SHEREHE
za miaka 36 za kuzaliwa kwa CCM jana ziliingia dosari, baada ya kuibuka vurugu
kubwa kati ya wafuasi wa chama hicho na Chadema mkoani Dodoma wakati wakigombea
eneo na mti wa kutundika bendera za vyama vyao.
Vurugu
hizo zilizotulizwa na Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU), zilitokea jana mchana
katika uwanja huo uliopo karibu na Baa ya Mwanga, baada ya CCM kung’oa bendera
ya Chadema iliyokuwepo uwanjani hapo, ili waweke bendera zao kwa ajili ya
mkutano ambao ulikuwa sehemu ya maadhimisho hayo.
Vurugu
zilizuka baada ya wafuasi wa Chadema kuwataka wenzao wa CCM waendelee na
mkutano katika eneo hilo kwa sharti la kurejeshwa kwa bendera iliyong’olewa.
Wafuasi wa vyama hivyo wakiwamo wabunge wa CCM walionekana wakivutana
kunyang’anyana mti wa bendera.
“Baada
ya CCM kugoma, Chadema walijaribu kurudisha bendera hiyo kwa nguvu, jambo
ambalo lilifanya wafuasi wa CCM waanze kuokota mawe na kuwarushia wapinzani wao
hao, huku Chadema nao walianza kujibu mapigo,” alisema mmoja wa mashuhuda wa
tukio hilo.
Baadhi
ya wabunge wa CCM walioshiriki katika vurugu hizo na majimbo yao kwenye mabano
ni Ismail Aden Rage (Tabora Mjini), Nyambari Nyangwine (Tarime), Seleman Jafo
(Kisarawe), Said Mtanda (Mchinga) na Mary Chatanda (Viti Maalumu).
Baadhi
ya wafuasi wa CCM walionekana wakibeba mawe na kuwapiga wenzao wa Chadema na
kusababisha tafrani kubwa katika eneo hilo la mkutano.
Katibu
wa Chadema Wilaya ya Dodoma Mjini, Jellah Mambo alisema kuwa tukio hilo
limetokana na wafuasi wa CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwa ikipepea eneo
la Mwanga Baa kulikofanyika sherehe za chama chao (CCM).
“Kwa
nini sisi (Chadema) tuzuiwe mikutano yetu wakati wenzetu wanafanya? Huku si
kutenda haki....Tulikuwa na mikutano ya kuimarisha chama katika kata kuanzia
Ijumaa, Jumamosi na Jumapili, lakini tumezuiwa na tukaheshimu mamlaka,” alisema
katibu huyo.
Pia
tulikuwa tufanye mkutano na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, lakini
tukazuiwa na tuliheshimu amri hiyo, alisema. Mambo
alisema katika vurugu hizo wafuasi wawili wa Chadema; Idd Kizota na Anord Swai
waliumizwa na kushonwa nyuzi saba usoni.
Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Ezekiel Mpuya alisema hana taarifa za
majeruhi hao.
“Ni
vigumu kujua, unless (isipokuwa) wafike hospitalini wakisindikizwa na kundi la
wafuasi wenzao waliokuwa kwenye sare. Kama walikuja kama wagonjwa wengine sio
rahisi sana kwangu kujua,” alisema Dk Mpuya.
Kumi mbaroni
Vurugu
hizo zilizosababisha watu wawili kuumizwa vibaya, zililazimisha Jeshi la Polisi
kuwatia mbaroni watu kumi wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Chadema. Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alikiri kutokea vurugu hizo, lakini
akasema bado anafanyia kazi suala hilo.
Kamanda
Misime alikiri Serikali mkoani Dodoma kuzuia mikutano ya kisiasa wakati wa
Bunge, lakini akasema kwa CCM ni tofauti kwa kuwa hizo ni sherehe zao za
kuzaliwa kwa chama.
“Ninasoma
hapa magazeti yenu, mmeandika wenyewe maadhimisho ya miaka 36. Sasa hawa
wanaadhimisha hiyo miaka 36 na siyo mkutano wa kisiasa...Tulichokataza ni
maandamano, misafara ya pikipiki na kufanya mikutano ya siasa,” alisema Misime.
Akihutubia
katika mkutano huo baada ya hali kutulia mgeni rasmi, Mbunge wa Jimbo la
Tarime, Nyangwine aliwakandia wapinzani na kusema kuwa wanachokifanya ni
kuendeleza vurugu nchini na hawana sera ya maendeleo.
“Hivi
jamani, hii leo hawa jamaa watasema nini? Kama suala la barabara, leo hii
unaweza kutoka Mtwara hadi Mwanza kwa baiskeli, kama maji, michakato
inafanyika, kama umeme ndiyo usiseme, hivi wanataka nini?
“Hawa
jamaa wamezoea kufanya vurugu...Si mmeona wenyewe hapa, hawana lolote zaidi ya
kufikiria vuru, wananchi msikubali kuhadaiwa,”alisema.
No comments:
Post a Comment