NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, amekishutumu Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kwamba kinachonganisha viongozi wa chama chake kwa lengo la
kukidhoofisha wakati huu kinapoelekea kushika dola mwaka 2015.
Zitto alisema hayo jana alipokuwa
anazungumza na viongozi wa CHADEMA wa matawi na kata zote kutoka Jimbo la
Kigoma Kaskazini ukiwa ni mkakati wake wa kuendelea kukijenga chama na kujua
matatizo ya kisiasa na kijamii yanayowakabili wananchi wake.
Mbunge huyo ambaye ameamua kupiga kambi
jimboni humo kwa lengo la kuwazuia CCM wasipotoshe wananchi wake wakati huu
wanapoadhimisha miaka 36 ya kuzaliwa chama chao, alisema kuwa licha ya maneno
na uvumi kuzagaa kwamba CHADEMA Taifa inakabiliwa na mgogoro baina ya viongozi,
jambo hilo si kweli.
Zitto alibainisha kuwa hali hiyo
inakuzwa na watu waliopandikizwa na kutumiwa na CCM kwa ajili ya kuleta mpasuko
na kukigawa chama ili kupunguza kasi yake ya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka
2015.
“CHADEMA hakuna mpasuko wala migogoro
kama inavyotafsiriwa na wengi, badala yake kuna kakundi kanataka kutuhujumu kwa
kutugawa kwa kutumia itikadi za kidini, kimaeneo, kimitazamo na hata kiitikadi
kama walivyotumwa na hicho chama chao.
“Ninachoweza kusema ni kwamba ndani ya
chama chetu kuna majungu, fitina, kuoneana wivu, usaliti na hata kumalizana
kisiasa, haya tutahakikisha tunayamaliza kikatiba kwa sababu hiyo ndiyo sheria
mama inayotuongoza ili tufikie malengo tuliyojiwekea,” aliongeza Zitto.
Alidai kuwa wajibu wake ni kupigania
misingi ya uwajibikaji na demokrasia ndani ya CHADEMA ili kuondokana na vitendo
vya uongozi wa kutumia mabavu kama ilivyo kwa CCM, ambayo imekuwa ikitumia
nguvu katika kuendesha mambo yake, sambamba na serikali iliyopo madarakani.
Hata hivyo, aliwashutumu viongozi wa
jimbo lake kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo katika kujenga chama na badala
yake kila kitu kumtegemea yeye kama mbunge ikiwa ni pamoja na vikao na mikutano
ya hadhara.
“Ili tujenge chama chenye nguvu na
heshima, ni lazima viongozi wote tushirikiane kuanzia ngazi ya matawi, kata na
jimbo badala ya kila kitu kunitegemea mimi mbunge, lazima tuweke misingi imara
ya chama ili mgombea ajaye wa CHADEMA asipate wakati mgumu wa kufanya kampeni,”
alisisitiza.
Zitto aliongeza kuwa, wakazi wa Kigoma
kwa miaka mingi wamekuwa hawana mtetezi katika ngazi za kitaifa, kiasi kwamba
hoja za kuendeleza mkoa kwa kupatiwa miradi ya maendeleo zinapata upinzani
mkubwa kwenye vikao vya uamuzi kama vile Baraza la Mawaziri na Bunge.
“Lazima sisi watu wa Kigoma tuwe na
umoja kwa sababu tumekuwa wanyonge kwa miaka mingi, na daima nguvu ya wanyonge
ni umoja baina yaoNa sisi tunapaswa kuwa na umoja kwa ajili ya maendeleo ya
mkoa wetu na hata hii miradi inayoletwa Kigoma sasa ni kutokana na kelele
tunazopiga,” alisema.
Aliongeza kuwa hata kama hatagombea
nafasi yoyote ndani ya chama, bado ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu na
ataitumikia CHADEMA kwa vile misingi aliyoshiriki kuitengeneza kwa ajili ya
ustawi wa chama hicho bado haijakamilika na hawezi kuiacha ikiwa hivyo.