To Chat with me click here

Monday, June 18, 2012

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI NDUGU KABWE ZUBERI ZITTO (MB), WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI, KUHUSU MAPENDEKEZO YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013


I. UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, ninatoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Bajeti ya Nchi ya mwaka wa fedha2012/2013 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99(7) toleo la Mwaka 2007. 

Mheshimiwa Spika, Natoa pongezi za dhati kabisa kwa Ndugu William Augustao Mgimwa, Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa kwa kuteuliwa na Rais kuwa Waziri wa Fedha na Uchumi.

Vile vile nawapongeza Ndugu Saada Mkuya na Ndugu Janeth Mbene kwa kuteuliwa kwao kuwa Wabunge na baadaye kuwa Manaibu Mawaziri  katika Wizara hii nyeti sana. Ninawapa pole pia maana Wizara ya Fedha sio Wizara lelemama. Kambi ya Upinzani itaendelea kuisimamia Wizara hii kwa ukaribu sana kama ilivyofanya katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Mtakapofanya vizuri tutawapongeza ili muongeze juhudi, mtakapoharibu tutawawajibisha.

Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kwamba Mwaka wa Fedha uliopita ulikuwa mwaka mgumu sana kwa Watanzania. Ni mwaka ambao gharama za maisha zilipanda kwa kasi kubwa sana na juhudi za Serikali kuwakwamua wananchi na hasa wananchi wanyonge kutoka kwenye lindi la ufukara ziligonga mwamba. Kambi ya Upinzani inawapa pole Watanzania kwani hili ndilo walilochagua.

No comments:

Post a Comment