Mhe. John Mnyika |
YASADIKIKA
KUWA LILIRUSHWA NA POLISI ALIPOSIMAMA
VITUKO
na matukio ya hatari kwenye mikutano ya CHADEMA vimeendelea kushika kasi. Jana
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alinusurika kupigwa na bomu la machozi
lililorushwa na polisi waliokuwa wakizuia kufanyika mkutano ulioitishwa na
chama hicho.
Tukio
hilo lilitokea katika eneo la Mabibo kwenye viwanja vya Sahara ambapo bomu hilo
lilimpata mtu aliyekuwa karibu na Mnyika anayeitwa Thomas Jerome, aliyejeruhiwa
sehemu ya paja.
Baada
ya kurushwa kwa bomu hilo, polisi walitaka kumchukua majeruhi huyo ili wamweke
kwenye gari lao apelekwe hospitalini, lakini Mnyika aliwaelekeza wafuasi wa
CHADEMA kumchukua kwa madai kitendo kilichofanywa na askari hao kililenga
kuficha ushahidi wa jambo hilo.
Polisi
waliokuwemo eneo la tukio waliamua kukubaliana na matakwa ya wafuasi wa CHADEMA
waliomchukua Jerome na kumpeleka hospitali ambako hali yake inadaiwa inaendelea
vizuri.
Akielezea
hali ilivyokuwa akiwa katika mkutano mwingine uliofanyika Ubungo, Mnyika
alisema polisi walifika katika viwanja vya Sahara wakiwa na magari matatu kwa
lengo la kutawanya wafuasi wa CHADEMA wasifanye mkutano wakidai haukuwa na
baraka za jeshi hilo.
Mnyika
alisema polisi hao walisema sababu ya kuuzuia mkutano huo ni uwepo wa ziara ya
Makamu wa Rais katika Wilaya ya Kinondoni, hivyo walikuwa wameelekeza nguvu zao
katika ziara hiyo, kwamba hawakuwa na uwezo wa kuulinda mkutano wa CHADEMA.
“Nikiwa
nimejiandaa kupanda jukwaani ndiyo polisi walikuja kusema tuache tusifanye
mkutano, nilisogea karibu na gari kumlalamikia ofisa wa polisi kwani kitendo
cha kuahirisha mkutano kwa barua waliyoileta saa sita mchana siku ya mkutano
wakati sisi tuliwapa taarifa siku nne zilizopita ilikuwa sio haki.
“Nilimwambia
ofisa huyo wa polisi kuwa nilikuwa najadiliana kwa simu na viongozi wakuu wa
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Inspekta Jenerali wa Polisi
Said Mwema kumlaumu kutumika vibaya kwa Jeshi la Polisi.
“Nilipokuwa
bado najibizana naye bila fujo zozote, bomu lilirushwa kutoka ndani ya gari ya
polisi na kupita karibu na mimi likamjeruhi mtu aliyekuwa karibu yangu, ki
ukweli nimeshangazwa sana na matumizi mabaya ya silaha za moto,” alisema.
Aliongeza
kuwa katika purukushani zilizotokea baada ya bomu kupigwa, alipoteza nyaraka
mbalimbali alizokuwa amebeba kama ushahidi kuwaonyesha wafuasi wa chama hicho
hasa jinsi serikali ya CCM na wabunge wake walivyopitisha kodi ya huduma za
simu, na kodi ya laini za simu.
Slaa anena
Aidha
katika mkutano huo ambao awali ulitangazwa kuwa ungehutubiwa na Katibu Mkuu wa
chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, haukuweza kuhutubiwa naye kwa kile alichosema
kuwa watu wake wa usalama walimwambia mapema hali si salama kwenye mkutano huo.
“Nilipata
taarifa kutoka vyanzo vyangu kuwa polisi walikuwa na mpango wa kuleta fujo,
hivyo nikaona kwa kuwa wanatuwinda nisingeenda kuhutubia, pengine bomu
lililomkosa Mnyika lilikusudiwa kwangu au kwa mwingine,” alisema Dk. Slaa
alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu baada ya kutoonekana mkutanoni.
Jeshi
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana liliahirisha mkutano huo wa
CHADEMA kabla viongozi hao kupanda jukwaani. Liliwapelekea
barua ya zuio CHADEMA inayosomeka: “Kumbuka barua ya tarehe 17 Julai, yenye
kumb. CHADEMA/MKT/UBUN/015/2013 uliyomwandikia Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu
Dar es Salaam. Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam amezuia
kufanyika kwa mkutano huo tarehe 21 Julai 2013 katika viwanja vya Sahara,
Mabibo kwa sababu siku mliyoomba kufanya mkutano wenu wa hadhara, Wilaya ya
Kinondoni ina mapokezi ya ugeni wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.”
Hata
hivyo Mnyika alipinga sababu hiyo ya polisi kwa madai CHADEMA wamepeleka
taarifa kwa Jeshi la Polisi tangu Julai 17 kwamba wangefanya mkutano katika
viwanja hivyo Julai 21, lakini jeshi hilo halikuwajibu hadi walipokuwa wanaenda
mkutanoni.
CHADEMA wabadili mbinu
Kutokana
na kuzuiwa kufanya mkutano kwenye viwanja vya Sahara, CHADEMA waliamua
kuufanyia Ubungo kutokana na kuomba vibali viwili kwenye maeneo tofauti.
Baada
ya kuzuiliwa Mabibo, kibali cha Ubungo kilikuwa halali, hivyo Mbunge wa Ubungo
aliyekuwa amefika Sahara kwa ajili ya kuhutubia, aliandamana kwa miguu na
wafuasi wa chama hicho hadi Ubungo, huku kukiwa na makachero wengi wa polisi
waliofuatilia maandamano hayo.
Akizungumza
na wananchi katika mkutano uliofanyika Ubungo, Mnyika alisema polisi walifanya
kitendo cha kikatili, kusubiri watu wamalize maandalizi, wakusanyike uwanjani
ndipo wanaleta barua ya kupiga marufuku mkutano kwa kisingizio kuwa katika
Wilaya ya Kinondoni kulikuwa na ziara ya makamu wa Rais katika Jimbo la Kawe na
Kindondoni.
“Sisi
tupo Ubungo, Makamu wa Rais yupo Kawe na Kinondoni, sasa suala la kuzuia
mikutano isifanyike lilikuwa na maana gani? Kama Jeshi la Polisi walisema
hawana askari wa kutosha kulinda mkutano wetu mbona katika kuutawanya wamekuja
na magari matatu?” alihoji.
Mnyika
alitumia muda mwingi kulilaumu Jeshi la Polisi, kwanza kwa kuahirisha mkutano
muda mfupi kabla ya viongozi kupanda jukwaani, lakini pia kitendo cha kurushwa
bomu mahali ambapo hakukuwepo fujo zozote.
Madudu zaidi ya CCM
Mwenyekiti
wa CHADEMA, Freeman Mbowe ameendelea kuanika madudu ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), safari hii akitoa nyaraka za mikakati ya chama hicho tawala kufundisha
vijana kukabiliana na wapinzani.
Akihutubia
mkutano wa hadhara juzi katika Viwanja vya Mahakama ya Mwanzo, Nguzo Nane,
mjini Shinyanga, Mbowe alisema kuwa ili kujilinda dhidi ya vitendo alivyodai
wanafanyiwa na vijana wa Green Guards - kikosi cha vijana wa CCM, chama chao
kitaendelea na mipango ya kuwapatia vijana wao mafunzo ya ukakamavu.
Mbowe
alionyesha nyaraka mbili za CCM zinazoonyesha kuwa chama hicho tawala kupitia
wanachama wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) kimekuwa kikitoa mafunzo ya ukakamavu
kwa vijana wake, huku nyaraka moja ikionyesha kuwa moja ya malengo ya mafunzo
hayo ni kukabiliana na upinzani.
“Tunashambuliwa,
watu wetu wanapigwa, wanateswa, wanatekwa na wengine kuuawa, kwa sababu tu
wanataka mabadiliko na wanapenda CHADEMA, majuzi mlisikia Waziri Mkuu Pinda
anasema wamechoka...sasa tunasema Pinda kama umechoka ondoka upishe ofisi ya
umma hiyo, upishe kwenye ofisi ya watu kama umechoka, maana kuchoka huko ni
kuchoka kwa CCM. Pisheni ofisi sio za kwenu hizo, ni za Watanzania.
“Wananchi
hapa mkononi nimeshika nyaraka mbili za CCM, moja ni cheti cha kuhitimu mafunzo
na nyingine hapa juu imeandikwa ‘Sera za Msingi za CCM’, sasa mi sitawasomea,
naomba aje hapa jukwaani mtu yeyote anayejua kusoma, awasomee mjue tunaposema
CCM wamekuwa na kikundi kinachoshambulia, kupiga, kutesa, kuteka na hata kuua
Watanzania wenzao eti tu kwa sababu wanaunga mkono CHADEMA, huwa tunamaanisha
nini,” alisema Mbowe.
Mmoja
wa wananchi aliyehudhuria mkutano huo wa hadhara, ambao ulikuwa ni sehemu ya
shughuli za ukamilishaji wa kuzindua Kanda ya Ziwa Mashariki (mikoa ya
Shinyanga, Simiyu na Mara), alipewa kabrasha kubwa na kusoma sehemu
inayozungumzia majukumu ya jumuiya za chama hicho.
Gazeti
hili pia lilifanikiwa kuona kabrasha hilo kwa karibu, ambapo kifungu cha 9.1
kinachozungumzia UVCCM, kinasomeka hivi;
“(i)
Umoja wa vijana wa CCM unapaswa kuwajenga vijana katika itikadi, ukakamavu na
mafunzo yatakayowafanya wajiamini, wawe vijana wenye ari ya kutimiza wajibu wao
wakiwa walinzi wa chama, viongozi na wagombea wa CCM.
“(i)
Utaratibu wa kuandaa makambi ya vijana usimamiwe kwa dhati. Chama kiwe na
mipango mizuri ya kutafuta na kuwateua wakufunzi watakaofaa kuwapatia vijana
mwelekeo unaotakiwa ikiwa ni pamoja na elimu ya uchaguzi/uraia. Mafunzo ya
makambi ya vijana, mbali ya kujifunza nyimbo za hamasa yatilie mkazo pia
mafunzo ya ukakamavu kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya kihuni vya baadhi
ya vijana wa vyama vya upinzani.”
Mbowe
pia aliwaonyesha wananchi waliofurika kwenye mkutano huo cheti cha mmoja wa
watu waliohitimu mafunzo ya makambi ya vijana wa CCM ambacho kilionyesha
mhusika alianza mafunzo Juni 27, 2009 na kumaliza Julai 4, 2009, mkoani Dodoma.
Cheti
hicho kimesainiwa na watu wawili, mmoja mwenye jina la Jumanne Kitundu, akiwa
na nafasi ya Katibu wa UVCCM, Dodoma mjini na mwingine, Robert Mwinje,
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Wilaya ya Dodoma mjini.
Cheti
hicho kinaonyesha mhusika (jina linahifadhiwa) alihitimu mafunzo ya masomo ya
kanuni ya umoja wa vijana, wajibu wa vijana katika chama, ulinzi na usalama,
ujasiriamali, ukakamavu, wajibu wa vijana katika uchaguzi, rushwa, ukimwi,
historia ya TANU na ASP pamoja na maadili.
Msimamo wa CHADEMA
Mbowe
alisitiza kuwa CHADEMA kitasimamia azimio la kikao cha Kamati Kuu ya chama
hicho juu ya kuimarisha kitengo chake cha ulinzi na usalama ikiwemo kuanzisha
makambi ya mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wa chama hicho watakaokuwa na jukumu
la kulinda viongozi wao.
Ingawa
msimamo huo umekuwa ukipingwa na wadau mbalimbali likiwemo Jeshi la Polisi,
Msajili wa Vyama vya Siasa na CCM, Mbowe amesisitiza kuwa hawatarudi nyuma juu
ya mpango huo utakaoimarisha ulinzi.
Kodi ya laini za simu
Hoja
ya tozo ya simu imekuwa ajenda kubwa kwenye mikutano iliyofanywa na viongozi
mbalimbali wa CHADEMA.
Mwenyekiti
wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), John Heche alisema kama wananchi
wasingeipa ushirikiano CHADEMA na kupinga maovu mbalimbali, CCM ingekuwa
imeshauza nchi na wananchi wake.
Alisema
tozo la laini za simu lilipitishwa wakati wabunge wa CHADEMA walipokwenda
Arusha kushiriki maombolezo na mazishi ya marehemu wa tukio la bomu, hivyo
serikali ikaona ipeleke jambo hilo lililobarikiwa na wabunge wengi wa CCM.
“Maana
yake ni nini? Kodi hii kwanza mwananchi maskini kabisa ambaye amedunduliza na
kununua simu, atakuwa analipa sawa sawa na matajiri wakubwa, yaani wewe hapa
utakuwa unalipa kodi sawa na Reginald Mengi...lakini kama hiyo haitoshi,
ukipiga mahesabu utakuwa unalipa kodi takriban shilingi 12,000 kwa mwaka.
“Serikali
hii ya CCM inayowaletea kodi ya sh 12,000 kwa mwaka ndiyo ililazimika kuondoa
na kufuta kodi ya kichwa, baada ya CHADEMA kuwa imefanya hivyo kwenye
halmashauri zake, kwa kuanza na Hai ambako Mwenyekiti Mbowe alikuwa ni mbunge
na Karatu kwa Dk. Slaa. Sasa walifuta kodi ya manyanyaso ya kichwa kwa
maelekezo ya CHADEMA iliyokuwa sh 3,000 kwa mwaka, ambapo watu walikuwa
wanakimbia nyumba na kujificha maporini, wengine wakaliwa na wanyama, sasa
wanataka mlipe kimya kimya, sh 12,000 kwa mwaka. Ni matokeo ya kushindwa kwa
sera za CCM,” alisema Heche.
Mkutano wa Geita
Wabunge
wa CHADEMA wanaotoka Kanda ya Ziwa na viongozi wa chama hicho nao waliendelea
kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali huku wakilalamikia tozo la laini za
simu pamoja na mapendezo ya rasimu ya katiba mpya yaliyotolewa na CCM hivi
karibuni yakipinga mambo mengi yaliyopendezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Jana,
wabunge hao wa viongozi walifanya mikutano ya hadhara katika mji wa Kasamwa
huko Geita na Sengerema mkoani Mwanza ambako walisema CCM imekosa sifa ya
kuongoza ndiyo maana maisha ya Watanzania yamezidi kuwa magumu kadiri siku
zinavyokwenda mbele.
Wabunge
hao pamoja na viongozi na makada wa CHADEMA ambao wapo kwenye msafara wa
kuimarisha chama katika kanda hiyo, ni pamoja na Ezekiel Wenje (Mbunge wa
Nyamagana), Profesa Kulikoyela Kahigi (Bukombe), Dk. Anthony Mbasa (Biharamulo
Magharibi) na Conchesta Rwamlaza (Viti Maalumu – Kagera).
Viongozi
na makada wengine ni pamoja na mjumbe wa Baraza Kanda ya Ziwa Magharibi, Anwar
Kashaga, katibu wa CHADEMA Manispaa ya Bukoba, Lenatus Kilongozi pamoja na
Mwenyekiti wa Wilaya ya Biharamulo Magharibi, George Kasaiza.
Akizungumza
kwenye mikutano hiyo, Wenje alisema CHADEMA inatarajia kuunda mabaraza ya
wananchi kuhusu muundo wa serikali tatu, na wanatarajia kukusanya saini za
Watanzania kupinga tozo ya kodi mpya ya laini za simu iliyopitishwa hivi
karibuni bungeni.
Alisema
kwa sasa CCM wametoa mapendekezo ya kutaka kusiwepo uwazi wa mikataba, maadili
ya umma na haki za binadamu kwenye katiba mpya, na inataka Spika wa Bunge
lazima atokane na mbunge, jambo aliloliita ni kuendeleza ukandamizaji kwa
wananchi.
“Wakati
CHADEMA tunataka spika na mawaziri wasitokane na wabunge, CCM wao wamependekeza
viongozi hao watokane na wabunge ili waendelee kuwakandamiza Watanzania.
CHADEMA tunataka nchi iwe na mawaziri saba tu, na siyo 15 wa pendekezo la tume
na 64 waliopo sasa.
“Si
hilo tu, ibara ya 22 hadi 23 ya rasimu ya katiba mpya, CCM kwa mapendekezo yao
wanataka haki za binadamu zisiwepo kwenye katiba mpya ijayo, bali ziwepo kwenye
sheria tu. CCM haitaki kuwepo malengo ya taifa kwenye katiba mpya!
“Tutakusanya
saini milioni 10 za wananchi kuhusu mapendekezo ya katiba mpya. Pia tutakusanya
saini milioni tano za wananchi kutaka tozo ya laini za simu ifutwe,” alisema
Wenje huku akisisitiza uundwaji wa serikali tatu; Tanganyika, Zanzibar na
Shirikisho.Mbunge wa Biharamuro Magharibi, Dk. Mbasa, mbunge Conchesta, Katibu
wa CHADEMA Manispaa ya Bukoba, mjumbe wa Baraza Kanda ya Ziwa Magharibi, Anwar
pamoja na mwenyekiti wa chama hicho Biharamulo Magharibi, Kasaiza waliishutumu
serikali kwa kushindwa kuwaondolea umasikini wananchi wake.
Walisema
kwa sasa Watanzania walio wengi wanalazimika kuvaa viatu vya ‘yebo yebo’ kwa
sababu ya umasikini unaotokana na kushindwa kwa Serikali ya CCM kuwatumikia
wananchi wake kwa kuwanufaisha na rasilimali zilizopo hapa nchini.
“Serikali
ya chama tawala imekosa sifa ya kuwaongoza wananchi. Tunahitaji tuungane wote
kuiondoa CCM mwaka 2015. CHADEMA ni mkombozi wa Watanzania na ndiyo maana
wabunge na viongozi wake wanapambana usiku na mchana kutwa kupigania maendeleo
ya wananchi,” alisema Dk. Mbasa.
No comments:
Post a Comment