To Chat with me click here

Friday, February 22, 2013

VIGOGO WATEMA CHECHE



WAKATI Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akiinyooshea kidole Serikali kwa kuzitelekeza shule za sekondari za kata, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa amesema hatajiuzulu ng’o kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne.

Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), nalo limetishia kuitisha maandamano ya nchi nzima kwa kushirikisha wanafunzi wote waliopata sifuri ikiwa waziri huyo hatajiuzulu.

Taifa limeshikwa na mshtuko kutokana na matokeo hayo ambayo yanaonyesha kuwa asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo mwaka jana, walipata sifuri.

Dk Kawambwa
Akizungumza jana katika uzinduzi wa Mpango Maalumu wa Mafunzo ya Kompyuta katika Shule ya Msingi ya Majengo wilayani Bagamoyo, Dk Kawambwa alisema hawezi kuachia ngazi kwa shinikizo la wanasiasa.

Alisema yeye si wa kulaumiwa kutokana na wanafunzi hao kufanya vibaya kwenye mtihani wa kidato cha nne na kwamba wanaosema waziri anapaswa kujiuzulu hawana hoja za msingi zaidi ya kutaka kujipatia umaarufu kwa kudandia hoja zinazokuwapo kwa wakati husika.

“Unajua katika mfumo wa vyama vingi, kila linapotokea jambo baya basi wanaona dawa ni kiongozi mhusika kung’oka. Unapozungumza waziri kujiuzulu hiyo ni lugha ya kisiasa lakini hata akijiuzulu inakuwa bado tatizo halijaweza kupatiwa ufumbuzi,” alisema.

Dk Kawambwa alisema hata Serikali haijafurahishwa na matokeo hayo mabaya na kushauri njia nzuri ni kutafuta dawa ya kukabiliana na tatizo la wanafunzi kufeli huku akiahidi kuwa wizara yake inaangalia tatizo hilo kwa karibu zaidi ili kujua chanzo chake.

Alisema amesikitika kuona hata shule ambazo zilikuwa zinategemewa kufanya vizuri zikiwamo za seminari, watu binafsi na kongwe za Serikali, nazo zimefanya vibaya.

Aliunga mkono maoni ya kutaka mfumo mzima wa elimu nchini uangaliwe upya kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa elimu.

Lowassa
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Lowassa alisema matokeo hayo ni aibu kwa taifa na kuilaumu Serikali kwa kuzitelekeza shule za sekondari za kata.
Alisema taifa kwa sasa linazalisha wabeba kuni na maji na siyo wasomi ambao wanaweza kushindana kwenye soko la ajira.

Alisema sekondari za kata ambazo zilianzishwa chini ya usimamizi wake akiwa Waziri Mkuu, zilikuwa ukombozi kwa Watanzania wengi wa kipato cha kawaida na ndiyo sababu waliitikia wito kwa kuchangia ujenzi, hatua ambayo alisema ilimpa faraja kubwa.

“Serikali tuliahidi kuzikamilisha shule hizo kwa kuzijengea maabara na kuhakikisha zina walimu. Ni wajibu wake kutimiza. Mimi ndiyo maana hata kwenye Katiba Mpya nilipendekeza uwezekano wa elimu ya sekondari kuwa bure, elimu ni kama mapigo ya moyo ya taifa ukiona hayaendi vyema lazima ujiulize,” alisema.

Lowassa, ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008, alisema tangu aondoke madarakani, shule hizo nazo zimetelekezwa.

Alimwomba Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua za makusudi, ikiwa ni pamoja na kuunda tume ili ichunguze kwa makini kiini cha matokeo hayo mabaya.

“Matokeo hayo ni aibu kwa taifa, walimu, wazazi na wanafunzi wenyewe. Namwomba kwa dhati Rais afanye kitu cha ziada, natambua mchango wa juhudi zake katika sekta nyingine ikiwamo ujenzi wa barabara nchini lakini elimu ndiyo iwe ya kwanza,” alisema.

Alitaka ufike wakati nchi iamue kuwekeza katika elimu tofauti na ilivyo sasa kwa Tanzania kuwa nchi inayotenga fedha kidogo zaidi katika sekta hiyo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Alisema Tanzania inatumia asilimia 1.4 ya bajeti yake, Kenya asilimia saba, Rwanda 5.8%, Uganda 4.8% na Burundi ni 3.2%.

Bavicha na maandamano
Bavicha imetishia kuitisha maandamano hayo yatakayowahusisha wanafunzi wote waliofeli ikiwa Waziri Kawambwa hatajiuzulu ndani ya siku 14 kama Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alivyomtaka Jumanne wiki hii.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Bavicha, Deogratius Munishi alisema wameshaanza kuwajulisha viongozi wa mikoa na wilaya kuhusu taratibu zote za kuandaa maandamano hayo.

Alisema kuwa lengo la maandamano hayo ni kutaka kushinikiza pia Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Shule za Sekondari wa Wizara ya Elimu kujiuzulu ili kupisha wengine watakaosimamia kikamilifu mabadiliko ya mfumo wa elimu nchini.

“Tunaitaka pia Serikali ya CCM ieleze hatima ya maisha ya vijana waliofelishwa na mfumo mbovu wa elimu,” alisema na kuongeza kuwa kuna wanafunzi 800,000 waliofeli ambao wako mitaani tangu tatizo la matokeo ya kidato cha nne lilipoanza mwaka 2009.

Alisema Serikali ya CCM ilikuwa na lengo la ufaulu wa asilimia 70 kwa kidato cha nne tangu mwaka 2009 lakini imekuwa kinyume chake.

“Ukweli usiofichika ni kuwa Serikali ya CCM haiwezi kufikia lengo la kuwa na taifa lililoelimika ifikapo 2025 kama ilivyobainisha kwenye dira yake ‘Vision 2025’ na badala yake itajenga taifa la watu mbumbumbu kwa wakati huo,” alisema.

MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2012: MATAIFA MAWILI KATIKA NCHI MOJA


Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Joyce Ndalichako akionyesha karatasi ya majibu ya mmoja wa watahiniwa wa mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2012, Dar es Salaam jana.

Kila Mtanzania sasa anajadili matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 yaliyotangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi mwanzoni mwa wiki hii. Matokeo hayo yanaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 90 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne walipata daraja la nne na daraja la sifuri. Dara la Sifuri limebeba asilimia 60 ya matokeo yote. Taifa limepata mtikisiko mkubwa kuona vijana wake wakiwa wamefeli kwa kiwango hiki.

Hata hivyo hii sio mara ya kwanza kupata matokeo ya namna hii. Ukiangalia matokeo ya kidato cha nne kuanzia mwaka 2009 utaona kuwa kila mwaka wanafunzi wanaofeli wanaongezeka. Mwaka 2011, wanafunzi 302,000 sawa na asilimia 89 ya wahitimu wote wa kidato cha nne walipata daraja la nne na sifuri. Mwaka 2010 wanafunzi 310,000 ambao ni asilimia 90 ya wahitimu walipata madaraja hayo ya chini kabisa na mwaka 2009 jumla ya wanafunzi 195,000 sawa na asilimia 78 ya wahitimu wote walipata madaraja ya sifuri na daraja la nne. Kila mwaka matokeo yakitangazwa kuna kuwa na mjadala wa wiki moja au mbili, wabunge tunapiga kelele kidogo kisha tunasahau kabisa suala hili mpaka matokeo mengine.

Hivi tumewahi kujiuliza hawa vijana wanaoishia kidato cha nne wanakwenda wapi? Wanafanya nini? Hii nguvu kazi kubwa ya Taifa inapotelea wapi?

Ni vema ifahamike kwamba Tanzania ni Taifa la vijana na watoto. Kwa mujibu wa taarifa za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, hivi Tanzania ina jumla ya vijana 38 milioni wa chini ya umri wa miaka 35 , hii ni sawa na idadi ya watu waliokuwepo Tanzania mwaka 2003.

 Asilimia 78 ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 35 na nusu ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 17. Kwa takwimu hizi ni dhahiri kwamba suala moja kubwa kuliko yote linalohusu Watanzania ni Elimu. Suala moja kubwa linaloweza kujenga au kubomoa Taifa hili ni Elimu. Suala moja kubwa linaloweza kuepuka matabaka katika nchi ni Elimu. Tena Elimu Bora, na BURE.

Kuna nadharia inaitwa ‘gawio la idadi ya watu’ na ‘bomu la idadi ya watu’. Nadharia hizi zatumika kuelezea namna mataifa yanaweza kufaidika au kupata hasara kutokana na kuwepo kwa nguvu kazi kubwa ambayo ama inatumika kwa faida ya nchi hiyo kwa kufanya kazi na kuongeza uzalishaji ama inatumika kwa kwa kukaa tu kwenye vijiwe na kupiga soga. 

Taifa ambalo linaandaa vijana wake kwa maarifa na stadi za kazi huvuna gawio (demograpich dividend). Mataifa yaliyofaidika na hali hii ni kama India, Uchina na Ujapani ambapo nyakati wana vijana wengi sana kuliko wazee vijana hawa walipewa ujuzi mkubwa na stadi za maisha na hivyo kuongeza uzalishaji mali kwa Taifa. Watu ndio mtaji mkuu wa Taifa lolote lile duniani. Taifa ambalo haliandai vijana wake kupata elimu huingia kwenye mgogoro mkubwa maana kundi la vijana wasio na kazi na wasio na maarifa yeyote ni sawa sawa na bomu.

Tanzania tuna chaguzi katika masuala haya mawili, ama tuvune gawio la kuwa na vijana wengi sana kwa kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika Elimu au tusubiri bomu lilipuke. Kwa matokeo haya ya kidato cha nne kwa miaka minne iliyopita, ni dhahiri tumeamua kulipikiwa na bomu.

Tunajua chanzo cha matokeo haya. Watoto hawasomi wala kujifunza shuleni. Hasa watoto wa vijijini ambapo hakuna walimu wala vitabu. Tumejenga mataifa mawili ndani ya nchi moja, Taifa la masikini na wana shule zao, wanapata masifuri kila siku. Taifa la walalaheri wana shule zao na wanapata madaraja ya juu. Hawa ndio watakaoenda vyuoni na wenye elimu wataendelea kutawala. Suluhisho ni moja tu, kuamua kwa dhati kabisa kuwekeza kwenye elimu kwa kuhakikisha kuna walimu wa kutosha, walimu wanalipwa vizuri na kuishi kwenye mazingira mazuri. Iwe na marufuku wenye kufeli ndio wafanye kazi ya ualimu.

Ni lazima kuhakikisha kuwa kunakuwa na vitabu vya kutosha kwenye mashule. Serikali ihakikishe kwamba inaingia makubaliano na wachapishaji wa vitabu wa ndani na kutoa vitabu vinavyojenga Taifa kwa kutoa maarifa ya uhakika kwa watoto. Ieleweke kwamba shughuli ya uchapishaji wa vitabu ni ajira tosha iwapo tutawezesha wachapishaji wa ndani kutoa vitabu vingi zaidi na vyenye ubora.

Matokeo ya mwaka huu ya kidato cha nne yanatuambia jambo moja kubwa sana, kwamba sisi ni Taifa linalokufa. Tuweke siasa pembeni na kahakikisha kwamba kunakuwa na uwajibikaji kwa viongozi kutokana na matokeo ya namna ya hii ya vijana wetu. Tusione tabu kubadilisha mawaziri wa Elimu kila mwaka kwa kuwafukuza kutokana na matokeo ya mitihani ya watoto wetu. Hii itafanya Waziri ajue umuhimu wa elimu anayoisimamia. Tukate mzizi wa fitina, elimu ni suala la uwajibikaji. Makala zijazo tutaona hatua za kuchukua ili kuhakikisha hawa watoto zaidi ya 300,000 waliofeli tunawafanya nini. 

Kwa hisani ya Zitto Kabwe | Zitto na Demokrasia

MZEE AMOS KAGUTA MUSEVENI (BABA WA RAIS MUSEVENI) AFARIKI DUNIA


Mzee Amos Kaguta Museveni (96)


KAMPALA, Uganda

“Rais Museveni na familia yote ya Kaguta, inasikitika kutangaza kifo cha baba yao mpendwa Mzee Amos Kaguta, 96, ambacho kimetokea leo Februari 22 saa 1 asubuhi kwenye Hospitali ya Kimataifa ya Kampala”

MZEE Amos Kaguta Museveni, baba mzazi wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda (pichani kulia), amefariki dunia leo asubuhi, taarifa kutoka Ikulu zimethibitisha kifo hiki.

Amos Kaguta amefariki akiwa katika Hospitali ya Kimataifa ya Kampala, alikokuwa amelazwa kwa siku kadhaa kwenye Wodi ya Wagonjwa Mahututi (ICU).

Baba huyo wa Rais, alikimbizwa hapo kutokana na matatizo ya tumbo aliyokuwa nayo, na kulazimisha familia yake kumkimbizia hapo kwa matibabu zaidi.

Rais Museveni
“Rais Museveni na familia yote ya Kaguta, inasikitika kutangaza kifo cha baba yao mpendwa Mzee Amos Kaguta, 96, ambacho kimetokea leo Februari 22 saa 1 asubuhi kwenye Hospitali ya Kimataifa ya Kampala.

“Familia inawashukuru madaktari wote kwa kujitoa na kupigania maisha ya Mzee Kaguta hadi umauti ulipomkuta.

“Taarifa zaidi juu ya mazishi yake zitatangazwa baadaye. Apumzike kwa Amani Mzee Kaguta,” ilisomeka taarifa fupi kutoka kwa Katibu Mkuu Msaidizi wa Idara ya Habari Ikulu, Lindah Nabusayi Wamboka.

Daktari wa familia, Diana Atwine alisema kuwa Mzee Kaguta alikimbizwa Hospitali baada ya kuanza kulalamika mamumivu ya tumbo, huku habari nyingine zikieleza kuwa marehemu alikuwa na matatizo ya kichwa.

Imeelezwa pia kwamba, Rais Museveni alikuwa akitembelea mara kwa mara hospitalini hapo, kujua maendeleo ya hali ya baba yake, hadi kifo kinamfika.

Kifo cha Amos Kaguta, kinamuacha Rais Museveni bila wazazi, baada ya mama yake mzazi Esteri Kokundeka kutangulia mbele ya haki mwaka 1997.

Mungu alitoa, Mungu ametwaa – Jina lake lihimidiwe, pia ailaze roho ya marehemu mahali pema PEPONI, Ameen.