To Chat with me click here

Friday, June 15, 2012

BAJETI MWONGOZO - SEHEMU YA 3.


Mzunguko wa bajeti katika Serikali za Mitaa


Bajeti ya Serikali za Mitaa hufuata utaratibu ule ule unaotumiwa na bajeti ya serikali kuu. Hatua ya 1 na 2 inahusu upangaji wa bajeti na hatua ya 3 na 4 inahusu matumizi  na ufuatiliaji. Jedwali lifuatalo linafafanua zaidi kuhusu Mzunguko wa Bajeti ya Serikali za Mitaa. 

Hatua
Mwezi
Shuguli
Mhusika
Hatua

Hatua ya 1 na 2: Kupanga
Novemba – Desemba
OFISI YA WAZIRI MKUU- TAMISEMI huwasiliana na wizara husika. Hutoa miongozo ya Bajeti kwenye serikali za mitaa (LGAs)
OFISI YA WAZIRI MKUU-TAMISEMI

Hatua ya 3  na 4: matumizi na ukaguzi
Januari
LGA ina 50% ya fedha kwa ajili ya matumizi kutoka katika mfuko wa maendeleo wa serikali za mitaa (MKUKUTA.) Huandaa bajeti.  Kamati za maendeleo za Kata na viji nazo hupatiwa asilimia 50 nyingine ya fedha kwa ajili ya matumizi katika kata na vijiji.
Halmashauru ya wilaya/Kamati ya Maendeleo ya kata/Halmashauri ya kijiji.
Februari
Wana vijiji huchagua vipaumbele na huandaa bajeti kwa kutumia mchakato wa kuangalia fursa na vikwazo vya maendeleo. Maofisa wa kata wa wilaya husaidia katika kuandaa bajeti. Mipango hukubaliwa na halmashauri ya kijiji na mkutano mkuu wa kijiji
Halmashauri ya kijiji/mkutano mkuu wa kijiji
Machi
Kamati ya Maendeleo ya Kata huijadili na kuiunganisha mipango ya vijiji katika mipango ya kata. Mipango hupelekwa katika halmashauri ya wilaya, miji, manispaa na jiji.
Mamlaka ya serikali za mitaa na kamati ya maendeleo ya kata
Machi-Aprili
Mamlaka ya serikali za mitaa huijadili mipango ya kata na kuiunganisha katika mipango yake
Idara ya mipango ya halmashauri ya wilaya, mji, manispaa au jiji.

Aprili
Halmashauri huipitia, huijadili pamoja na kuipitisha mipango ya mamlaka ya serikali za mitaa. Sekretariati ya Mkoa huichambua mipango hiyo. Baada ya hapo mipango hiyo hupelekwa ofisi ya waziri mkuu TAMISEMI.
Halmashauri ya wilaya, kamati ya mipango ya wilaya, Sekretariati ya Mkoa (RS), ofisi ya waziri mkuu TAMISEMI

Mei
Ofisi ya waziri mkuu-TAMISEMI huchambua mipango yote ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGA) na kuiunganisha kwenye bajeti ya taifa ambayo huwasilishwa bungeni.
Ofisi ya waziri mkuu TAMISEMI .Bunge

Juni –Julai
Bunge hujadili na kupitisha bajeti ya ofisi ya waziri mkuu-TAMISEMI.
Ofisi ya waziri mkuu TAMISEMI /Bunge

Agosti
Ofisi ya waziri mkuu-TAMISEMI huziarifu halmashauri kuhusu bajeti. Fedha za kila mwezi huanza kusambazwa katika halmashauri.
Ofisi ya waziri mkuu TAMISEMI /Bunge

Septemba
Halmashauri huzifahamisha kata pamoja na vijiji kuhusu bajeti. Utekelezaji wa miradi huanza kufanyika.
Halmashauri / kata/vijiji

Hatua ya 1 na 2: 
Kupanga Matumizi ya Fedha
Ubainishaji wa fursa na vikwazo katika mchakato wa maendeleo (O&OD) unalenga kuhakikisha kuwa vipaumbele vya vijiji vinajumuishwa katika bajeti ya taifa. Ni muhimu kushiriki katika mchakato huu ili kuhakikisha kuwa mahitaji pamoja na sauti zenu zinasikika.

Mchakato wa kuangalia fursa na vikwazo vya maendeleo hufanyika kwa muda wa siku 9 Wanakijiji hujadili mahitaji yao ya kimaendeleo pamoja na changamoto wanazokumbana nazo katika kufikia maendeleo yao. Kwa mfano ukosefu wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vyoo katika shule za msingi; au ukosefu wa vifaa kwa ajili ya kufukia mashimo yaliyopo barabarani. Mpango huu huratibiwa na halmashauri ya kijiji kabla ya kuwasilishwa katika mkutano mkuu wa kijiji kwa ajili ya kupitishwa. Afisa mtendaji wa kata pamoja na muwezeshaji wa O&OD husimamia mchakato mzima.

Hatua ya 3: 
Matumizi ya Fedha
Wizara ya fedha (MoF) hupelekea fedha halmashauri kila mwezi. Kiwango cha fedha kinachopelekwa katika halmashauri hutangazwa kupitia magazeti. Halmashauri huvifahamisha vijiji, kata na mitaa kuwa fedha zimeletwa na serikali. Mchanganuo mzima wa fedha hizo huwekwa katika mbao za matangazo. Halmashauri huandaa utaratibu wa jinsi fedha hizo zitakavyotumika katika kata, vijiji na mitaa. Utekelezaji wa miradi huanza mara moja.

Kama kutakuwa na mabadiliko katika bajeti iliyopitishwa mwanzo, basi halmashauri ina wajibu wa kukufahamisha kuhusu mabadiliko hayo na una haki kuhoji sababu za mabadiliko katika bajeti hiyo.

Fedha zinazotumika katika kununua vitu pamoja na huduma kama vile vifaa vya ujenzi, vitabu mashuleni, pampu za maji pamoja na kulipa wataalamu mbalimbali huitwa manunuzi. Manunuzi yote lazima yaratibiwe na bodi ya zabuni ya wilaya na yanatakiwa kufanyika kwa haki, ushindani na kwa uwazi zaidi. ‘Fedha za umma’ lazima zithaminiwe na wala si urafiki.   

Hatua ya 4: 
Kuhakiki kama fedha zilizotengwa zinatumika katika miradi iliyopangwa.
Halmashauri huwasilisha ripoti katika ofisi ya waziri mkuu-TAMISEMI kila baada ya miezi mitatu kuelezea kama fedha zilizopokelewa zimetumika kwa usahihi na kufuata bajeti iliyopangwa. Ripoti hii huwasilishwa mbele ya kikao cha halmashauri   na lazima iwekwe wazi.

Halmashauri ya kijiji (VC), Baraza la Mtaa (MC) na halmashauri ya kata hukutana kila baada ya miezi mitatu lengo likiwa ni kuratibu mipango ya maendeleo katika halmashauri. Halmashauri ya kijiji na baraza la mtaa zinawajibika kuwasilisha ripoti katika mkutano mkuu wa kijiji au mtaa ambao huwahusisha watu wazima wote katika kijiji au mtaa huo. Mahesabu ya halmashauri hukaguliwa na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG). Fedha zingine kama vile za mradi wa Barabara, Afya, Maendeleo ya Elimu (MMEM), maboresho ya serikali za mitaa pamoja na fedha zinazotolewa na wahisani, wenyewe hukaguliwa tofauti. Fedha zinazotolewa na LGCDG hukaguliwa kila mwaka ifikapo mwezi Septemba.  

Jinsi unavyoweza kushiriki
Ushiriki wako katika mchakato wa bajeti ni muhimu sana kwa sababu unakupa wewe fursa ya kuhakikisha maoni yako yameingizwa katika maamuzi ya bajeti. Ushiriki wako utawezesha vipaumbele vyako kuzingatiwa katika bajeti. Unaweza kushiriki katika hatua zote za mchakato wa bajeti kama ifuatavyo.

Hatua ya 1 na 2: Kupanga jinsi ya kutumia fedha
Unaweza kuwashawishi waandaaji wa bajeti kwa kuwaeleza kuhusu masuala yanayotakiwa kupewa kipaumbele. Labda unaweza kufikiria kuwa kuwaongezea walimu mshahara ni jambo muhimu au kutoa ruzuku kwa dawa pamoja na usambazaji wake.

o   Mchakato wa fursa na vikwazo vya maendeleo: Huu ni mpango shirikishi ambapo kila mwanakijiji anapaswa kushirikishwa kuanzia hatua ya awali. Ni vizuri uhudhurie vikao ili kutoa maoni yako kuhusu mambo yatakayoamuliwa kuhusu maendeleo na mahitaji ya kijiji chako. KILA MMOJA lazima ashiriki: wanawake, wanaume, vijana, wazee, wasiojiweza pamoja na masikini. Kila mmoja ana haki ya kushiriki na ana haki ya kusikilizwa. Vipaumbele vya kijiji ni lazima vizingatiwe wakati wa kuandaa bajeti.

o   Mikutano mikuu ya kijiji: Mikutano hii huitishwa kila mwezi. Wanawake na wanaume wote wanaoishi katika kijiji husika ni muhimu kuhudhuria. Unaweza kuuliza maswali na kudai masuala muhimu uliyoyapendekeza yawepo kwenye bajeti.

o   Kamati ya maendeleo ya kata (WDC): Mikutano ya WDC ipo wazi kwa wananchi wote kuhudhuria. Unapaswa uhudhurie ili kuhakikisha kuwa mipango ya maendeleo ya kijiji chenu imeingizwa kwenye mpango wa maendeleo wa Kata. Mpango huu hupelekwa kwenye halmashauri.

o   Mjadala wa Baraza na upitishaji wa bajeti: Unaweza kuhudhuria vikao vya Baraza la halmashauri ya wilaya ili kuhakikisha kuwa vipaumbele vilivyojadiliwa katika kijiji chenu vinatetewa na diwani wenu. Wananchi wanaweza kuwahamasisha madiwani wao ili watetee maslahi ya jamii zao pamoja na kuhakikisha kuwa mambo yote yaliyokubaliwa yamejumuishwa katika bajeti na mpango wa maendeleo wa wilaya.

Hatua ya 3 na 4: Kutumia fedha na kuhakikisha kama inatumika kwa usahihi.

Unaweza kufuatilia matumizi ya fedha ili kuhakikisha kama fedha zilizoombwa zinatumika kwa usahihi: kwa mfano kama mwanafunzi mmoja ametengewa Dola kumi za Marekani kwa mwaka kwa ajili ya shule, basi unaweza kukagua kama shule imepokea fedha hizo kutoka serikalini na iwapo zinatumika kama zilivyopangwa. Vile vile unapaswa uhakikishe kuwa huduma zilizotolewa kwa ubora unaotakiwa na kwa wakati muafaka.

Wananchi kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia (CSO) wana nguvu na mamlaka katika kusimamia utendaji wa halmashauri (LGA). Kama unapenda, ni muhimu kuwasiliana na Asasi za Kiraia iliyo karibu nawe ili kusaidia kufanikisha mchakato huu. Kuna namna nyingi za kufanya; udhibiti wa matumizi ya Fedha za umma (PETS), usimamizi wa huduma za jamii na usimamizi wa matumizi ya fedha.

o   Usimamizi wa matumizi ya Fedha za umma: Hii hufiatilia matumizi ya Fedha kuanzia pale serikali inapozipokea hadi mwisho. Unaweza kuuliza maswali kama vile: Je, fedha zinatumika kama zilivyopangwa? Je, fedha zimefika kwa wakati? Je, kiwango cha fedha kilichopokelewa ni sahihi? Je, fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi fulani zimetumika kama ilivyopangwa? Je, huduma zimeboreshwa?

Mfano wa mbinu za kutumia katika kufuatilia matumizi ya umma ni kupitia kadi za viwango za kijamii (PIMA Cards). Jamii huandaa kadi maalumu zinazoonesha kiwango cha kuridhishwa ama kutoridhishwa na huduma zinazotolewa. Maswali huandikwa kwenye kadi. Huu ni mfano mojawapo wa kupima ni kwa jinsi gani kilimo kimeboreshwa. Kuna kamati maalum ambayo huchaguliwa na kupewa mafunzo ya jinsi ya kukusanya habari kutoka kwa raia wengine. Taarifa hiyo huratibiwa na kuwasilishwa katika halmashauri. 

KILIMO NA MASOKO - UZALISHAJI
B1
HUDUMA
B1 . 1
JE, HUDUMA GANI ZA KITAALAMU ZILIZOTOLEWA MWAKA JANA KATIKA KIJIJI CHAKO?
JE, ULIRIDHISHWA NA HUDUMA HIZO?

UDHIBITI WA WADUDU,
MBEGU ZILIZOBORESHWA,
USHAURI WA KITAALAMU,
USHAURI WA UTUNZAJI WA NAFAKA,
TIBA YA MIFUGO,
UTUNZAJI WA MAZINGIRA,
KUZUIA MMOMONYOKO,
KUANZISHWA VYAMA VYA MSINGI,
MBINU ZA UMWAGILIAJI,
UHIFADHI WA MAZAO,
UHIFADHI WA MAZAO YA MIFUGI
HAZIKUTOLEWA
HAFIFU
INARIDHISHA
VIZURI




 
 o   Ufuatiliaji wa uwajibikaji wa kijamii: Hii husimamia na kufuatilia utoaji wa huduma za kijamii kwa kuhakikisha kuwa serikali inatoa huduma kwa wakati muafaka, kwa ufanisi na kwa kulingana na thamani halisi ya fedha zilizotengwa. Kinyume na hivyo, viongozi wa serikali wanapaswa kuwajibika. Ni muhimu kuhakikisha kuwa fedha zilizotengwa zinatumika kwa uangalifu na kwa ufanisi. Watumishi au idara zinazoshindwa kutoa huduma kwa ubora ni muhimu waeleze ni kwa nini huduma zinazotolewa hazina ubora. Unaweza kusimamia utendaji wao.

o   Usiamamizi wa fedha: Unaweza kuisoma na kuifanyia kazi ripoti ya kila mwaka inayotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG). Katika kipindi cha mwaka 2006 na 2007, Taasisi mbalimbali mfano mzuri: HakiElimu, ziliandaza machapisho yanayoelezea mapato pamoja na taarifa kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mfumo rahisi. Idara za serikali kuu pamoja na halmashauri zilizowekwa katika viwango vya ubora katika utendaji kuanzia Idara ya kwanza kiufanisi hadi mwisho. Machapisho haya yalisaidia kuongeza uelewa juu ya usimamizi wa fedha za umma. Unaweza kupata taarifa kamili ya bajeti kutoka katika ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) au kwa kusoma machapisho ya vyombo mbalimbali vya habari. Kama utakuwa hujaridhika unaweza kuomba maelezo zaidi kutoka kwenye halmashauri yako kama changamoto.   

NB: Usikose kesho kupata sehemu ya mwisho wa Mwongozo wa Bajeti.

No comments:

Post a Comment