugu zilizotokea Dodoma.

“Nimeagizwa na Katibu Mkuu nikujulishe kuwa hatatoa maoni kuhusu tukio lililotokea Dodoma siku ya tarehe 03/02/2013 kwa kuwa suala hilo ni la jinai na viongozi wa Chadema Mkoa wa Dodoma wameshafungua mashitaka polisi, kutokana na suala hilo kuwa la jinai, Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka ya kulishughulikia,” ilisema sehemu ya barua hiyo ya Chadema ambayo NIPASHE imeona nakala yake.

Februari 5, mwaka huu, Tendwa alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Chadema yenye kumbukumbu Na. AB.115/123/01A/45, ikimtaka ashiriki kutoa maoni kuhusiana na vurugu hizo.

Tendwa alipotafutwa  jana kuhusiana na barua aliyoandikiwa na Chadema, hakupatikana kutokana na simu yake ya kiganjani kufungwa.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari juzi, Tendwa alisema amesikitishwa na vurugu zilizotokea katika shughuri za kisiasa mkoani Dodoma Jumapili iliyopita kati ya CCM na Chadema na kusema kuwa ni ukiukwaji wa masharti ya usajili wa vyama vya siasa.

Alisema kifungu namba 9(2)(c) cha sheria ya vyama vya kisiasa ya mwaka 1992 kikisomwa pamoja na kifungu 5 (b)(i) kama ilivyorekebishwa mwaka 2009 kinakataza vurugu, fujo, matumizi ya nguvu na uvunjifu wa amani wa aina yoyote na kuwa ni kosa la jinai linalopaswa kufanyiwa kazi na mamlaka.

Tendwa alisema matukio kama hayo yanatengeneza taswira mbaya ya siasa nchini na kushusha heshima na imani ya wananchi kwa vyama vya siasa.

Alisema ofisi ya msajili inachukua suala hili kwa kuvihusisha vyama husika ili ipate ukweli na undani wake na iweze kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Alisema ofisi yake inavikumbusha na kuviasa vyama vya siasa kuheshimu sheria za nchi, sheria ya vyama vya siasa na maadili ya vyama vya siasa.

RPC DODOMA ANENA
Wakati hayo yakiendelea, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema jeshi hilo limepeleka majalada mawili kwa Mwanasheria wa Serikali kuhusiana na vurugu hizo ili wahusika wachukuliwe hatua.

Misime ambaye hata hivyo, hakutaka kutaja majina ya watu ambao majalada yao yamepelekwa kwa mwanasheria huyo, badala yake alieleza kuwa yanahusu kufanya vurugu kwenye sherehe na jingine la shambulio.

“Tumepeleka majalada mawili jana (juzi) kwa Mwanasheria wa Serikali, moja la kufanya fujo kwenye sherehe na jingine la shambulio, tumeyapeleka baada ya kuwakamata wahusika na kuwahoji,” alisema Kamanda Misime.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment