To Chat with me click here

Saturday, June 16, 2012

NWONGOZO WA BAJETI SEHEMU YA MWISHO.


Changamoto
Zipo changamoto nyingi unazoweza kukutana nazo pale unapoamua kushiriki kikamilifu katika mchakato wa bajeti. Baadhi ya changamoto hizi ni kama zilivyoainishwa katika sehemu inayofuata.

Changamoto

Ukosefu wa takwimu sahihi ambazo imekuwa ngumu kuzipata: Hii inamaanisha kwamba serikali za mitaa zimekuwa hazina uhakika kuhusu kiwango cha fedha zinazotakiwa kupokelewa katika halmashauri. Hali hii imekuwa kikwazo katika upangaji wa mipango endelevu.

Upotevu wa vipaumbele: Hii hutokea kwa sababu bajeti hujadiliwa na ofisi nyingi na katika ngazi tofauti tofauti na hivyo kusababisha baadhi ya mipango iliyopangwa hapo awali kusahaulika. Fedha zinazotolewa na serikali kuu zinaweza kuelekezwa mradi ambao wananchi hawakuuchagua.

Fursa na changamoto za maendeleo pamoja na makundi ya pembezoni pia yanaweza kusahaulika.

Kuchelewa kwa mpango wa maendeleo katika halmashauri huchelewesha pia miongozo ya bajeti katika kata na vijiji.

Serikali kuu kuchelewa kutuma fedha katika halmashauri: Hali hii husababisha miradi ya maendeleo kuchelewa kuanza na vilevile kuchelewa kumalizika kwake.

Ni muhimu utambue changamoto hizi kabla ya kuchukua hatua yoyote. Kumbuka kuwa ushiriki wa raia na uhitaji wa uwajibikaji ni mambo muhimu katika kuleta mabadiliko yoyote. Una haki ya kupata taarifa na kujibiwa maswali yako.

Mahali tunapoweza kupata Taarifa zaidi.
Halmashauri zinawajibika kisheria kubandika taarifa kuhusu bajeti kwenye mbao za matangazo zilizopo katika halmashauri husika. Pia taarifa kuhusu bajeti hutangazwa kupitia vyombo vya habari. Vyombo hivyo hutoa taarifa muhimu kuhusu bajeti. Kwa mfano hutangaza kuhusu kiasi cha fedha kilichopokelewa na halmashauri kutoka serikali kuu. Afisa mipango wa wilaya na wajumbe wa halmashauri, Kata pamoja na maofisa watendaji wa vijiji wana wajibu wa kukupatia taarifa kuhusu mipango ya bajeti, maendeleo yake pamoja na taarifa zingine muhimu. Kwa bahati mbaya baadhi ya maofisa wa serikali hawatoi ushirikiano mzuri hasa linapokuja suala la kutoa taarifa muhimu kuhusu bajeti.

Kumbuka
Kama hutashiriki kuna madhara yake vilevile. Kitendo cha wewe kutoshiriki kitasababisha serikali itelekeze mipango yake ya maendeleo bila kuangalia mahitaji yako. Ushiriki hukufanya ujisikie kwamba miradi ya maendeleo ni mali yako na inaendelezwa kulingana na vipaumbele ulivyojiwekea.

o   Kupata huduma za jamii ni haki yako na wala si hisani.
o   Hata pale ambapo rasilimili zitakuwa hazitoshi ni lazima zigawiwe kwa usawa kwa kuzingatia haki.
o   Dola ina wajibu wa kutumia rasilimali zake kuhakikisha kuwa raia wanatambua haki zao pamoja na uwezo wao.
o   Wale wanaodhibiti fedha za umma pamoja na wale wanaohusika katika kutoa huduma, wanawajibika katika kutoa maelezo ni kwa nini wameshindwa kuwatumikia wananchi kwa ufanisi.
o   Pale rasilimali za umma zinapotumiwa vibaya au kuharibiwa, vyombo vya udhibiti kama vile Bunge pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali vinapaswa kuchukua hatua.
o   Raia wana haki kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumiwa kama zilivyopangwa. Kama kutakuwa na matumizi mabaya ya fedha za umma, watumishi wanapaswa kuhojiwa.
o   Maendeleo huanzia pale unapokuwa na shauku ya kujua wapi kodi yako inapelekwa.
o   Ushiriki na matendo huleta mabadiliko.

Wadau mbalimbali wanaweza
o   Kubadilishana mawazo na wewe kuhusiana na jinsi ya kutatua matatizo yako.
o   Kukuunganisha na Asasi zenye rasilimali ambazo zinaweza kukusaidia kuleta mabadiliko.
o   Kuunga mkono juhudi zako ili uweze kutambua haki zako.
o   Kufanya kazi na wewe ili kuendeleza uwezo wako.

NB: 
Watanzania wenzangu, nashukuru sana kwa kuwa umekuwa nami katika mfululizo wa mwongozo wa bajeti tangu sehemu ya kwanza mpaka sehemu hii ya mwisho. Kuelewa, kushiriki pamoja na kuifuatilia bajeti ni jambo la muhimu kwa kila mtanzania mwenye kupenda maendeleo ya kweli. 

Hivyo napenda kuwaasa watanzania wote kwa ujumla kuwa, tusichoshwe wala kupuuzia juu ya ufuatiliaji wa bajti za halmashauri zetu ili kujua ni jinsi gani pesa zetu za kodi zinavyotumika na kama zinakidhi haja na kutekeleza vipaumbele vyetu katika maendeleo ya halmashauri zetu na Taifa kwa ujumla. 

Unaweza kunitumia email: kattymax2001@yahoo.com au kunifuatilia katika blog hii ili kuendelea kupata elimu zaidi. 

Mungu ibariki Tanzania na watu wake.

No comments:

Post a Comment