To Chat with me click here

Monday, February 4, 2013

WAFUASI CHADEMA, CCM WAGOMBEA MTI WA BENDERA



SHEREHE za miaka 36 za kuzaliwa kwa CCM jana ziliingia dosari, baada ya kuibuka vurugu kubwa kati ya wafuasi wa chama hicho na Chadema mkoani Dodoma wakati wakigombea eneo na mti wa kutundika bendera za vyama vyao.

Vurugu hizo zilizotulizwa na Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU), zilitokea jana mchana katika uwanja huo uliopo karibu na Baa ya Mwanga, baada ya CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwepo uwanjani hapo, ili waweke bendera zao kwa ajili ya mkutano ambao ulikuwa sehemu ya maadhimisho hayo.

Vurugu zilizuka baada ya wafuasi wa Chadema kuwataka wenzao wa CCM waendelee na mkutano katika eneo hilo kwa sharti la kurejeshwa kwa bendera iliyong’olewa. Wafuasi wa vyama hivyo wakiwamo wabunge wa CCM walionekana wakivutana kunyang’anyana mti wa bendera.

“Baada ya CCM kugoma, Chadema walijaribu kurudisha bendera hiyo kwa nguvu, jambo ambalo lilifanya wafuasi wa CCM waanze kuokota mawe na kuwarushia wapinzani wao hao, huku Chadema nao walianza kujibu mapigo,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.

Baadhi ya wabunge wa CCM walioshiriki katika vurugu hizo na majimbo yao kwenye mabano ni Ismail Aden Rage (Tabora Mjini), Nyambari Nyangwine (Tarime), Seleman Jafo (Kisarawe), Said Mtanda (Mchinga) na Mary Chatanda (Viti Maalumu).

Baadhi ya wafuasi wa CCM walionekana wakibeba mawe na kuwapiga wenzao wa Chadema na kusababisha tafrani kubwa katika eneo hilo la mkutano.


Katibu wa Chadema Wilaya ya Dodoma Mjini, Jellah Mambo alisema kuwa tukio hilo limetokana na wafuasi wa CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwa ikipepea eneo la Mwanga Baa kulikofanyika sherehe za chama chao (CCM).

HOJA YA MBUNGE MWINGINE KUTIKISA BUNGE TENA LEO



Mkutano wa 10 wa Bunge unaendelea leo mjini Dodoma baada ya mapumziko ya mwisho wa wiki na leo itakuwa zamu ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, kuwasilisha hoja binafsi kuhusu hatua za uboreshaji wa upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es Salaam.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya vikao vya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinaeleza kwamba hoja ya Mnyika itakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wabunge hao kwa madai kwamba siyo Jiji la Dar es Salaam pekee lenye tatizo la maji.

Taarifa zaidi zinaeleza kwamba wabunge hao wamejipanga kuizuia hoja hiyo kama walivyofanya hoja ya Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, ambayo ilikuwa ikizungumzia udhaifu ulipo katika sekta ya elimu hasa kutokuwapo kwa mitaala rasmi ya shule za msingi na sekondari.

Wabunge hao wamejipanga kuilazimisha serikali iangalie kwanza tatizo la maji vijijini badala ya Jiji la Dar es Salaam kama Mnyika anavyopendekeza.

Akizungumza na NIPASHE jana, Mnyika alisema Ijumaa aliwasilisha kwa Katibu wa Bunge mapendekezo ya kuboresha na kupanua wigo wa hoja yake pamoja na hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji jijini Dar es Salaam.

Alisema katika mapendekezo hayo, hoja yake imejielekeza katika  kuboresha utekelezaji wa miradi ya maji nchi nzima kwa kuingiza masuala muhimu kuhusu Programu ya Maji Safi na Mazingira Vijijini (RWSSP) maarufu kama mradi wa vijiji kumi ambao unatekelezwa katika Halmashauri za Dar es Salaam na wilaya zote nchini.

“Nimeeleza kuwa Programu ya Maji Safi na Mazingira Vijijini ikiwamo katika Manispaa za Jiji la Dar es Salaam ilipaswa kutekelezwa kuanzia mwaka 2005/2006 na kukamilika mwaka 2010/2011 kwa kugharimu dola za Marekani milioni 292 (zaidi ya Sh. bilioni 438).  Hata hivyo, tathmini ya miaka miwili na nusu ya utekelezaji imebainisha kasoro nyingi katika utekelezaji,” alisema.

Alisema: “Nitawasilisha bungeni hatua zipi za haraka ambazo napendekeza zichukuliwe ikiwamo kuhusu ufisadi katika sekta ya maji kwenye Jiji la Dar es Salaam na nchini kwa ujumla.”

Alisema mabadiliko aliyofanya yanalenga pamoja na mambo mengine, kuifanya iguse matukio ya karibuni kuhusu tatizo la maji nchini.

Kabla ya Mnyika kuwasilisha hoja yake, wabunge wataendelea na mjadala wa hoja ya Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Hamis Kigwangalla, ya kuitaka serikali ianzishe mfuko maalum wa kukuza ajira kwa vijana kwa kuanzisha mfuko wa mikopo wa vyama vinavyowekeza katika kilimo na viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja na kilimo.

Hoja ya Kigwangalla iliwasilishwa bungeni Ijumaa iliyopita na kujadiliwa na baadhi ya wabunge, lakini leo wengine zaidi watapata nafasi ya kuchangia kabla ya mbunge huyo kupewa nafasi ya kuhitimisha.

Hoja ya Mnyika ambayo itafuatiwa na ya Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, ambaye kesho atawasilisha hoja binafsi kuhusu mwenendo wa Baraza la Mitihani la Taifa unavyoathiri elimu nchini.

Mbali ya hoja hizo, Bunge pia litajadili maazimio ya mikataba mbalimbali ya Kimataifa pamoja na miswada ya sheria itakayowasilishwa na serikali.

Hoja ya Mnyika huenda ikageuzwa kama ilivyofanywa na Mbatia baada ya wabunge wa CCM kutoiunga mkono. Hatari ya hoja kutoungwa mkono na wabunge wa CCM ni kura za ndiyo na siyo ambazo zinakwamisha hoja hata kama zina nguvu.

Katika hoja yake, Mbatia aliliomba Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza udhaifu uliopo kwenye sekta ya elimu hasa kutokuwepo kwa mitaala rasmi.

Hoja hiyo ilipingwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, ambaye alipinga kamati akieleza kwamba tayari serikali imechukua hatua nyingi za kuitekeleza elimu kwa kujenga madarasa mengi na idadi ya wanafunzi wanaojiunga elimu ya msingi na sekondari imekuwa ikiongezeka kila mwaka.
Waziri Kawambwa aliahidi kwamba atawasilisha miswada hiyo bungeni Februari 6, kabla Mkutano huu haujamalizika.

Baadhi ya wabunge waliochangia hoja ya Dk. Kigwangalla wameonyesha wasiwasi wa zitakakopatikana fedha za kuweka kwenye mfuko wa kukopesha vijana na badala yake wamependekeza mfumo mzima wa elimu uboreshwe ili nchi izalishe wahitimu wanaoweza kujiajiri na kushindana kwenye soko la ajira.
Kwa mujibu wa ratiba, Mkutano wa Kumi wa Bunge unatarajiwa kuahirishwa Februari 8, mwaka huu.

CHANZO: NIPASHE

AHADI ZAWA MWIBA KWA JK


AHADI za ujenzi wa barabara za lami zilizopata kutolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati akiomba kura mwaka 2010, zimezua balaa na kuibua mzozo bungeni.

Hali hiyo ilitokana na swali la Mbunge wa Buhambwe, Felix Mkosamali (NCCR- Mageuzi), kuhoji utekelezaji wa ahadi ya Rais Kikwete ya kujenga barabara ya Nyakanazi-Kibondo-Kigoma katika kiwango cha lami.

Pia alihoji ahadi ya Rais Kikwete ya ujenzi wa barabara ya Kibondo Mjini yenye urefu wa kilomita 1.5 na ujenzi wa barabara ya kimataifa ya kutoka Kibondo –Mabamba mpaka wa Burundi.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge alisema serikali bado iko mbioni kutekeleza ahadi hizo kutegemea na upatikanaji wa fedha. Alisema ahadi za rais zitatekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha kwani mwisho wa ahadi zake ni mwaka 2015.

Kutokana na majibu hayo, Mkosamali aliuliza swali la nyongeza na kutumia maneno yaliyotafsiriwa kama ni kashfa kwa Rais Kikwete. “Mhesmiwa Naibu Spika, sikubaliani na majibu mepesi ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Hivi unataka kusema ahadi za Rais Kikwete kujenga barabara ya Kibondo ilikuwa ya uongo? Ina maana alisema uongo ili kupata sifa ya kuchaguliwa kuwa rais?”

Swali hilo la nyongeza ambalo hata hivyo lilijibiwa vizuri na Naibu Waziri wa Ujenzi, lilimkera Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi ambaye alisimama na kuomba mwongozo wa spika akipinga lugha iliyotumiwa na Mkosamali dhidi ya Rais Kikwete.

“Mheshimiwa Naibu Spika, mbunge aliyeuliza swali la msingi kuhusu ahadi za rais, wakati akiuliza swali la nyongeza, alitumia maneno makali dhidi ya rais kinyume cha kanuni za Bunge. “Anasema rais alisema uongo au alisema uongo ili achaguliwe, sio maneno ya kistaarabu kutumika hasa kwa rais.

“Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni ya 61 (2) inasema mbunge hatatumia kumdhihaki rais au kulishawishi Bunge kuamua jambo fulani dhidi ya rais.

“Nimesimama sio kutaka aombe radhi, bali kuwakumbusha vijana wawe makini na matumizi ya lugha, hasa lugha ya kuudhi. Mwongozo wangu ni kutaka uwakumbushe wabunge matumizi mazuri ya lugha, ni hilo tu,” alisema na kuketi.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) ambaye ni mnadhimu kambi ya upinzani bungeni, kwanza alimtaka Waziri Lukuvi afute kauli yake kwamba kuna vijana kwa madai kuwa ndani ya Bunge hakuna vijana.

”Pili, Waziri Lukuvi amemwelewa vibaya mbunge maana hajasema rais muongo. Alitaka kujua kama ahadi ya rais ni ya uongo. Na tatu mbunge hakutaka kushawishi Bunge kuchukua hatua dhidi ya rais,” alisema Lissu.

David Kafulila, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), naye alisimama na kuongeza kuwa waziri amepotosha umma na huo ni uchochezi. Mkosamali naye alisimama na kusema kuwa hajamtukana rais bali alitaka kujua kama ahadi hiyo ni ya uongo au la.

Akitoa mwongozo wake, Naibu Spika aliwataka wabunge kutumia lugha ya kistaarabu. Mbali ya swali la Mkosamali, wabunge wengine waliohoji ahadi ya ujenzi wa barabara katika maeneo yao ni Ester Bulaya (Viti Maalumu), Paul Rwanji (Manyoni Magharibi), wote CCM na Said Arfi wa Mpanda Kati (CHADEMA), ambao nao waliohoji ahadi za Rais Kikwete za ujenzi wa barabara katika maeneo yao.

Friday, February 1, 2013

TUNDA LA STAFELI LINATIBU SARATANI


TUNDA la stafeli linatibu magonjwa kadhaa, ikiwamo saratani kwa ubora wa karibu mara 10,000 ya matibabu ya kawaida yanayopatikana kwenye vituo vya afya, utafiti umebaini.

Utafiti huo uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dawa cha Purdue nchini Marekani, umeeleza kuwa mbali na kutibu saratani, tunda hilo pia ni tiba ya matatizo ya msongo na mfadhaiko.

“Maajabu ya stafeli ni kwamba lina uwezo wa kuangamiza chembehai zenye saratani pasipo kusababisha madhara katika mwili kama zinavyofanya dawa nyingine za ugonjwa huo au mionzi,” imesema sehemu ya utafiti huo uliochapishwa kwa mara ya kwanza katika Jarida la Kemia na Madawa la nchini Marekani, mwaka 2010.

Taasisi ya  utafiti  wa Saratani ya Nchini Uingereza(NIR) ilifanya  utafiti wa kwanza kuhusu maajabu ya stafeli mwaka 1976.

Katika utafiti huo ilibainika kuwa majani, mizizi na tunda la stafeli, vina uwezo wa kutibu saratani, lakini matokeo ya utafiti huo hayakutangazwa kwa umma kwa hofu ya kuua viwanda vya dawa za saratani.

Inaelezwa kuwa kirutubisho kilichopo katika stafeli kinatumia  jina la kibiashara la ‘Triamazon’  na kimepigwa marufuku kutumika nchini Uingereza na Marekani  kutokana na uwezo wake mkubwa wa kitiba.

Utafiti mwingine uliofanywa na Chuo Kikuu cha Kikatoliki nchini Korea na kuchapishwa katika jarida la Bidhaa Asilia  ulibaini kuwa stafeli lina uwezo wa kuponya saratani ya tumbo.



Utafiti wa chuo hicho ulienda mbali na kusema kuwa tunda hilo linaweza kulenga seli za saratani tu, bila kushambulia seli muhimu za mwili kama ambavyo tiba ya mionzi ifanyavyo.

Tunda la Stafeli lina kirutubisho muhimu kiitwacho Annona Muricata, ambacho ndicho chenye uwezo wa kupigana na maradhi ya saratani. Imeelezwa kuwa stafeli lina uwezo wa kutibu aina 12 za saratani ikiwemo ya matiti, kongosho, mapafu na ya kibofu cha mkojo.

Pamoja na kutibu saratani, kirutubisho hicho kilichopo katika tunda hilo pia huweza kutibu vimelea, shinikizo la damu, msongo wa mawazo, matatizo ya mfumo wa fahamu na sukari.

Utafiti  huo unaonyesha kuwa kirutubisho kimegwacho katika tunda hilo   kinaweza  kwa asilimia kubwa kupambana na saratani bila kumuacha mgonjwa na madhara kama kusikia kichefuchefu, kutapika, kupungua uzito na kunyonyoka nywele.

Aidha huweza kuupa mwili kinga na kukupa nguvu  bila madhara yasababishwayo na dawa nyingine. Tangu mwaka 1976, tunda hilo liliendelea kufanyiwa utafiti  katika maabara binafsi  zaidi ya 20duniani.

Stafeli nini?
Stafeli ni tunda la chanikiwiti ambalo linastawi zaidi katika ukanda wa kitropiki. Mti wa tunda hilo ni mfupi wa wastani, Wabrazili wanauita Graviola na Waingereza wanaliita Soursop. Hapa Tanzani stafeli linajulikana kwa jina jingine la topetope.

MUHOGO UNAFAIDA NYINGI ZAIDI TUNAVYOFIKIRI


Zao la Muhogo mkombozi wa Mwananchi Tanzania
Zao la muhogo linalimwa karibu katika mikoa yote nchini. Karibu asilimia 48.8 ya zao hilo linalimwa ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi.  Asilimia 23.7 inalimwa katika mikoa inayozunguka ukanda wa Ziwa Victoria, asilimia 13.7 inalimwa katika ukanda wa Ziwa Nyasa, na asilimia 7.9 inalimwa ukanda wa Ziwa Tanganyika.

Uwiano huo wa kuzalisha muhogo umekuwa ukipanda na kushuka kulingana na sababu mbalimbali. Katika maeneo hayo yote, zao la muhogo ni chakula muhimu kikifuatiwa na mahindi, mtama, uwele, mchele au ndizi, na viazi vitamu katika baadhi ya maeneo nchini.

Zao la muhogo lina uwezo wa kulifanya baa la njaa nchini kuwa historia. Zao hilo muhimu pia lina uwezo mkubwa wa kutokomeza umaskini uliokithiri vijijini ambako wakulima wadogo wanaishi kwa pato dogo yaani chini ya dola moja kwa siku (dola ya Marekani).

Muhogo ni zao ambalo lina soko kubwa la nje, tofauti na wengi wanavyofikiria.
Endapo muhogo utafanywa kuwa zao rasmi la biashara, kutaongeza hamasa kwa wakulima wa zao hilo, na hatimaye kunufaika.

Kuna mambokaribu kumi ambayo ambayo lazima yazingatiwe ili kufanikisha azma ya kusababisha muhogo kuwa zao la biashara kama mazao mengine.

Kwanza, lipo suala la kuzalisha mbegu za kisasa za muhogo, ambazo zitatoa mavuno mengi zaidi kuliko mbegu za jadi na kujenga mtandao imara wa kusambaza mbegu kwa wakulima kote nchini bila ukiritimba na mizengwe isiyokuwa na lazima.

Katika mpango huo  uzalishaji wa mbegu au vishina bora unapaswa  ufanyike katika vituo mbalimbali vya utafiti wa zao hilo katika maeneo mbalimbali nchini na kusambazwa kwa wakulima.

Pia wakulima wanapaswa kupewa mafunzo kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuzalisha vishina hivyo.

Baadhi ya vituo hivyo ni Naliendele (ARI) mkoani Mtwara, Kibaha (ARI) Mkoa wa Pwani, Ukiliguru (ARI) Mkoa wa Mwanza, Maruku (ARI) Mkoa wa Kagera, Uyole (ARI) Mkoa wa Mbeya, Hombolo (ARI) Mkoa wa Dodoma, Tumbi (ARI) Mkoa wa Tabora, Tengeru (ARI) Mkoa wa Arusha,  na Kizimbani (ARI) Unguja visiwani.

Wakulima wanapaswa kupewa mafunzo ya kutosha katika kukabiliana na waadudu wanaoshambulia zao la muhogo pamoja na pembejeo nyingine.

Jitihada za kuimarisha kilimo cha muhogo ziende sanjari na utengenezaji wa mashine maalum za kusindika muhogo kwa njia za kisasa na kuzalisha unga wa muhogo wenye ubora wa hali ya juu (HQCF) ambao una soko kubwa hapa nchini na nje ya nchi.

Hivi sasa, kuna kiwanda au karakana moja tu nchini, mjini Morogoro yenye uwezo wa kufanya kazi hiyo. Hili ni jambo la aibu.

Karakana za aina hiyo ni muhimu ziwepo katika kila mkoa, na ikibidi katika kila wilaya. Ni teknolojia rahisi ya kisasa na yenye gharama nafuu .

Jaribio la kwanza la matumizi ya mashine hizo za teknolojia ya kisasa ya kusindika muhogo ili kupata unga bora (HQCF) , lilifanyika miaka 17 iliyopita (1997/98) katika Kituo cha Utafiti cha Naliendele Mtwara , katika vijiji vinne vya majaribio vya Makukwe, Nakahako, Mumbaka, na Mkarango, mkoani Mtwara.

ZITTO AMSHUKIA JK


AMTAKA ASITUMIE MALI ZA SERIKALI KWA KAZI ZA CCM


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kuacha kutumia mali za serikali kwa ajili ya kufanya shughuli za Chama chake cha Mapinduzi (CCM).

Angalizo hilo la Zitto limekuja wakati Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, akitarajiwa kuwasili mkoani Kigoma wakati wowote kwa ajili ya sherehe za maadhimisho ya miaka 36 ya chama hicho.

Rais pia atatumia nafasi hiyo kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali kuu na halmashauri.

Akihutubia mkutano wa hadhara jana mjini hapa, Zitto alimtaka Rais Kikwete kama anakuja kwenye shughuli za CCM aje kwa gharama za chama chake na si kwa gharama za serikali.

“Rais anakuja kwenye shughuli za CCM, ndege atakayopanda ni ya serikali. Tunasema kama unakuja kwenye shughuli za CCM njoo kwa gharama za CCM,” alisema.

Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, aliongeza kuwa Rais Kikwete asichanganye kazi za CCM na kazi za serikali na kuongeza kuwa hana kinyongo naye kwa kuwa vitu alivyofanya mkoa wa Kigoma vinaonekana kulinganisha na marais waliotangulia.

“Sisi hatuna kinyongo naye, maanake Nyerere alipita hakuna kitu, Mwinyi amepita hamna kitu, Mkapa alipita hamna, yeye kaja kuna vitu tumeviona, hatuna kinyongo naye lakini asije kwa gharama za serikali kwa mambo ya CCM, asichanganye kwa kuwa si utawala bora.

“Haiwezekani miradi ya maendeleo ya halmashauri kama ile stendi ya mabasi ya daladala ya kituo cha stesheni, ni mradi wa halmashauri, Rais anakuja kuzindua hatukatai lakini kama anakuja kwa shughuli za CCM amalize mambo yao kwanza arudi Dar es Salaam halafu aje kiserikali atufungulie miradi,” alisema.

Aliwataka madiwani wa CHADEMA kutotoa ushirikiano kama Rais anakuja kwa shughuli za CCM kufungua miradi ya maendeleo kwa sababu itakuwa ni propaganda ya CCM.

“Hatuwezi kuruhusu mkuu wa nchi kutumia fedha za nchi kufanya kazi ya CCM na usalama wa taifa mlioko hapa mpeleke taarifa,” aling’aka.

Katika hatua nyingine Zitto pia amemtaka mkuu wa mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali mstaafu Issa Mchibya asiende kukagua miradi ya maendeleo akiwa na katibu wa CCM kwa gari la serikali na kwamba kuanzia leo wataanza kufanya ufuatiliaji.

SAKATA LA GESI MTWARA: MBOWE AMBANA PINDA


KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amembana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akitaka serikali iwachukulie hatua watendaji waliozembea kudhibiti vurugu za mzozo wa gesi Mtwara.

Mbowe pia alimhenyesha Pinda akimtaka alihakikishie Bunge ni lini serikali itakuwa tayari kuweka wazi mikataba kadhaa ikiwamo ya mafuta na gesi asili ili kuondoa upotoshaji wa miradi hiyo kama ilivyotokea Mtwara.

Akiuliza swali hilo bungeni jana mjini hapa, Mbowe alisema kwa kuwa vurugu hizo zimetokana na uzembe wa kisiasa na viongozi wakiwamo wa vyombo vya dola kushindwa kubaini na kudhibiti ghasia hizo mapema, kwanini wasichukuliwe hatua kwa uzembe huo.

Akijibu maswali hayo, Pinda alirejea kauli yake ya mara kwa mara tangu alipotoka kusuluhisha mzozo huo Mtwara, akisema vyama vya siasa vimechangia sana kukuza na kupotosha ukweli wa mradi huo.

Alisema wanasiasa walitumia mzozo huo kujiimarisha kisiasa na kujijenga kwa ajili ya uchaguzi unaokuja. "Suala la kuwawajibisha watendaji hao liko chini ya waziri mkuu na rais, tutaliangalia,” alisema Pinda.

Hata hivyo, Pinda alisema jambo la msingi si kutafuta mchawi, kwani tatizo la Mtwara ni la wote, na siku zijazo kutakuwa na ushirikishwaji wa jamii katika kutoa elimu ili kuepuka madhara kama yaliyotokea Mtwara.

Kuhusu kuweka wazi mikataba ili kuondoa upotoshaji, Pinda alisema mikataba hiyo haina siri na inaweza kuwekwa wazi kupitia mifumo ya kibunge.

Hata hivyo, Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hakuridhika na majibu hayo na katika maswali yake ya nyongeza alimtaka waziri mkuu kutamka wazi bila kumng’unya maneno kama serikali iko tayari kuweka mikataba hiyo wazi.

Pia alihoji ni kwa nini serikali iko tayari kutekeleza kero za wananchi pale inapobanwa kwa presha na maandamano kama ilivyotokea Mtwara.

Katika hoja hiyo, Pinda alisema serikali haiko tayari kuweka wazi mikataba hiyo kupitia magazeti, kwani mingine ina taratibu zake lakini iko tayari kuweka wazi kupitia mifumo ya kibunge.

Kuhusu serikali kusikiliza kero za wananchi baada ya presha za maandamano, Pinda alisema maandamano si njia sahihi ya kuwasilisha madai ya wananchi. "Ndugu yangu Mbowe anajaribu kuleta hoja ambayo haina mashiko. Mimi siamini kuwa maandamano ndiyo njia sahihi ya kuwasilisha malalamiko ya wananchi,” alisema Pinda.

Mapema kabla ya maswali kwake, Pinda alitoa taarifa ya kueleza kuhusu vurugu za Mtwara pamoja na madhara yaliyojitokeza, ambapo hata hivyo alirudia kile alichowaeleza waandishi wa habari juzi.

Alisema kulikuwa na upotoshaji mkubwa kwamba bomba hilo la gesi lingeishia Bagamoyo ambako inajengwa bandari ya kusafirishia gesi hiyo nje na kumhusisha Rais Jakaya Kikwete, jambo ambalo si la kweli kabisa.

Waziri Mkuu Pinda aliwatangazia wabunge uharibifu wa mali na hasara iliyopatikana kutokana na vurugu hizo, sambamba na kuorodhesha majina ya watu waliochomewa nyumba, magari na mali nyingine.

Pia alitaja majengo na ofisi za serikali zilizochomwa moto pamoja na magari, ambapo uharibifu huo umesababisha hasara ya mabilioni ya fedha, akisema serikali itaangalia namna ya kuwafidia.