To Chat with me click here

Wednesday, June 13, 2012

KUFUATIWA KUSOMWA KWA BAJETI KESHO MAXMILLIAN KATTIKIRO ATOA MWONGOZO JUU YA BAJETI

Kufuatia kusomwa kwa bajeti ya mwaka wa Fedha (Julai mosi 2012 mpaka Juni 30, 2013) kesho bungeni na waziri wa husika wa wizara ya fedha na uchumi na Mipango, Ndg. Maxmillian Kattikiro, mwanaharakati na mpigania haki za wanyonge, ameona ni vyema wananchi wakafahamu zaidi kuhusu bajeti, hivyo ameamua kuifahamisha jamii juu ya bajeti ili wananchi wote kwa ujumla waweze kuwa na uwelewa wa kutosha juu ya bajeti vilevile kuwapa ufahamu na sababu za ufuatiliaji wa utekelezwaji wa bajeti hiyo.

BAJETI kwa kawaida imekuwa ikichukuliwa kuwa ni kazi ya wataalamu, wachumi na wahasibu tu. Lakini uamuzi wa Serikali wa namna gani ya kukusanya mapato huwaathiri wananchi wote. Kiwango cha kodi ya Ongezeko la Thamani (Value Added Tax - VAT) na kodi nyingine huathiri bei za vitu vinavyotumiwa katika kaya.

Uamuzi wa matumizi ya Serikali ndiyo huweka bayana iwapo viwango vya mishahara ya walimu vitapanda au la, na iwapo kutakuwa na dawa na vifaa vya kutosha katika zahanati au la. Wakati huo huo, bajeti  hutupatia pia nafasi ya kuelewa msukumo ‘halisi’ wa kisera wa Serikali katika ngazi ya Taifa na Wilaya.

Kimsingi, bajeti inahusiana na pesa za wananchi. Kwa bahati mbaya, mchakato wa kuamua namna ya kuzitumia na kusimamia pesa hizo na kuhakikisha kuwa zinaenda zinakotakiwa kwenda ni mgumu. Hali hii inawafanya wananchi wa kawaida washindwe kushiriki katika mchakato huo. Sehemu kubwa ya taarifa zinazohusiana na bajeti huwa haziwekwi wazi kwa umma, na hata zile zinazopatikana huwa zimeandikwa katika lugha ambayo huwa ni vigumu kueleweka kwa mwananchi wa kawaida. Hivyo, wananchi wengi hukosa fursa ya kushiriki katika michakato ya bajeti. 

Kutokana na hali hii, Ndg, Maxmillian Kattikiro kwa kushirikiana na wadau wegine na wachambuzi wa Bajeti, wameandaa mwongozo huu katika jitihada za kuziba pengo hilo la uelewa wa wananchi na kuwawezesha kushiriki kikamilifu zaidi katika mchakato huu. Mwongozo huu umetayarishwa kama sehemu ya jitihada za Ndg, Maxmillian Kattikiro katika kuirahisisha bajeti ili wananchi wengi waweze kuelewa mchakato wa bajeti nchini. 

Ninaamini kuwa ushiriki mkubwa zaidi wa umma katika kufuatilia bajeti utaboresha uwazi na uwajibikaji na hivyo kuziba mianya zaidi ya ufisadi. Pia tunaamini kuwa mwongozo huu utakuwa msaada mkubwa kwa wananchi na wawakilishi wa ngazi nyingine za chini katika kujadili na kufuatilia utekelezaji wa bajeti.   

Bajeti ni nini?
Bajeti hutueleza namna fedhaa za umma zinavyotumika. Pia bajeti huelezea kuhusu vyanzo vya fedha au mapato ya serikali. Vyanzo vya mapato ya serikali hutokana na kodi mbalimbali, ushuru wa vitu (VAT) na misaada kutoka nchi wahisani. Bajeti huelezea namna fedha au mapato ya serikali yanavyotumika. Kwa mfano kutoa mafunzo kwa walimu, kujenga wodi za hospitali na kuboresha barabara zilizopo. Kila mwaka huandaliwa bajeti mpya. Mwaka wa fedha unatofautiana na mwaka wa kawaida kwa mujibu wa kalenda. Mwaka wa fedha huanza Julai 1 na kuisha Juni 30. Taarifa zinazohusu Bajeti huwasilishwa siku ya Bajeti. Tarehe ya kusomwa Bajeti hutangazwa kupitia magazeti, radio na TV.

Bajeti hutumika katika maeneo makuu mawili – matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo. Matumizi ya kawaida hufanyika kila mwaka na hujumuisha mishahara, gharama za vyombo vya usafiri, nishati, makongamano pamoja na utawala. Matumizi ya maendeleo hujumuisha upanuzi wa miundombinu na haufanyiki kila mwaka. Miundombinu hii hujumuisha ujenzi wa barabara, shule pamoja na hospitali. Ukarabati wa majengo na barabara hugharimiwa na fedha zilizotoka kwenye matumizi ya kawaida.

Kwa nini ni muhimu kuielewa bajeti na mchakato wa bajeti?
Ni muhimu kutambua mchakati mzima wa Bajeti ili kufahamu mambo yanayopewa kipaumbele na serikali kwa niaba yako. Hali hii itakusaidia kutambua namna mapato ya serikali yanavyotumika na utakuwa na uwezo wa kuhoji uhalali wa matumizi hayo. Kwa mfano utaweza kujua ni kiasi gani cha fedha ambacho serikali imepanga kutumia kwenye makongamano au magari. Pia utaweza kulinganisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi mengine na zile zilizotengwa kwa ajili ya mishahara ya walimu na vitabu.

Mchakato wa Bajeti ya Taifa.
Mchakato wa bajeti huwahusisha watu wengi. Wote wana kazi na majukumu mbalimbali kama inavyoonekana hapa chini. 

Fedha zinatoka wapi?
Fedha (mapato ya serikali) zinatoka kwenye vyanzo viwili- Mapato ya ndani na misaada kutoka nchi wahisani. Mapato ya ndani hutokana na kodi mbalimbali. Kodi hizo ni pamoja na kodi ya mapato ambayo hulipwa na mtu yeyote mwenye ajira ya kudumu. Kodi hii pia inajulikana kama kodi ya mishahara yaani PAYE. Kodi ya biahashara (Corporate Income Tax) ambayo hulipwa na wafanyabiashara. Kodi nyingine ni Kodi ya thamani (VAT) ambayo hutozwa kwenye bidhaa pamoja na huduma zingine. Pia kuna ushuru unatozwa kwa bidhaa zinazoingia ndani ya nchi, kwa mfano magari.

Mapato mengine ya ndani hutokana na leseni. Kwa mfano leseni ya biashara ama kufanya shughuli za kitabibu pamoja na ada. Kwa mfano uzoaji wa takataka au leseni za ujenzi. Serikali pia inaweza kupata fedha kutokana na ubinafishaji (uuzaji) wa rasilimali zake.

Misaada kutoka nchi za nje ni fedha zinazotolewa na nchi wahisani na taasisi za kimataifa za fedha. Benki ya Dunia pia huchangia sana katika Bajeti nzima. Fedha hizi huja kama misaada na mikopo. Misaada huwa hailipwi wakati mikopo huhitajika kurejeshwa hapo baadaye. Fedha hizi zimegawanyika katika mafungu yafuatayo: Kuchangia miradi mbalimbali (Project Funding), zile zinazoingizwa  katika mfuko wa fedha za serikali (Basker Funding) na zile zinazoingia katika mfuko wa Jumla wa Bajeti (General Budget Support). Fedha zinazolengamiradi hutolewa moja kw moja na nchi wahisani au taasisi za fedha za kimataifa kwa ajili ya kuhudumia miradi Fulani. Kwa mfano fedha  zilizotolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya kuhudumia mpango wa maendeleo ya elimu  ya msingi MMEM. Pale nchi wahisani wanaposhirikiana kuchangia mradi mmoja au mradi Fulani basi hali hiyo hujulikana kama kuchangia sekta ya afya au mradi wa barabara yaani TANROADS. Utaratibu ulizoeleka kwa sasa ni kwa nchi wahisani kuchangia fedha kwa ajili ya bajeti kwa ujumla. Nchi wahisani huipatia serikali kuu fedha.Serikali ya Tanzania hufanya uamuzi wa namna, wapi na lini fedha hizo zinaweza kutumika.    

Mzunguko wa Bajeti ya Taifa
Mzunguko wa Bajeti ya kitaifa hufanyika ndani ya mwaka mzima. Mzunguko huo una hatua nne: 
  1. Novemba hadi Mei - Muda wa Mipango (Mamlaka ya Mapato {TRA},Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango, Wahisani, pamoja na Wizara nyingine)
  2. Juni hadi Agosti-Kujadili kupitisha bajeti {Bunge} 
  3. Julai hadi Juni - Mwaka wa Fedha {Utekelezaji wa Bajeti}
  4. CAG, CSDS, WIZARA etc. (Kuona jinsi Fedha ilivyokusanya na kutumika kama iivyopangwa). 
NB: 
Sehemu ya Pili itaendelea Kesho usikose kuungana na Maxmillian Kattikiro katika mwongozo huu ili kufahamu zaidi juu ya bajeti na jinsi gani ya kuhakikisha utekelezwaji wake.

Mungu ibariki Tanzania. 

2 comments:

  1. Hivi bajeti ya Tanzania huwa inafanya kazi gani?mbona bajeti hutangazwa kila mwaka wa fedha lakini hatuoni maanikio yake matokeo yake maisha ndiyo yanazidi kuwa magumu zaidi

    ReplyDelete
  2. Ndugu, bajeti kama yenyewe ni sahihi kabisa kuandaliwa na kusomwa bungeni ili ijadiliwe na bunge pia kupewa baraka na bunge ili kutekeleza miradi ya maendeleo ya nchi ambavyo ndiyo vipaumbele kwa wananchi.

    Lakini tatizo linakuja pale watu wachache wenye mamlaka ya kusimamia utekelezwaji wa bajeti hiyo katika kila ngazi za utekelezwaji wake, kutokuwa na uzalendo wa dhati katika kutekeleza majukumo yao. Hivyo utakuta vile vipaumbele vya kimaendeleo ambavyo wananchi wamevipendekeza havitekelezeki, na matokeo yake hali hubaki kuwa vile vile au ngumu zaidi.

    Ili kuwasaidia wananchi ndo maana nimnejaribu kuweka mwongozo huu,ili kila mmoja wetu afahamu wajibu wake na aweze kufuatilia ili kuhakiki utekelezwaji wa bajeti husika. Ili kuendelea kuelewa zaidi tafadhali endelea kusoma sehemu zifuatazo za mfululizo wa mwongozo huu.

    Asante kwa kunifuatilia.

    ReplyDelete