To Chat with me click here
Showing posts with label MACHAFUKO. Show all posts
Showing posts with label MACHAFUKO. Show all posts

Tuesday, September 17, 2013

BREAKING NEWS!!!! SEKONDARI YA ILBORU VIPAJI MAALUM YAFUNGWA KWA MUDA USIOJULIKANA KWA HOFU YA KUCHOMWA MOTO...

SHULE ya Sekondari ya Ilboru, jijini Arusha imefungwa kwa muda usiojulikana kuanzia leo baada ya kuwepo hofu ya kuchomwa moto.

Uchunguzi wa madai ya shule hiyo kuchomwa moto, unaendelea kufanywa huku ikielezwa kwamba wanafunzi wanne wanahojiwa na polisi wilayani Arumeru wasaidie kubaini ukweli juu ya madai hayo.

Wanafunzi wengine 10 inadaiwa wamepewa barua za kusimamishwa shule kwa siku kadhaa wakihusishwa na suala hilo.

Tangazo la kufunga shule hiyo lilitolewa ghafla leo asubuhi na Mkuu wa Shule, Julius Shila baada ya kushauriana na bodi yake, huku polisi wa kawaida wakifanya doria kudhibiti vurugu zozote ambazo zingeweza kutokea.

Ingawa Mkuu wa Shule, Shila hakutaka kuzungumzia suala hilo, Kaimu Ofisa Elimu wa Mkoa, Sifael Mollel, alisema uchunguzi wa madai hayo unaendelea katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wamepewa likizo.

Alisema kuwepo kwa hofu hiyo na wasiwasi wa kuzuka vurugu ndiko kulikosababisha shule ifungwe kwa muda licha ya kwamba walikuwa hawajamaliza mitihani.

“Uongozi umeamua wanafunzi warudishwe nyumbani kutokana na hofu ya kuchomwa moto shule, wanafunzi walikuwa wakifanya mitihani kabla ya kuanza likizo fupi lakini uwepo tishio hilo na kuzuka kwa vurugu, ilionekana ni vema ikafungwa,” amesema.

Alisema kwa kawaida likizo fupi ni ya siku 10 lakini kwa tukio hili wanafunzi hao wamepewa maelekezo ya kwenda kuonana na wakuu wa wilaya zao kwa udahili kabla ya kurejea tena shuleni.

Akizungumzia vitisho vya moto, alisema wanafunzi hao waliwasilisha barua ofisini kwake wakitoa madai kuwa baadhi ya walimu walikuwa wanataka kuchoma moto shule hiyo.

Alisema polisi walienda kufanya uchunguzi Ijumaa ambapo walinusa harufu ya petroli iliyokuwa imemwagwa jirani na bweni.

Hata hivyo Kaimu Ofisa Elimu huyo hakutawataja wanafunzi ambao wanahojiwa na polisi wala wanafunzi 10 ambao wamesimamishwa kwa siku 21.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Liberatus Sabas, alikiri polisi kuwepo shuleni hapo wakati tangazo la kufungwa shule likitolewa akasema hiyo ilikuwa ni kwa sababu ya kuimarisha usalama.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, wanafunzi wote watatakiwa kurejea shuleni hapo baada ya kudahiliwa na wakuu wa wilaya zao.

Thursday, August 29, 2013

MWANAJESHI WA UN AUAWA NA WAASI (M23) DRC



Umoja wa Mataifa umesema kuwa mwanajeshi wake mmoja wa kutunza amani ameuawa na wengine watatu kujeruhiwa kufuatia mapigano makali kati ya na wapiganaji wa waasi Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wanajeshi wa serikali ya Congo
Msemaji wa Umoja wa Mataifa mjini New York, Farhan Haq, hata hivyo hajatangaza uraia wa wanajeshi waliouawa au kujeruhiwa.

Wanajeshi hao wa Umoja wa Mataifa walitumia ndege za helicopta kuwasukuma nyuma wapiganaji wa M23 karibu na mji wa Goma, ambao ndio mji mkubwa zaidi katika eneo hilo la Mashariki. Watu themanini waliuawa kwenye mapigano hayo wiki iliyopita.
 
Mwaka wa 2012, waasi wa M23 waliuteka mji huo kwa muda kabla ya kuondoka kufuatia shinikizo kutoka kwa jamii ya kimataifa. Umoja wa Mataifa Umetuma kikosi maalum katika eneo hilo lenya utajiri mkubwa wa madini kukabiliana na waasi hao.
 
Wanajeshi hao wa Umoja wa Mataifa MONUSCO, wanapambana na wapiganaji hao wa waasi kwa ushirikiano na wanajeshi wa serikali. Jeshi hilo la Monusco limelazimika kufanya mashambulio ya anga na ardhini ili kuzuia waasi hao wa M23 kukaribia Goma na ripoti zinasema mapigano makali yanaendelea katika maeneo ya milima ya Kibati, takriban kilomita kumi na tano Kaskazini mwa Goma.
 
Watu wapatao laki mbili wanasemekana kuishi katika eneo hilo la Kibati. Wapiganaji wa M23 wamesema kuwa wanajeshi wa Congo na wenzao wa Umoja wa Mataifa walifanya mashambulio ya anga na ardhini katika maeneo wanayoyadhibiti, Kaskazini mwa Goma.
 
Daktari mmoja mjini Goma, Isaac Warwanamiza, ameliambia shirika la habari la AP kuwa aliona miili ya watu themanini na wawili, ishirini na tatu zikiwa za wanajeshi wa serikali. Umoja wa Mataifa una zaidi wanajeshi elfu kumi na nane nchini Congo.

KUMBE! JEURI, KIBURI CHA KAGAME VINATOKA KWA WAZITO!



Paul Kagame; Rais wa Rwanda
Aliyekuwa Rais wa Marekani Bill Clinton, hivi majuzi amemtetea Kagame kutokana na tuhuma zinazomkabili za kuwasaidia waasi wa M23 nchini DRC.

Kwa muda wa miezi takriban minne kumekuwa na maneno ya kejeli kutoka kwa Serikali ya Rwanda na kwa hakika maneno hayo yanatoka mdomoni mwa Rais Paul Kagame na maofisa wa ngazi za juu katika Serikali yake.

Kagame amekuwa mbogo baada ya Rais Jakaya Kikwete kumshauri afanye mazungumzo na wapiganaji wa Kihutu waliokimbilia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) baada ya kutuhumiwa kufanya mauaji ya kimbari nchini mwake mwaka 1994.

Inakadiriwa kuwa Watutsi na Wahutu 800,000 wenye msimamo wa wastani waliuawa wakati huo, ingawa takwimu hizo zina utata, kwani wako wanaodai kuwa nchi hiyo wakati huo ilikuwa na idadi ndogo ya watu ambao idadi hiyo inasemekana ndio waliouawa.

Pia, wapo wale ambao wanaweza kushangaa kwa nini Kagame amekuwa hivyo na kuikosea heshima Tanzania, nchi ambayo imekuwa mstari wa mbele kupokea wakimbizi wake toka miaka ya 1960 na kwa nini Rais Kikwete alitoa ushauri huo.

Kagame hakupendezwa na ukweli huo kwani kila mara amekuwa akikataa kuwa hana mkono katika mapigano yanayoendeshwa na vikundi vya msituni vinavyoanzishwa nchini DRC kila inapotokea hali kutulia.

Kikwete amekuwa akijua jambo hili kwa muda mrefu kwani amekuwa Waziri wa Mambo  ya Nje kwa kipindi cha miaka kumi na amekuwa akihudhuria mikutano ya kutafuta amani ya DRC bila mafanikio kwa sababu kila kikundi kinapoingizwa katika jeshi la DRC na kudai kuwa kimemaliza vita kinazuka kikundi kingine ambacho nacho kinaanzisha mapambano dhidi ya serikali.

Kofi Annan, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN) alikuwa mkuu wa shughuli za kijeshi za umoja huo kabla hajapanda cheo na kuwa katibu mkuu wa umoja huo, alipotembelea Rwanda baada ya kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe, msafara wake ulirushiwa nyanya.

 Hiyo ilikuwa ni kama kumpa ujumbe kuwa hakuna alichofanya wakati  ule Watutsi walipouawa na Wahutu mwaka 1994.

Masikini! Annan angefanya nini wakati alipokuwa akiyaomba mataifa makubwa kuingilia kati ili kusitisha mauaji kila moja lilikuwa likiangalia maslahi yake na ulikuwepo mpango wa uchelewashaji wa makusudi.

Baadaye Annan alipokuwa akigombea Ukatibu Mkuu wa UN ni Rwanda pekee katika nchi za Afrika ndiyo iliyopinga na hata alipokuwa akiomba kuongezewa muda ni nchi hiyo iliyokuwa kinara wa kumpinga wakati ukweli ni kuwa mambo yote yaliyokuwa yakifanyika wakati huo Kagame alikuwa akiyajua.

Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Rwanda, Meja Jenerali Kayumba Nyamwasa, alinukuliwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC)  akiwa uhamishoni Afrika Kusini akithibitisha kuwa vikundi vyote vimekuwa vikianzishwa na Kagame kwa nia ya kuhakikisha kuwa Wahutu na jeshi la zamani la nchi hiyo ambalo kwa sehemu kubwa linaundwa na waliokuwa vijana wa Inteharamwe hawapati muda wa kujijenga.

Kwa maneno mengine, Kagame ameifanya ardhi ya DRC kama uwanja wa mapambano kati yake na wapinzani wake ambao wako mashariki mwa nchi hiyo.

Jenerali Nyamwasa, ambaye kabla ya kukimbilia Afrika Kusini alikuwa Balozi wa Rwanda nchini India anasema kuwa Kagame ndiye aliyeamrisha kutunguliwa kwa ndege iliyokuwa imebeba ujumbe wa nchi hiyo  pamoja na Rais Juvenal Habyarimana na Cyprian Ntyaramira wa Burundi ambao ulikuwa umetokea Tanzania kwenye mkutano wa kujadili amani ya nchi hiyo.

Baada ya vita kumalizika na hatimaye RPF kuchukua uongozi, Ufaransa, mtawala  wa zamani wa Rwanda ilimtuhumu Kagame kwa kusababisha mauaji ya kimbari kwani Wahutu wasingianzisha chinja chinja ya Watutsi kwa wakati huo kwani mazungumzo yale yalikuwa yanaelekea ukingoni na hatua ya mwisho ingekuwa kwa RPF kuwa chama cha kisiasa ambacho kingeshiriki  kwenye uchaguzi.

Nia ya Kagame ilikuwa ni kuchukua uongozi Rwanda kwa nguvu kwa sababu kwa mizania ya siasa za nchi hiyo ambazo zimejikita zaidi kwenye ukabila ingekuwa vigumu kwa Watutsi walio wachache kushinda.

Sababu ya pili ambayo ndiyo iliyowafanya RPF wakatae au watumie nguvu ilikuwa ni juhudi ya Marekani ambayo ilikuwa mfadhili mkuu wa RPF kuhakikisha kuwa ushawishi wa Ufaransa katika eneo la Maziwa Makuu unaondoshwa kwa gharama yoyote.

Sunday, May 19, 2013

IRINGA PACHAFUKA, MSIGWA AKAMATWA!



Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) amekamatwa na polisi leo hii kwa tuhuma kuwa ndiye chanzo cha kuhamasisha wafanya biashara wadogo wadogo (wamachinga) kufanya vurugu huko Iringa.Askari polisi wa kutuliza ghasia (FFU) katika Manispaa ya mji wa Iringa pia imewakamata zaidi ya watu hamsini, akiwemoo aliyekuwa mgombea udiwani katika kata ya Mvinjini, Abuu Majeck.

Biashara zilisimama wakati wa sekeseke hilo, moshi ulitanda kutokana na matairi kuchomwa moto katika barabara za kuu ya Iringa-Dodoma na ile ya Mashine Tatu.

Leo hii pia, Mbunge huyo alikuwa katika eneo la chuo cha Tumaini kwenye harambee iliyokuwa imehudhuriwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.

Monday, February 4, 2013

WAFUASI CHADEMA, CCM WAGOMBEA MTI WA BENDERA



SHEREHE za miaka 36 za kuzaliwa kwa CCM jana ziliingia dosari, baada ya kuibuka vurugu kubwa kati ya wafuasi wa chama hicho na Chadema mkoani Dodoma wakati wakigombea eneo na mti wa kutundika bendera za vyama vyao.

Vurugu hizo zilizotulizwa na Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU), zilitokea jana mchana katika uwanja huo uliopo karibu na Baa ya Mwanga, baada ya CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwepo uwanjani hapo, ili waweke bendera zao kwa ajili ya mkutano ambao ulikuwa sehemu ya maadhimisho hayo.

Vurugu zilizuka baada ya wafuasi wa Chadema kuwataka wenzao wa CCM waendelee na mkutano katika eneo hilo kwa sharti la kurejeshwa kwa bendera iliyong’olewa. Wafuasi wa vyama hivyo wakiwamo wabunge wa CCM walionekana wakivutana kunyang’anyana mti wa bendera.

“Baada ya CCM kugoma, Chadema walijaribu kurudisha bendera hiyo kwa nguvu, jambo ambalo lilifanya wafuasi wa CCM waanze kuokota mawe na kuwarushia wapinzani wao hao, huku Chadema nao walianza kujibu mapigo,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.

Baadhi ya wabunge wa CCM walioshiriki katika vurugu hizo na majimbo yao kwenye mabano ni Ismail Aden Rage (Tabora Mjini), Nyambari Nyangwine (Tarime), Seleman Jafo (Kisarawe), Said Mtanda (Mchinga) na Mary Chatanda (Viti Maalumu).

Baadhi ya wafuasi wa CCM walionekana wakibeba mawe na kuwapiga wenzao wa Chadema na kusababisha tafrani kubwa katika eneo hilo la mkutano.


Katibu wa Chadema Wilaya ya Dodoma Mjini, Jellah Mambo alisema kuwa tukio hilo limetokana na wafuasi wa CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwa ikipepea eneo la Mwanga Baa kulikofanyika sherehe za chama chao (CCM).

Friday, October 19, 2012

WAKATI POLISI WAKITAWANYA WATU KWA MABOMU YA MACHOZI DARAJANI ZANZIBAR, DAR ES SALAAM HAMKANI SI SHWARI.




Pichani ni Vipeperushi  vilivyotolewa na Waumini wa Dini ya Kiislamu kabla ya maandamano leo.



Wakati Zanzibar Sakata la Waislamu kuendeleza kitimtim kufuatia kutoonekana kwa Kiongozi wa Kundi la Uamsho Vurugu zimeendelea kutawala eneo la Darajani na kusababisha Polisi kulazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya watu.

Jijini Dar es Salaam hali si tofauti na hiyo maeneo ya Kariakoo maduka kadhaa yamefungwa kufuatia vurugu kama hizo baada ya Swala ya Ijumaa kufuatia pia kukamatwa kwa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania Sheikh Ponda yamekuwa ni matokeo ya vurugu watu kukimbizana huku Polisi wakidhibiti Usalama na Amani kuelekea harijojo..

Maeneo ya Posta karibu na Wizara ya Mambo ya Ndani Askari wameweka utepe wa kudhibiti watu kuingia katika maeneo hayo kitendo kilichosababisha shughuli nyingi kusimama.

 Pichani ni Jeshi la Wananchi Tanzania likiwasilia maeneo ya Kariakoo kuongezea nguvu kwa ajili ya kutuliza ghasia.
 Baadhi ya waumini wanaodaiwa kutoka kikundi cha dini ya kiislamu wakidhibitiwa eneo la jirani na geti la Ikulu..mapema leo ambapo jumla ya watu 6, walikamatwa.
 Pichani ni maeneo ya Kariakoo magari ya jeshi JWTZ zaidi ya 8 yakiwa katika doria  maeneo ya Kariakoo.