To Chat with me click here

Friday, July 26, 2013

JK: TUTAMNYUKA ATAKAYETUCHEZEA!



RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali ya Tanzania iko tayari kukabiliana na mtu yeyote atakayejaribu kuichezea au kuichokoza kwa namna yoyote ile, ikiwamo kumega ardhi yake, itamfundisha kama ilivyomfundisha aliyekuwa Rais wa Uganda, Idd Amin Dada, katika Vita ya Kagera.

Kikwete alisema serikali ilimshikisha adabu Amin alipojaribu kumega sehemu ya ardhi ya Tanzania, hivyo haitosita kufanya hivyo tena kwa asiye na nia njema na Tanzania.

Kiongozi huyo mkuu wa nchi alitoa onyo hilo jana wakati akizungumza na wananchi katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa yaliyofanyika kitaifa katika makaburi yaliyopo Kambi ya Kaboya, wilayani Muleba, mkoani Kagera.

Rais Kikwete alisema serikali iko tayari kukabiliana na kupambana kwa nguvu yoyote ile bila kuogopa mtu anayejaribu kuichezea nchi ya Tanzania kwa lengo la kukwaza amani na utulivu uliopo hivi sasa.

“Laleni usingizi salama. Msisikilize maneno ya mitaani, kwa sababu jeshi letu liko imara kabisa kulinda nchi yetu na mipaka yake. Yeyote atakayejaribu kuivamia ama kuichokoza nchi yetu atakiona cha mtema kuni. Nchi iko salama na jeshi liko imara kulinda nchi yetu.

“Ujumbe wetu mkubwa wa leo ni kwamba tuko tayari wakati wote na saa yoyote kuilinda nchi yetu na mipaka yake. Hatuna nchi nyingine. Hivyo, kamwe hatuwezi kumruhusu yeyote kuichezea nchi yetu, ama kuichezea ama kuimega nchi hii. Kama tulivyoshughulika na Amin naye tutashughulika naye vivyo hivyo,” alisema.

Rais Kikwete alisema shughuli ya kulinda amani ni ghali. “Na moja ya gharama hizo ni makaburi haya ya ndugu zetu ambao wamelala hapa baada ya kupoteza maisha yao katika vita dhidi ya nduli Idi Amin. Tutaendelea kuwaenzi kwa sababu hawa walijitolea maisha yao kulinda mipaka ya nchi yetu, kulinda amani ya nchi yetu na usalama wake na wetu sote,” alisema Kikwete.

Kiasi cha askari 619 waliopoteza maisha yao wamelazwa kwenye makaburi hayo ya Kaboya.

Rais Kikwete amesema kuwa serikali yake kwa ushauri wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania inaangalia jinsi gani ya kuwahudumia vizuri zaidi askari wa Tanzania ambao walipata vilema katika vita hiyo na bado wanaendelea kuishi.

“Nimesikia kuna malalamiko kuhusu ubora wa jinsi tunavyowahudumia, hivyo tutazungumza na Jeshi kuhusu njia bora zaidi ya jinsi ya kuwahudumia. Hawa ni mashujaa wetu, ni watu waliojitolea maisha yao kuweza kulinda uhuru wetu. Tunaendelea kuwashukuru na kuwaenzi. Hii ndiyo sababu sherehe za leo ni sherehe kubwa kwa nchi yetu,” alisema.

Rais Kikwete alishuhudia sherehe za kumbukumbu hizo ambapo miongoni mwa mambo mengine, ametembelea makaburi ya askari wa Tanzania waliopoteza maisha yao wakati wa kuikomboa nchi kutokana na uvamizi wa Amin wa Uganda na kuona silaha zilizotumika katika vita hiyo mwaka 1978/79.
Naye Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ ), Davis Mwamunyange, alisema jeshi lake liko makini na lina uwezo mkubwa wa kupambana dhidi ya wale wanaotaka kuivunja amani iliyopo.

Alisema uwepo wa amani na utulivu nchini umechangia watu washiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo pasipo kuhofia chochote, hivyo anayetaka kuivuruga JWTZ haitamuachia wala kumuonea huruma.

Mwamunyange alisema JWTZ wako mstari wa mbele kuwalinda na kuwatetea kwa hali na mali wananchi wa Tanzania ili kuhakikisha wanakuwa katika hali ya utulivu na amani.

Naye Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mehtodius Kilaini, alisema ni wajibu wa viongozi wa dini na serikali kutambua wajibu wao katika kutenda haki na kutetea wananchi.

Askofu Kilaini alisema hayo wakati akiongoza sala ya kuwaombea mashujaa 619 waliouawa katika vita ya Kagera kati ya mwaka 1978 na 1979 wakitetea taifa lao.
Alisema ushindi wa nchi unatokana na umoja, mshikamano na uvumilivu baina ya viongozi na wananchi wanaoungana kutetea masilahi ya taifa lao kutoka kwa adui.

Aliongeza kuwa ili nchi iendelee pamoja na kustawi vizuri kwa jamii yake, amani ni msingi mkubwa unaopaswa kuzingatiwa.

Askofu Kilaini aliwataka viongozi wa dini na serikali kuhubiri amani pamoja na kutekeleza wajibu wa majukumu yao kwa wakati na kufuata utaratibu ulio sahihi kwa wananchi wake.

No comments:

Post a Comment