LICHA ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwataka madaktari nchini
kurejea katika meza ya mazungumzo, kwa maelezo kuwa baadhi ya madai yao
yameshughulikiwa, wataalamu hao wamemjibu wakisisitiza kwamba mgomo wao
upo pale pale kuanzia kesho.
Madaktari hao wamesema kuwa Waziri Mkuu, amelidanganya Bunge jana
wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo, kwa kuesema kuwa kati ya madai
yao kumi waliyowasilisha, matano yameafikiwa na kila upande.
Kwa mujibu wa madaktari, wiki mbili za mgogoro na serikali walizozitoa
zinamalizika leo, hivyo kuanzia kesho kada zote wanaingia katika mgomo
usiokuwa na kikomo. Majibu ya madaktari hao, yalitoka na kauli ya Pinda bungeni jana
wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe
(CHADEMA), aliyetaka kujua malumbano kati ya serikali, madaktari na
walimu yatatatuliwa lini ili kuepusha mgomo.
Katika hilo, Pinda, alilieleza Bunge kuwa tangu awali serikali iliunda
kamati maalumu ya kushughulikia suala hilo ambapo miongoni mwa madai
yao kumi, matano yameafikiwa na kila upande. “Ninajua uzito wa hili jambo na lilipotokea tulijitahidi kuhakikisha
tunaunda kamati maalumu ili kuweza kushughulikia masuala haya, na kwa
mujibu wa kamati ni mambo matano kati ya kumi, tumeafikiana kwa pamoja,”
alisema na kuongeza kuwa: “Baada ya hatua zote hizo kwa mujibu wa sheria ni lazima makubaliano
yao yasajiliwe na Tume ya Usuluhishi (CMA), na kwamba hilo limefanyika
ambapo tume ya serikali na upande wa madaktari wamemaliza kazi yake.
“Hata hivyo mambo matano yaliyobaki, nilimuagiza tena Waziri wa Afya
awaandikie barua madaktari ili waweze kukutana, lakini hadi juzi
wanajibu barua ile wanasema hawazezi kukutana tena na serikali kwa
sababu haijatelekeza madai yao,” alisema Pinda.
Kwamba kati ya madai waliyotaka na serikali imeyatekeleza ni pamoja na
kuondolewa kwa mawaziri wa wizara hiyo, kuongezwa posho ya kuitwa
kazini, kufanya uchunguzi wa maiti na nyinginezo.
“Lakini pamoja na hali hii serikali ilifungua kesi ikilalamikia mgomo
wa madaktari uliotokea mwanzoni mwa mwaka huu, tume ya usuluhishi
ilizitaka pande mbili, kamati ya serikali na wawakilishi wa madaktari
kukaa meza moja na kuzungumza Juni 19, mwaka huu,” alisema.
Alifafanua kuwa mambo matano waliyoafikiana ni serikali kukubali
kuongeza posho ya kuitwa kazini kutoka sh 10,000 hadi sh 15,000 kwa
madaktari walio kwenye mafunzo kazini na sh 20,000 kwa madaktari na sh
25,000 kwa madaktari bingwa.
“Pia serikali iliongeza posho ya uchunguzi wa maiti kutoka sh 10,000
hadi 100,000 kwa madaktari na sh 50,000 kwa wasaidizi,” alisema Waziri
Mkuu Pinda.
Aliongeza kuwa serikali ilikubali kuwapa kadi ya Bima ya Afya ya rangi
ya kijani ambayo ina hadhi ya huduma za daraja la kwanza kwa madaktari,
pia kutoa chanjo ya ugonjwa wa ini ambapo fedha za chanjo hiyo zimo
kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2012/2013.
Hata hivyo, maelezo yake ylipingwa na Chama cha Madaktari (MAT),
ambapo kwa niaba yao, Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanataaluma hao, Dk.
Steven Ulimboka, alisema kuwa hawako tayari kupeleka suala hilo katika
Mahakama ya Kazi kama alivyoeleza waziri mkuu.
Alisema ni jambo la aibu kwa viongozi wakuu wa serikali kuamua kwa
makusudi kulidanganya Bunge wakati wakijua wazi hakuna utekelezaji wa
aina yoyote uliofanywa.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa katika madai yote ya madaktari hakuna
dai hata moja ambalo limetekelezwa kama inavyoelezwa na viongozi.
Alisema kitu cha kushangaza hata taarifa ya ufafanuzi wa madai yao hakuna eneo ambalo serikali imeweka saini. “Mgomo huu ni wa madaktari wa ngazi zote nchini ambao hauna kikomo na
tunachohitaji ni kuelezwa na serikali hatua waliyofanya kuliko
wanavyoendesha propaganda na kuweka siasa katika madai yetu,” alisema.
Alisema pamoja na madai yaliyotolewa na madaktari lakini kitu cha
ajabu kilichofanywa na serikali ni kuamua kuchomeka dai la posho ya
uchunguzi wa maiti ambalo halijawahi kutolewa na madaktari. “Serikali inataka kutafuta ionekane imetenda mema kwa madaktari kwa
kudai kupandisha kima cha posho ya uchunguzi wa maiti kutoka sh 10,000
hadi sh 100,000 wakati sisi hatujawahi kuomba posho hiyo,” alisema.
Alisema posho hiyo si muhimu kwa madaktari kwa kuwa wapo baadhi ya
madaktari wanaoweza kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 30 bila kufanya
uchunguzi huo.
Dk. Ulimboka alisema kuwa Watanzania hawapaswi kuwalaumu madaktari kwa
kuwa anayepaswa kubebeshwa lawama hizo ni serikali iliyoshindwa
kuboresha afya pamoja na kutatua migogoro.
Alisema walitegemea kwa siku 90 walizokaa katika meza ya majadiliano
na kamati iliyoundwa na serikali wangepata ufumbuzi wa madai yao,
matokeo yake imekuwa ni matatizo zaidi. “Kuhusu huduma za dharura katika maeneo nyeti watakaa na kutafuta ufumbuzi hapo baadaye,” alisema.