To Chat with me click here

Thursday, February 7, 2013

HALIMA MDEE ATIMULIWA

Mbunge wa Kawe Chadema - Halima Mdee
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, ametimuliwa kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kwa madai kwamba ana maslahi ya upande mmoja katika mgogoro uliotokea bungeni juzi wakati Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.

Taarifa za uhakika zilizopatikana bungeni jana zilieleza kwamba Mdee ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo, alizuiwa kuhudhuria kikao kilichojadili sakata hilo kwa kuwa alikuwa akishabikia vurugu bungeni.

Taarifa zaidi zimedai kwamba kumeibuka mvutano kuhusu kanuni iliyotumika kumruhusu Waziri Maghembe kutumia nusu saa kujibu hoja ya Mnyika wakati alipaswa kutumia dakika 15 kama wachangiaji wengine.

Jana Mdee alithibitisha kuwa alizuiwa kuhudhuria kikao cha kamati hiyo kwa maelezo kuwa ana maslahi na upande wa kambi ya upinzani juu ya suala la mgogoro wa hoja ya Mnyika ambayo ilipokwa na serikali juzi na kuiua.

Mdee alielezwa kuwa alikuwa bungeni siku hiyo na alishiriki katika kadhia iliyosababisha Bunge kuahirishwa kabla ya muda wake baada ya wabunge wote wa Chadema na NCCR-Mageuzi kusimama kwa muda mrefu na kuzuia shughuli za Bunge kuelendelea wakipinga kitendo cha kuvunjwa kwa kanuni za Bunge kwa kuipa nafasi serikali uondoa hoja binafsi ya Mnyika juu ya upatikanaji wa maji safi na uondoaji wa maji taka katika jiji la Dar es Salaam.

Kamati ya Maadili imepewa jukumu la kuchunguza chanzo cha vurugu hizo kwa kuwahoji wabunge waliohusika na kadhia ya Jumatatu jioni ili kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa dhidi yao.

WAJUMBE WA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE

Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi (Mwenyekiti); Christopher Ole Sendeka; Rashid Ali Abdallah, Dk. Maua Daftari; John Chiligati; Dk. Christina Ishengoma; Riziki Omar Juma; David Kafulila; Vita Kawawa; Philemon Ndesamburo; Augustino Masele, Said Arfi; Augustine Mrema; Cynthia Ngoye; Halima Mdee na Gosbert Blandes.

Hata hivyo, Chadema imewaelekeza wabunge wake wote kutoitikia wito wa kamati hiyo hadi hapo Spika wa Bunge, Anne Makinda, atakapotoa uamuzi wa rufaa 10 ambazo wabunge hao wamekata kwake, lakini amezikalia tangu mwaka 2011.

Pia Chadema kimetishia kuwasilisha hoja ya kumng'oa madarakani Spika Makinda na Naibu Spika, Job Ndugai, kwa madai ya kukiuka kanuni za Bunge kwa kutotenda haki kwa pande zote, hasa kambi ya upinzani, kwa maana hiyo wamepoteza sifa za kuongoza muhimili huo.

WABUNGE HAWAJAHOJIWA
Wakati huo huo, Kamati hiyo bado haijawahoji wabunge wanaodaiwa kufanya fujo ndani ya Bunge.

Katika hatua nyingine, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu, amesema kitendo cha Spika wa Bunge, Anne Makinda, kumtuhumu kuwa ni mropokaji namba moja bungeni ni kwa sababu ya chuki na upendeleo dhidi ya wabunge wa upinzani.

Lissu jana alisema siyo kweli kwamba amekuwa ni mropokaji bungeni kama Spika Makinda alivyomtuhumu na kwamba amekuwa akifuata kanuni zinazotakiwa kwa kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuisimamia na kuishauri serikali.

Alisema yeye ni miongoni mwa wabunge wachache ambao wanazifahamu kanuni za Bunge, Katiba ya nchi na sheria mbalimbali.

“Kuniita mropokaji ni kunifananisha na baadhi ya wabunge wa CCM ambao hawajui sheria wala wajibu wa Bunge…wanadhani kazi ya mbunge ni kuikingia kifua serikali na kuitetea, wamesahau kwamba wajibu wao ni kuishauri na kusimamia, " alisema.

Lissu alisema kamwe hawezi kuogopa kuisimamia serikali kama Katiba inavyomtaka na hawezi kuitetea pale inaposhindwa kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

No comments:

Post a Comment