UAMUZI
wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukataa
kuwasilisha ushahidi wa mauji ya mlipuko wa bomu uliotokea jijini Arusha,
umeliweka njia panda Jeshi la Polisi na hivyo kushindwa kuchukua hatua.
Licha
ya jeshi hilo kumhoji Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, na kumtaka
awasilishe ushahidi huo, kiongozi huyo amekataa agizo hilo akisema kuwa
wamekubaliana kuutoa ushahidi huo kwa tume huru ya majaji endapo Rais Jakaya
Kikwete ataiunda kama walivyomuomba.
Chanzo
chetu ndani ya jeshi hilo, kimedokeza kuwa msimamo huo wa CHADEMA umeliweka
njia panda na hivyo kushindwa kuchukua hatua za kuwabaini watuhumiwa wa tukio
hilo na kuwafungulia mashtaka kutokana na mkanganyiko wa taarifa zinazotolewa.
Jeshi
hilo linadaiwa kuwa awali lilitaka kujiegemeza kwenye kauli za kisiasa za
baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikali ili kuonyesha kuwa
CHADEMA ilisababisha mlipuko huo yenyewe kwa ajili ya kuwahadaa wafuasi na
kujitafutia umaarufu.
Hata
hivyo, mbinu hiyo ya kutaka kuwasakama baadhi ya viongozi na wafuasi wa CHADEMA
inadaiwa kufifishwa na tamko la Mbowe pamoja na mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema, kwamba chama kina ushahidi unaoonyesha kuwa tukio hilo
lilifanywa na polisi.
“Hapa
kuna mkanganyiko hasa baada ya Mbowe kudai wanao ushahidi wa video ya tukio
hilo. Wakubwa wetu wamegawanyika na kujikuta wakitoa kauli za kukinzana maana
wanahofia wakiwafungulia kesi watu wengine mashtaka halafu CHADEMA ikaonyesha
ushahidi tofauti itakuwa ni aibu,” kilisema chanzo chetu.
Kwa
mujibu wa chanzo hicho, jeshi hilo mkoani Arusha lilikuwa limewakamata watu
wawili raia wa kigeni likiwatuhumu kuhusika na mlipuko huo lakini baada ya
Mbowe kugoma kupeleka ushahidi huo, watuhumiwa hao hawakuweza kufunguliwa
mashtaka.
Pia
katika hali ya kushangaza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alikaririwa
na baadhi ya vyombo vya habari kuwa makachero wa Taasisi ya Uchunguzi ya
Marekani (FBI) wamefika mkoani Arusha kuchunguza jambo hilo.
Hata
hivyo taarifa kutoka ubalozi wa Marekani zilikana FBI kuingia nchini kuchunguza
jambo hilo hivyo kusababisha mkanganyiko wa tukio hilo lililovuta hisia kubwa
ndani na nje ya nchi.
CHADEMA
mara kwa mara imekuwa ikilituhumu jeshi la polisi na makada wa CCM kuendesha
harakati za kukidhoofisha kwa kutumia matukio mbalimbali yanayofanywa na chama
hicho cha upinzani.
Mmoja
wa viongozi wa CHADEMA aliviambia vyanzo vyetu vya habari, kuwa polisi walikuwa
wamepanga kuwatumia FBI kuuhabarisha umma kuwa CHADEMA ilihusika na ulipuaji
huo bomu lakini kutokana na mazingira yaliyopo wameshindwa kutekeleza uovu huo.
“Unajua
hila za polisi na CCM kila siku zinabadilika lakini kwa bahati mbaya hawajui
kuwa wananchi wanajua kinachofanyika, kuna askari hawaridhiki na uovu
unaofanywa na wenzao,” alisema kiongozi huyo.
Hata
hivyo Senso hakuwa tayari kulizungumzia akisema kuwa alikuwa eneo baya na
akitoka eneo hilo angelijulisha gazeti hili lakini mpaka tunakwenda mitamboni
hakutimiza ahadi hiyo.
Mlipuko
huo ambao ulisababisha vifo vya watu wanne na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa,
ulitokea Juni 15 mwaka huu wakati wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa
madiwani jijini humo, zikiwa zimepita dakika chache baada ya Mbowe kumaliza
kuhutubia na kutelemka katika jukwaa lililokokuwa limeelekezwa bomu hilo.
Siku
moja baada ya tukio hilo, serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ilitoa taarifa tata bungeni
ikionyesha kulikingia kifua jeshi la polisi na kuwatwisha lawama viongozi wa
CHADEMA.
Lukuvi
alisema kuwa mkutano wa CHADEMA ulikuwa na ulinzi wa polisi wenye magari mawili
waliosimama upande wa kaskazini ya uwanja na mrushaji wa mlipuko huo akiwa
upande wa mashariki ya uwanja huo na kurusha kuelekea magharibi.
“Jaribio
la askari kutaka kumfuata aliyerusha mlipuko huo zilizuiliwa na makundi ya wananchi
ambao walianza kuwashambulia askari kwa mawe na kuwazomea na hivyo polisi
kulazimika kuanza kujiokoa badala ya kumsaka mhalifu huyo.
“Hivi
karibuni zimekuwepo jitihada za makusudi za baadhi ya vyama vya siasa, makundi
ya kijamii na watu binafsi kupandikiza chuki ya raia dhidi ya vijana wetu wa
polisi, kuwafanya raia wawachukie, wasiwaamini, wasiwape ushirikiano na
kuifanya nchi isitawalike,” alisema Lukuvi.
Aliliongeza
kuwa kufanikiwa kutoroka kwa mhalifu wa tukio hilo ni matokeo ya uchochezi
unaofanywa kwa makusudi na baadhi ya wanasiasa dhidi ya serikali na polisi na
hivyo kuwafanya wananchi wajenge chuki dhidi ya polisi.
Siku
chache baadaye viongozi wa CCM pamoja na baadhi ya mawaziri kana kwamba
wanafahamu mlipuaji wa bomu hilo, waliitwisha lawama CHADEMA wakidai ilihusika
na tukio hilo ingawa hadi leo hakuna aliyehojiwa na polisi kati yao
kuthibitisha tuhuma hizo badala yake Mbowe pekee ndiye anaandamwa awapelekee
ushahidi.
Makada
hao ni Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Mwigulu Nchemba, na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa
Ghasia, ambao walidai kuwa CHADEMA ndiyo imekuwa ikihusika na vurugu zote
zinazohusisha mauaji nchini.
Kauli
za viongozi hao zilitplewa baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama
cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kudai kuwa wanao ushahidi
wa kutosha kuwa CHADEMA iliandaa na kuratibu shambulio hilo.
“Ni
lazima tuwaze na kuvuka mipaka, kuna mambo ambayo yanawezekana kabisa yakawa
yamejificha pale. Watu wanaangalia, wanaojitoa ufahamu wanafikiria CCM inaweza
kushiriki.
“Mimi
niwaambie CCM hata bila kushiriki ni moja kwa moja inawekwa kwenye lawama jambo
kama hilo likitokea. Ila CCM haina ushiriki katika jambo kama hili kwa sababu
ndio watu wake kupitia serikali yake wanatakiwa kuwahakikishia usalama,”
alisema.
Mwigulu
ambaye pia ni mbunge wa Iramba Magharibi aliongeza kuwa hata video ya mauji ya
Arusha iliyowekwa kwenye mtando wa You tube inaonesha wazi kuwa yalipangwa.
“Yule
aliyekuwa anachukua video eti hakushtushwa kabisa na lile bomu, aliendelea
kufuatilia kama vile ni mkanda wa harusi. Iliwahi kutokea wapi mchukua video
kwenye mkutano wa hadhara kitu ambacho hakikupangwa kimelipuka, kinaua watu,
yeye anendelea kama anachukua send off?” alihoji.
Ghasia
naye alidai kuwa CHADEMA wamechochea vurugu Mtwara, Mwanza, Mbeya, Morogoro na
sasa Arusha ili maeneo hayo yasipate maendeleo.
Kutokana
na mlipuko huo, CHADEMA ilitangaza kuanza mpango wa kutoa mafunzo kwa vijana
wake kwa ajili ya kulinda mikutano na viongozi wake lakini CCM, polisi na
Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, walikionya chama hicho wakidai kuwa
hatua hiyo ni kinyume cha sheria za nchi, Katiba na sheria ya vyama vya siasa
ya mwaka 1992.
Hata
hivyo hoja zao zilipingwa vikali na baadhi ya wadau wa siasa na wananchi
wakihoji walikuwa wapi kwa kutoionya CCM ambayo ina kikundi cha vijana cha
Green Guard ambacho kinapewa mafunzo ya kijeshi na matumizi ya silaha za moto.
Julai
17 mwaka huu, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, alimwandikia
Mbowe barua na kumwamuru awasilishe ushahidi wa video aliyodai kuwa nayo
ikiwaonesha baadhi yao walivyoshiriki kwenye tukio la mlipuko wa bomu Arusha
kabla ya Julai 23 mchana saa nane.
Katika
hatua ya kuchanganyana, jeshi hilo Juni 20 mwaka huu, kupitia kwa Mkuu wa
Mafunzo na Operesheni, Paul Chagonja, aliwaeleza wanahabari kuwa Mbowe anapaswa
kuwa mkweli na kuacha kuuchezea umma kwa alichowaeleza polisi ni tofauti kwani
hana ushahidi huo.
Lakini
katika hatua ya kushangaza Chagonja huyo huyo ndiye amemwamuru Mbowe kupeleka
tena ushahidi huo polisi akitamba kuwa baada ya kukaidi kufanya hivyo, polisi
inao makachero wake wanaojua jinsi gani ya kuendelea na kazi hiyo.
Pamoja
na polisi kudai Mbowe hana ushahidi, Julai 10 mwaka huu usiku wa manane askari kadhaa
wakiwa na silaha walifika nyumbani kwake wamkisaka bila mafanikio wakitaka
awapatie video hiyo.
Hata
hivyo, kesho yake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alidai
hana taarifa za askari wake kufika nyumbani kwa Mbowe.
Muda
aliopewa Mbowe umemalizika bila kuwasilisha ushahidi huo, akidai kuwa hawezi
kwenda kinyume na msimamo wa chama kwani jeshi hilo ni watuhumiwa kwenye tukio
hilo la Arusha.
Juzi
jeshi hilo lilimtaka Mbowe kuwasilisha msimamo huo wa utetezi wake kwa
maandishi leo ambapo kiongozi huyo wa upinzani alisema mwanasheria wa chama
hicho ataandaa maelezo hayo.
No comments:
Post a Comment