To Chat with me click here

Thursday, February 7, 2013

RUSHWA MAHAKAMANI YAMTISHA JK


Rais Jakaya Mrisho Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete amesema mwenendo wa sasa wa utendaji kazi wa mahakama za hapa nchini unatiliwa shaka na wananchi, kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa idara hiyo.
Amesema malalamiko mengi ya wananchi yenye mwelekeo unaoonyesha haki haiwezi kupatikana mahakamani isipokuwa kwa kununuliwa na wenye fedha, ni ishara kuwa jamii imekosa imani na mhimili huo wa dola.

Rais Kikwete alisema hayo jana, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, yaliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu, jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo, ambayo pia yalihudhuriwa na Jaji Mkuu, Othman Chande, pamoja na wanataaluma wengine wa sheria, kauli mbiu yake ya mwaka huu ni utawala wa sheria, umuhimu na uimarishaji wake hapa nchini.

Rais Kikwete aliwataka watumishi wa idara hiyo kushirikiana kuondoa dhana iliyojengeka kwa wananchi kuwa haki inapatikana kwa kununuliwa na kusisitiza kuwa dhana hiyo ni doa kubwa kwa mahakama.

“Ni doa kubwa kusikia haki inatolewa kwa wenye fedha mahakamani, ikiwezekana shirikisheni jamii ili kuondoa doa hilo, lakini bila kukiuka miiko ya majaji na mahakimu.

“Watu wanapenda haki itendeke, mashauri yamalizike kwa wakati na wanachukizwa na mashauri kupigwa kalenda mara kwa mara. Na lawama zinazotolewa si kwa upande wa mahakama peke yake, bali hata ucheleweshaji wa kesi husababishwa na upelelezi kuchelewa kukamilika, mawakili na wadau wengine. Hapo muone kuwa ipo haja ya kukaa chini kuangalia jinsi ya kupunguza malalamiko hayo,” alisema Rais Kikwete.

Akizungumzia bajeti finyu inayotolewa na serikali kwa mahakama, alisema tatizo hilo lipo kila katika idara na wizara zote za serikali na linasababishwa na mapato madogo ya serikali.

Alisema maombi ya fedha kwa ujumla yanayowasilishwa serikalini ni trilioni 19 na bilioni 3, mapato ya Serikali kwa ujumla wake ni trilioni 15, jambo linaloonyesha wazi kuwa serikali haiwezi kutosheleza mahitaji yote.

Aliahidi kuongeza fungu la bajeti la mahakama katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha na kwamba kiasi kitakachoombwa na idara hiyo kitapelekwa kwa wakati.

Naye Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Francis Stolla, akizungumza katika maadhimisho hayo, alisema Bunge Tanzania linakabiliwa na changamoto ya umakini linapoketi kutunga sheria.

Alisema Bunge linapaswa kuichukua changamoto hiyo kwa sababu kuna tatizo la sheria kukinzana, jambo ambalo linasababisha usumbufu kwa baadhi ya wananchi na wakati mwingine haki kutotendeka.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu Chande, alikemea tabia ya wananchi kuchukua sheria mkononi kwa kuchoma moto wenzao na kuharibu mali za wanaotuhumiwa kwa makosa ambayo mengine huthibitika baadaye kuwa hawakufanya.

No comments:

Post a Comment