Mkutano wa 10 wa Bunge unaendelea leo
mjini Dodoma baada ya mapumziko ya mwisho wa wiki na leo itakuwa zamu ya Mbunge
wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, kuwasilisha hoja binafsi kuhusu hatua za
uboreshaji wa upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika
Jiji la Dar es Salaam.
Hata
hivyo, taarifa kutoka ndani ya vikao vya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
zinaeleza kwamba hoja ya Mnyika itakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa
wabunge hao kwa madai kwamba siyo Jiji la Dar es Salaam pekee lenye tatizo la
maji.
Taarifa
zaidi zinaeleza kwamba wabunge hao wamejipanga kuizuia hoja hiyo kama
walivyofanya hoja ya Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, ambayo
ilikuwa ikizungumzia udhaifu ulipo katika sekta ya elimu hasa kutokuwapo kwa
mitaala rasmi ya shule za msingi na sekondari.
Wabunge
hao wamejipanga kuilazimisha serikali iangalie kwanza tatizo la maji vijijini
badala ya Jiji la Dar es Salaam kama Mnyika anavyopendekeza.
Akizungumza
na NIPASHE jana, Mnyika alisema Ijumaa aliwasilisha kwa Katibu wa Bunge
mapendekezo ya kuboresha na kupanua wigo wa hoja yake pamoja na hatua za haraka
za kuboresha upatikanaji wa maji jijini Dar es Salaam.
Alisema
katika mapendekezo hayo, hoja yake imejielekeza katika kuboresha
utekelezaji wa miradi ya maji nchi nzima kwa kuingiza masuala muhimu kuhusu
Programu ya Maji Safi na Mazingira Vijijini (RWSSP) maarufu kama mradi wa
vijiji kumi ambao unatekelezwa katika Halmashauri za Dar es Salaam na wilaya
zote nchini.
“Nimeeleza
kuwa Programu ya Maji Safi na Mazingira Vijijini ikiwamo katika Manispaa za
Jiji la Dar es Salaam ilipaswa kutekelezwa kuanzia mwaka 2005/2006 na
kukamilika mwaka 2010/2011 kwa kugharimu dola za Marekani milioni 292 (zaidi ya
Sh. bilioni 438). Hata hivyo, tathmini ya miaka miwili na nusu ya
utekelezaji imebainisha kasoro nyingi katika utekelezaji,” alisema.
Alisema:
“Nitawasilisha bungeni hatua zipi za haraka ambazo napendekeza zichukuliwe
ikiwamo kuhusu ufisadi katika sekta ya maji kwenye Jiji la Dar es Salaam na
nchini kwa ujumla.”
Alisema
mabadiliko aliyofanya yanalenga pamoja na mambo mengine, kuifanya iguse matukio
ya karibuni kuhusu tatizo la maji nchini.
Kabla
ya Mnyika kuwasilisha hoja yake, wabunge wataendelea na mjadala wa hoja ya
Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Hamis Kigwangalla, ya kuitaka serikali ianzishe
mfuko maalum wa kukuza ajira kwa vijana kwa kuanzisha mfuko wa mikopo wa vyama
vinavyowekeza katika kilimo na viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja na
kilimo.
Hoja
ya Kigwangalla iliwasilishwa bungeni Ijumaa iliyopita na kujadiliwa na baadhi
ya wabunge, lakini leo wengine zaidi watapata nafasi ya kuchangia kabla ya
mbunge huyo kupewa nafasi ya kuhitimisha.
Hoja
ya Mnyika ambayo itafuatiwa na ya Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua
Nassari, ambaye kesho atawasilisha hoja binafsi kuhusu mwenendo wa Baraza la
Mitihani la Taifa unavyoathiri elimu nchini.
Mbali
ya hoja hizo, Bunge pia litajadili maazimio ya mikataba mbalimbali ya Kimataifa
pamoja na miswada ya sheria itakayowasilishwa na serikali.
Hoja
ya Mnyika huenda ikageuzwa kama ilivyofanywa na Mbatia baada ya wabunge wa CCM
kutoiunga mkono. Hatari ya hoja kutoungwa mkono na wabunge wa CCM ni kura za
ndiyo na siyo ambazo zinakwamisha hoja hata kama zina nguvu.
Katika
hoja yake, Mbatia aliliomba Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza udhaifu uliopo
kwenye sekta ya elimu hasa kutokuwepo kwa mitaala rasmi.
Hoja
hiyo ilipingwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa,
ambaye alipinga kamati akieleza kwamba tayari serikali imechukua hatua nyingi
za kuitekeleza elimu kwa kujenga madarasa mengi na idadi ya wanafunzi
wanaojiunga elimu ya msingi na sekondari imekuwa ikiongezeka kila mwaka.
Waziri
Kawambwa aliahidi kwamba atawasilisha miswada hiyo bungeni Februari 6, kabla
Mkutano huu haujamalizika.
Baadhi
ya wabunge waliochangia hoja ya Dk. Kigwangalla wameonyesha wasiwasi wa
zitakakopatikana fedha za kuweka kwenye mfuko wa kukopesha vijana na badala
yake wamependekeza mfumo mzima wa elimu uboreshwe ili nchi izalishe wahitimu
wanaoweza kujiajiri na kushindana kwenye soko la ajira.
Kwa
mujibu wa ratiba, Mkutano wa Kumi wa Bunge unatarajiwa kuahirishwa Februari 8,
mwaka huu.
No comments:
Post a Comment